DAR ES SALAAM.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimemtupia mpira Rais Jakaya Kikwete wa kuamua hatima ya mawaziri saba, wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mawaziri hao waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali
juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM chini ya
Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
chama hicho, Nape Nnauye alisema wamemshauri Rais Kikwete mambo matatu;
kuwafukuza, kuwahamisha wizara au kuwahimiza wafanye kazi.
“Kamati Kuu imetoa maazimio saba ambayo yote
yanazihusu wizara saba zinazoongozwa na mawaziri hao. Tumemshauri Rais
Kikwete, yeye ndiye ataamua nini cha kufanya kwa sababu ndiye
aliyewateuwa mawaziri hao,” alisema Nape.
Wakiwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika
ziara ya chama hicho, Nape pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulrahman Kinana aliwatupia lawama mawaziri hao wakati wakielezea
changamoto zinazowakabili wakulima ambao ni asilimia 80 ya Watanzania,
huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Nape alisema mawaziri hao waliitwa kuhojiwa na
kutakiwa kutoa maelezo ya masuala yaliyoibuliwa wakati wa ziara hiyo
ambayo pia iliwahusisha baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari jana,
Nape aliwataja mawaziri hao kuwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika
Christopher Chiza, Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya (alihojiwa kwa
niaba ya Waziri wa Fedha Dk William Mgimwa).
Wengine ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk
Abdallah Kigoda, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo
David, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma,
Celina Kombani na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Sakata la kutaka mawaziri ‘mizigo’ kutoswa
limekuwa likiibuliwa na wabunge mbalimbali katika mikutano ya Bunge
mjini Dodoma, huku baadhi wakipendekeza hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
naye atoswe kutokana na kushindwa kuwasimamia mawaziri.
Ushauri wa CCM kwa JK
Nape alisema kuwa kazi ya Kamati Kuu ni kushauri,
“Kazi yetu ni kushauri na siyo kufukuza. Rais Kikwete ndiye amewateua
mawaziri hao, ameupokea ushauri na yeye ndiye mwenye uwezo wa
kuwafukuza, kuwahamisha au kuwasukuma watende kazi. Hiyo siyo kazi yetu”
Alipobanwa zaidi kueleza ushauri ambao Kamati Kuu
ilimpa Rais Kikwete Nape alisema, “Kuna ushauri mwingine ambao tumempa
Rais Kikwete hatuwezi kuuweka hadharani.”
Alisema kuwa wakati wa kuhojiwa kila waziri
alikuja na majibu yanayoihusu wizara yake kutokana na udhaifu ulioelezwa
na wananchi. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment