KLABU YA YANGA KUJITOA KOMBE LA MAPINDUZI NI UHUNI MTUPU.
MWANZONI mwa wiki hii mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga walitangaza kujitoa kwenye michuano ya Kombe la mapinduzi inayoendelea Zanzibar na Pemba.
Awali, kabla ya kujitoa, Yanga ilikaririwa kuwa haijapata barua rasmi kutoka kwa waandaaji, hivyo inawawia vigumu kuzungumzia michuano hiyo na siku ambayo timu yao itakwenda Zanzibar kushiriki.
Kauli ambayo baadaye ilikanushwa na msemaji wa Kamati ya Maandalizi ya michuano hiyo, Farouk Karim aliyesema kwamba kila timu ilipewa barua na taratibu za michuano hiyo.
Hata hivyo, siku chache baada ya Yanga kudai haina barua rasmi ya kualikwa kushiriki michuano hiyo, ilitoa taarifa ya kujitoa kwa vile haina benchi la ufundi baada ya kuvunja benchi lake lote.
Tunapata shida kufikiria sababu za Yanga kuamua kufanya 'uhuni' huo katika michuano kama hiyo ambayo sasa imekuwa mikubwa tangu ilipoanzishwa mwaka 2002.
Hii sio mara ya kwanza kwa Yanga kufanya tukio la 'kihuni' kwenye michuano hiyo, mwaka jana ilipeleka timu B kinyume na ilivyoelekezwa kwenye michuano hiyo, matokeo yake wakaenguliwa.
Licha ya kwamba bingwa wa michuano hiyo haendi popote lakini ilikuwa na umuhimu wake katika kujenga uhusiano mzuri kwa timu shiriki.
Tunaona Yanga ilikuwa muhimu kushiriki michuano ya mwaka huu, hasa kwa vile yenyewe itacheza michuano ya kimataifa, hivyo kwa mchanganyiko na timu kutoka Uganda na Kenya, ingekuwa ni maandalizi tosha kwa wawakilishi hao wa Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Sababu za Yanga kwamba hawana benchi la ufundi hazina mashiko, kwasababu alipoondolewa kocha mkuu Ernie Brandts timu ilikuwa chini ya Fred Minziro, ingeweza kufanya mawili, ama timu iende chini ya Manziro, au iende na kocha mpya msaidizi Charles Mkwasa, ambaye mpaka Yanga inatangaza kutoshiriki michuano hiyo, tayari alikuwa ameshamalizana nao.
Katika historia ya Yanga, haiwezi kuikwepa Zanzibar, Rais wake Abeid Amaan Karume alikuwa shabiki mkubwa wa timu hiyo ya Jangwani, akitoa mchango mkubwa katika kujenga jengo la klabu hiyo Mtaa wa Twiga na Jangwani, jengo ambalo mpaka leo klabu hiyo inajivunia.
Sasa iweje basi klabu hiyo ishindwe japo kukumbuka hilo, na kumfariji marehemu Karume kwa kushiriki michuano hiyo?
Tunadhani ipo haja kwa viongozi wa Yanga kujiangalia upya, na kuona kwamba kuna mambo ya kufanyia mzaha na kuingiza siasa za mpira, lakini pia kuna mambo wanatakiwa kuyafanya licha ya kutowaingizia faida yoyote, lakini kwa kuenzi na kukumbuka mchango kwa viongozi waliotangulia kwao. HABARALEO.
0 comments:
Post a Comment