DAR ES SALAAM.
UNAWEZA kusema sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula kusema kuwa wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015 watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini;
“Wapo watu wanataka waichanechane CCM kwa sababu
ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata urais. Kuna
makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe hatuwezi
kuyafumbia macho.”
Akifafanua hilo Mangula alisema: “Tutawaita wote
walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwanini wanafanya
hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza katika mikutano
wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu,
tunajua dhamira yao ni nini.”
Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja
tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kusema
mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda
mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya Lowassa siku mbili
zilizopita, kutangaza nia ‘kimtindo’ akisema anaanza rasmi safari
aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za
Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa
wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,
alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya,
katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa
Monduli.
Mangula aliwashukia vigogo wa chama hicho
wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati ya
Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa salamu
za mwaka mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.
Ataja kanuni za uongozi
Katika mkutano huo Mangula alisaidiwa kusoma
kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea ufafanuzi mambo
mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa CCM na
wanachama taifa, Masoud Mbengula.
Moja ya kanuni hizo inasema “Ni mwiko kwa kiongozi
wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au eneo
analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye
mwenyewe ama mgombea anayemuunga mkono.”
Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za chama
hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa msaliti na
hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza chama wakati
wowote. MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment