BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

OBAMA RAHA, KARAHA.

ZIARA ya Rais wa Marekani, Barack Obama, imezidi kuwaweka njia panda wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, baada ya Serikali kuwataka wakazi wa jiji hilo, ambao hawana shughuli muhimu, kutofika maeneo ya katikati ya mjini kuanzia Jumamosi wiki hii.

Kauli ya Serikali, ilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, wakati alikihojiwa na Redio Clouds FM, kuhusu manufaa ya ujio wa viongozi wakubwa duniani nchini Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Membe amewataka Watanzania ambao hawana shughuli za lazima katika maeneo ya katikati ya jiji pamoja na eneo la Ubungo, kubaki nyumbani muda wote ambao Rais Obama atakuwa nchini.

“Natumia fursa hii, kuwaomba Watanzania ambao hawana shughuli za lazima katikati ya Jiji la Dar es Salaam wab

aki majumbani mwao, kwa kipindi chote cha uwapo wa Rais Obama nchini,” alisema Membe.

Alisema kutokana na mfumo wa ulinzi wa Marekani, kuna uwezekano mkubwa wa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, wakazuiliwa kufika mjini na eneo la Ubungo ambako Rais Obama atatembelea.

Kuhusu ziara hiyo, Waziri Membe alisema: “Ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kuweza kujitangaza kimataifa kwa kuvutia uwekezaji wa kiuchumi pamoja na utalii ambao unaweza kuchangia pato kubwa la taifa.

“Nachukua fursa hii, kuwaasa Watanzania wawe makini wakati dunia itakapokuwa hapa, tuwe wavumilivu katika siku hizo mbili ili dunia iweze kuondoka salama katika ardhi yetu ya Tanzania.

“Hii ni fursa ambayo ni adhimu sana, kila Mtanzania anapaswa kuwa mlinzi, toeni taarifa pale mnapoona kuna jambo lisilokuwa la kawaida, naomba tuionyeshe dunia kwamba sisi ni wastaarabu, sitarajii kuwepo chokochoko za aina yoyote kwa kisingizio chochote,” alisema Membe.

Hata hivyo, alipoulizwa, kwa nini Serikali isitangaze siku ambayo Rais Obama atakuwa nchini kuwa siku maalum ya mapumziko ili kuondoa mkanganyiko na usumbufu utakaojitokeza, Membe alisema hilo si jukumu lake kulizungumzia.

Alisema kutokana na ugeni huo mzito, Tanzania imetoa mwaliko kwa marais wote wa Jumuia ya Afrika Mashariki kuja Tanzania kushiriki ziara ya Obama, lakini hadi sasa hakuna aliyethibitisha.

Alipoulizwa kama Rais wa Rwanda, Paul Kagame amealikwa, Waziri Membe alisema: “Ndiyo, Kagame amealikwa kuja Tanzania kushiriki ziara hii ya kihistoria.

“Hili liko wazi, tulitoa mwaliko tangu  Februari, mwaka huu kwa marais wote wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuja kushiriki nasi kumpokea Rais Obama, mpaka sasa hatujapokea majibu rais gani atakuja, lakini tunawakaribisha hata kwa dharura… nachukua fursa hii kutoa wito kwa Rais Kagame kama anaweza kuja afike, tunamkaribisha sana,” alisema Membe.

Tanzania imepata fursa ya kutembelewa na marais wawili wa taifa lenye nguvu zaidi duniani. Mara ya kwanza Tanzania ilitembelewa na Rais mstaafu wa  Marekani, Bill Clinton, Agosti 28 hadi 29, 2000, akifuatiwa na Rais mwingine mstaafu, George W. Bush, alitembelea Tanzania mwaka 2008.

Gari za usafi zatanda mjini

Wakati huo huo, makampuni ya usafi katikati ya Jiji la Dar es Salaam yamekuwa yakihaha kufanya usafi katika maeneo mbalimbali.

Wengi wa wafanyakazi wa kampuni hizo, walionekana kuwa na vifaa vipya na mavazi nadhifu tofauti na siku zote.

Magari ya usafi yameonekana kuwa mengi nyakati za mchana, huku yakikusanya kila aina ya uchafu. Katika hali ya sasa hata maganda ya machungwa na maji huwezi kuyaona.

POLISI

Idadi ya askari wanaofanya doria katika eneo la katikati ya jiji na kandokando ya Barabara ya Nyerere ni kubwa kana kwamba wanajiandaa kufanya operesheni maalumu.

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambao wana silaha wamekuwa wakizunguka mitaa mbalimbali tofauti na siku zote.

KOVA ANENA

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limejipanga kuimarisha ulinzi katika ziara ya Obama na limezuia maandamano ya CUF ambayo waliomba kufanya Juni 29, mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalamu ya Dar es Salaam, Suleimani Kova,  alisema barua ya CUF haikuambatanishwa na barua yoyote kutoka Ikulu inayothibitisha kuwa Rais Jakaya Kikwete au wasaidizi wake, wapo tayari kupokea maandamano hayo.

“Hatutaruhusu maandamano ya aina yoyote, mabango, makundi yasiyokuwa na tija na aina yoyote ya uvunjifu wa amani kwa kipindi hiki tutakapokuwa na ugeni katika nchi yetu.

“Ni sifa kubwa kwa Taifa kama Tanzania kutumia fursa hii kutangaza jina la nchi yetu katika mataifa mbalimbali duniani, endapo tutadumisha amani, utulivu na ushirikiano wa hali na mali kwa wageni wetu.

“Tunatarajia ziara ya kiserikali Julai 1-2 ya Rais Obama na ujumbe wake, hivyo maandamano yao yataingilia maandalizi ya ziara hiyo, hata hivyo barabara wanayotarajia kutumia, Buguruni Petrol Station kupitia Barabara ya Uhuru ndiyo hiyo itaingiliana na misafara ya marais 14 na viongozi wakuu watakaokuja nchini katika mkutano wa Smart Partnership Dialogue (SPD),” alisema Kamishna Kova.

Alisema Jeshi la Polisi limepata taarifa za kuaminika kuwa kuna chama cha siasa na taasisi ambazo zimejiandaa kusambaza vipeperushi au kujitokeza na mabango ghafla barabarani wakati wa ujio wa Rais Obama wa Marekani, kitendo ambacho ni kinyume cha taratibu za usalama. CHANZO MTANZANIA.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: