HIKI NDICHO KILICHOSEMWA NA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA, YATOA TAHADHARI KWA MVUA ZA MWAKA 2014, UGONJWA WA KIPINDUPINDU CHATAJWA KUIBUKA.
Na Joachim Mushi
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa tahadhari kwa Mamlaka za miji Vipindi vya mvua kubwa zitakazonyesha kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2014 vinaweza kusababisha mafuriko endapo miundombinu ya maji taka (mitalo) haita safishwa kuhakikisha maji yanapita pasipo kutuama.
TMA imesema maeneo ambayo huenda yakaathiriwa zaidi ni yale ambayo yanatarajiwa kupata mvua chini ya wastani; yakiwemo maeneo ya mikoa ya Tabora, Rukwa, Katavi na Kusini mwa Mkoa wa Kigoma.
Akizungumzia leo jijini Dar es Salaam kuzungumzia utabiri wa hali ya hewa kiujumla na mwelekeo mvua za msimu wa kuanzia mwezi Januari hadi Machi, 2014, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agness Kijazi amezitahadharisha mamlaka za manispaa na miji katika maeneo hayo kuchukua tahadhari ili kuepuka maafa zaidi yanayoweza kusababishwa na mvua hizo.
Dk. Kijazi aliyataja maeneo mengine ambayo yanaweza kuathiriwa na mvua hizo kuwa ni pamoja na maeneo ya mwagharibi mwa Mkoa wa Mbeya, Mkoa wa Lindi na Kaskazini mwa Mkoa wa Lindi, maeneo ya kati na magharibi mwa Tanzania.
“…Hivyo mamlaka za manispaa na miji zinashauriwa kusafisha mitalo ya maji taka ili kuepusha kutuama kwa maji na kusababisha mafuriko.
Kuna uwezekano wa kuwepo kwa magonjwa ya mlipuko kama vile malaria na kipindupindu katika maeneo mbalimbali nchini. Hivyo hatua za tahadhari zichukuliwe..,” alisema Dk. Kijazi.
Alisema vipimo vya mifumo ya hali ya hewa vinaonesha kuwa mvua kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi, 2014 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya kusini mwa nchi na wastani hadi chini ya wastani katika maeneo ya kati na magharibi mwa nchi.
Aidha alisema maeneo ya Nyanda za juu Kusini Magharibi; Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajia kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani-huku maeneo ya mikoa ya Iringa, Njombe, kusini mwa Morogoro na mashariki mwa mkoa wa Mbeya yakipata kiwango kile kile cha mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“…Kanda ya kusini na Pwani ya kusini (Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi); Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu wastani isipokuwa kaskazini mwa mkoa wa Lindi ambapo mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.” Alisema Dk. Kijazi.
Aliongeza kuwa kwa maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za juu ya wastani kuna wezekano wa kupata mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa miundombinu hivyo kuvitaka vitengo vingine vya maafa kuchukua tahadhari ili kukabiliana na hali hiyo endapo itajitokeza.
“Kamati za maafa kwenye vituo vya kitaifa vinazoshughulikia maafa zinashauriwa kuchukua hatua muafaka zitakazokabiliana na athari zitokanazo na utabiri huu.
Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua juu ya wastani yanauwezekano wa kupata mafuriko, mmomonyoko wa ardhi na uharibifu wa miundombinu. Hata hivyo maeneo yanayopata mvua chini ya wastani yanatarajiwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata uhaba wa chakula,” alifafanua Dk. Kijazi.
“Kuimarika kwa mgandamizo mkubwa wa hewa katika maeneo ya Siberia kunatarajiwa kusababisha upepo usio na unyevunyevu kutoka kaskazini-mashariki kuelekea maeneo mengi ya nchi.
Uwezekano wa kuongezeka kwa joto la baharí katika eneo la kusini-magharibi mwa baharí ya Hindi katika ya mwezi Januari hadi Machi 2014 kunatarajiwa kusababisha uwezekano wa kutokea kwa vimbunga katika baharí ya Hindi.
Vilevile, kwa kipindi hiki kuwepo wa upepo kutoka magharibi unatarajiwa katika meneo mengi ya nchi kutokana na kupunguwa kwa joto katika baharí ya Atlantiki.”
Hata hivyo aliongeza kuwa; kuwepo kwa vimbunga katika bahari ya Hindi kunaweza kusababisha mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa, hivyo mamlaka ya Hali ya Hewa itaendelea kufuatilia mifumo na mienendo ya hali ya hewa na kutoa taarifa na ushauri kila itakapobidi.
TMA inatarajia kutoa utabiri mwingine wa mvua za masika katika maeneo hayo mwishoni mwa mwezi Februari, 2014.
0 comments:
Post a Comment