DAR ES SALAAM.
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu amesema atazungumzia hatima yake baada ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Gazeti la The Citizen,
lilimkariri Pinda jana akisema kwa sasa anahitaji amani na utulivu
katika kipindi hiki cha sikukuu baada ya shughuli za kikao kilichopita
cha Bunge.
Katika kikao hicho, mawaziri wanne walitimuliwa
baada ya ripoti ya kamati ndogo ya Bunge kufichua madhara yaliyojitokeza
wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Wabunge kadhaa walishinikiza kujiuzulu kwa Pinda
na mawaziri wengine, ambao wizara zao zilihusika katika utekelezaji wa
operesheni hiyo.
“Baada ya kikao cha Bunge Dodoma nilikwenda likizo
kuwasalimia wazazi wangu. Wasiliana na mimi baada ya likizo halafu
niulize maswali yako yote nitakujibu,” alisema Pinda, ambaye yuko katika
Kijiji cha Kibaoni, Mkoa wa Katavi.
Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa mawaziri
Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya
Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Dk
David Mathayo(Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo), baada ya malalamiko ya
wabunge.
Pinda alikiri bungeni kuwa operesheni hiyo ilikuwa
na matatizo na wale wote waliokuwa na dhamana walikiuka taratibu za
utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.
Pamoja na kujiuzulu kwa mawaziri hao, pia Serikali itaunda tume, ambayo itaongozwa na Jaji ili kuchunguza sakata hilo undani.
Kakobe amfagilia Pinda
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospal Bible
Fellowship, Zacharia Kakobe amemtetea Pinda kwa kumwelezea kuwa ni
kiongozi shujaa katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka 2013.
Pia, Kakobe amesema Waziri Pinda ana sifa zote za
mtu anayefaa kuwa kiongozi, kwani ana moyo wa kishujaa licha ya kupata
misukosuko akiwa kwenye nafasi yake ya uwaziri mkuu.
Akizungumza kwenye ibada ya Sikukuu ya Krismasi,
Askofu Kakobe alisema: “Kati ya viongozi waliopo nchini mimi anaweza
kusema kuwa Pinda ni kiongozi shujaa, kwani ametamka maneno mazito akiwa
bungeni ambayo hadhani kama kuna kiongozi anaweza kuyatamka.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment