HIKI NDICHO KILICHOWABAKIZA MAWAZIRI MIZIGO KATIKA SERIKALI YA RAIS JAKAYA KIKWETE.
RAIS JAKAYA KIKWETE.
SERIKALI imetoa kauli kuhusu tuhuma zilizokuwa zikiwakabili baadhi ya mawaziri, waliobatizwa jina la ‘Mawaziri Mizigo’, na hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa kukabiliana na kero zilizosababisha wapewe jina hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Ikulu Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Safue, alisema mawaziri hao walituhumiwa kutokana na changamoto zilizopo katika wizara zao; na si upungufu wao binafsi kama viongozi.
Mawaziri hao saba walitajwa katika ziara ya mikoani ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na baadae walihojiwa katika kikao cha Kamati Kuu cha chama hicho.
Baada ya kuhojiwa, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema Kamati Kuu ilimuachia Rais Kikwete jukumu la kuamua kuwafukuza kazi, kuwahamisha au kuwataka kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Miongoni mwa mawaziri waliohojiwa ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Fedha.
Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.
Akijibu swali kutoka kwa waandishi waliotaka kujua kwa nini mawaziri hao walituhumiwa na wameendelea kuwepo katika baraza la mawaziri baada ya mabadiliko ya jana, Balozi Sefue alisema baadhi ya changamoto walizotuhumiwa zilikuwa nje ya uwezo wao.
Kilichowanusuru “Kila wizara ina changamoto zake tofauti na wizara nyingine, wakati mwingine tatizo ni fedha, sasa huwezi kumlaumu Waziri na hata Waziri wa Fedha kama hakuna mapato, huwezi kumlaumu.
“Pia Rais anaangalia Waziri ana mpango gani katika kukabiliana na changamoto ya wizara yake…huwezi kumbadili Waziri anayefahamu tatizo na mwenye mpango wa kulikabili na kumweka mpya ambaye hajui kabisa hilo tatizo,” alifafanua Balozi Sefue.
Tayari Bunge lilipitisha azimio la kumtaka Ghasia pamoja na naibu wake wawili, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa, kupima na kutafakari kama wanatosha kusimamia wizara hiyo.
Kiini cha Bunge kupitisha azimio hilo ni taarifa ya Bunge ya Hesabu za Serikali, kubainisha kuwapo wizi, ubadhirifu na mtandao wa ufisadi ndani ya Tamisemi. Hata hivyo, Waziri Ghasia alinukuliwa akisema hakuna anayepaswa kunyooshewa kidole kwa matatizo yaliyopo Tamisemi.
Akifungua warsha ya kujadili changamoto za uongozi wa Serikali za Mitaa Dodoma hivi karibuni, Ghasia alisema kwa sasa kazi kubwa iliyoko ni kurekebisha kasoro baada ya kufanyika utafiti juu ya matatizo ya Tamisemi.
Alisema wizara yake inashughulikia matatizo hayo baada ya kupokea ripoti ya utafiti, uliofanywa na Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute).
Udhaifu wa waliotolewa Balozi Sefue alipotakiwa kufafanua kama uamuzi wa Rais Kikwete kuwapumzisha kazi mawaziri watano, ulitokana na udhaifu wao na kutakiwa kutaja udhaifu huo, Katibu Mkuu Kiongozi huyo alisema mawaziri hao hawakuwa na udhaifu wowote.
Mawaziri hao ni pamoja na Dk Terezya Huvisa, ambaye alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira). Naibu mawaziri waliopumzishwa kazi pamoja na Dk Huvisa ni Gregory Teu, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na Philipo Mulugo, aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wengine ni Benedict Ole-Nangoro, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Goodluck Ole-Medeye, aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Akielezea sababu za kuwapumzisha, Balozi Sefue alifafanua kwamba kilichofanyika ni kuimarisha Baraza, kutokana na upungufu uliosababishwa na kuachwa kwa nafasi tano za wazi.
“Hata katika timu ya mpira, wale wanaotolewa nje na kuwekwa benchi kabla ya mpira kuisha, haina maana kuwa wana udhaifu, bali ni mbinu tu ya kuimarisha kikosi,” alifafanua Balozi Sefue.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment