Amesema kwamba, pamoja na kwamba Tanzania ni kati ya nchi zinazojali misingi ya haki za binadamu, baadhi ya viongozi wake wamekuwa wakikiuka misingi kwa kutowatendea haki wananchi.
Padri Mapunda alitoa kauli hiyo jana, alipokuwa akihubiri katika misa ya Familia Takatifu kwenye Kanisa Kuu la Kiaskofu la Mtakatifu Mathias Mulumba Kalemba, Jimbo Kuu la Songea.
"Utawala huu sasa unafanana na ule wa Mfalme Herode, ambaye utawala wake ulikuwa ukiendesha vitendo vya mauaji kama ilivyo hapa ambapo Serikali inashindwa kufuata utawala wa haki na imekuwa ikikiuka misingi ya haki za binadamu," alisema Padri Mapunda.
Katika mahubiri yake, aliitolea mfano Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo hivi karibuni ilisababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu kwa kuwa iliendeshwa kinyume cha utaratibu.
"Hivi karibuni, Serikali ilisimamia Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo ilionekana kukiuka haki za binadamu, kwani Watanzania walio wengi wakiwemo wakulima na wafugaji, walifanyiwa vitendo vya kinyama.
"Wakati wa Operesheni Tokomeza Ujangili, wananchi walinyanyaswa kwa namna mbalimbali na wengine waliuawa na wengine waliharibiwa mali na kupata ulemavu wa kudumu.
"Unyama huo ndio ulileta mtafaruku kwa Watanzania na kupelekea Rais Jakaya Kikwete kufikia uamuzi mgumu wa kutengua uteuzi wa mawaziri wake wanne.
"Vitendo hivyo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, vinaashiria kuwakatisha tamaa wananchi katika maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao," alisema Padri Mapunda.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kuwa makini wakati wote huku akiwataka pia waandishi wa habari kuchukua tahadhari kutokana na habari za kweli wanazoziandika, ingawa zinaichukiza Serikali.
Kuhusu biashara ya dawa za kulevya, alisema Serikali inatakiwa kutaja watu wanaofanya biashara hiyo badala ya kuendelea kukaa kimya, wakati vijana wakiendelea kuathiriwa na dawa hizo.
"Inashangaza kuona kwamba, pamoja na Serikali kuwa na mkono mrefu, bado imeshindwa kuwataja watuhumiwa wa dawa za kulevya, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
"Badala yake, imewaacha wakiendelea kufanya biashara hiyo ambayo inaathiri vizazi hadi vizazi, hili siyo jambo zuri hata kidogo. Chanzo: MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment