BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUYU NDIYE ADUI NAMBA MOJA WA MHE ZITTO ZUBERI KABWE NDANI YA CHADEMA ?, ATAKA AFUTWE UANACHAMA KABISA.

 
MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) ametaka wana Chadema kuunga mkono mpango wa kumfuta uanachama aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wao, Kabwe Zitto.
http://kilimohai.files.wordpress.com/2012/06/zittokabwe1.jpg
Mhe Zitto Kabwe.


“Kuna mlolongo wa mambo yaliyofanya Chadema ikachukua hatua kali dhidi ya Zitto, mambo hayo yamesemwa sana na viongozi wetu; Januari 3, vikao vya chama vitaanza mchakato wa kuhitimisha suala hilo,” alisema. 



“Amekwishaandikiwa barua ya kujieleza kwa nini asifukuzwe uanachama, sasa nawaulizeni wana Chadema Iringa afukuzwe au asifukuzwe ili nikifika kwenye kikao nitoe msimamo wa Iringa?” Aliuliza na sehemu ya wananchi waliohudhuria mkutano wake wakijibu “afukuzweeee….” 


Katika mkutano wake Desemba 31, kwenye Uwanja wa Mwembetogwa mjini hapa, Mchungaji Msigwa alisema Zitto amekikosea mengi chama hicho, hali iliyowanyima uvumilivu na kuamua kumwondoa katika nafasi zake zote za uongozi. 



Alisema pamoja na kwamba alijiunga katika chama hicho akiwa na miaka 16, umaarufu wake kisiasa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na waasisi wa chama hicho, aki wamo Mwenyekiti Freeman Mbowe aliyekuwa akimsaidia kifedha wakati akisoma Chuo Kikuu (cha Dar es Salaam). 



Msigwa aliwasifu baadhi ya watendaji wa Serikali, akisema wanastahili pongezi kwa kazi nzuri wanayofanya kuwaletea wananchi maendeleo. 



“Lazima tuwe waungwana, inapotokea kuna kazi imefanywa na watendaji, ni lazima tuwapongeze bila kujali wanaitumikia serikali ya chama gani,” alisema. 



Alitaja watendaji hao kuwa ni Mkuu wa Mkoa, Dk Christine Ishengoma, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dk Leticia Warioba na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe. 



Aliwapongeza viongozi hao kwa kukataa stendi mpya ya mabasi ijengwe Igumbilo, pembeni mwa Mto Ruaha Mdogo.



“Najua kuna watu walinunua viwanja kuzunguka stendi hiyo kwa gharama kubwa; na wameniandikia barua wakinitisha, kwamba hawataiunga mkono Chadema endapo nitaunga mkono stendi hiyo isijengwe pembeni mwa Mto huo,” alisema.



Alisema watu wanaotaka alifumbie macho suala la ujenzi wa stendi hiyo karibu na chanzo hicho cha maji ni bora waondoke Chadema kuliko kuwaunga mkono. 



“Mbali na shughuli za kilimo, maji ya Mto huo ndio chanzo kikuu cha maji yanayotumika majumbani na wakazi wa Iringa na vitongoji vyake; ikijengwa stendi katika eneo hilo kutakuwa na uharibifu wa chanzo hicho unaoweza kuleta madhara kwenye maji ya Mto; sikubali, bora mtoke Chadema na kura zenu msinipe,” alisema. HABARILEO.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

2 comments:

Anonymous said...


Adui ana sura nyingi

Mola wetu maridhia, wawajua maadawa,
Kinga twakutegemea, salama ndani tukawa,
Ya kwake aanayezua, twakuomba kumng’oa,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Haki budi kutumia, ukweli kujipatia,
Chama kiweze jifua, na kuondoa madoa,
Kisafi kikabakia, huko tunakoelekea,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Wanachama mwatakiwa, jambo hili kutambua,
Hubadilika adawa, muhali kumtambua,
Nje anakoanzia, ndani huweza ingia,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Chama anakitambua, taratibu na sheria,
Umoja ndiyo silaha, ubinafsi hadaa,
Peke ukijichepua, uchama hukupotea,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Chama kinatangulia, na wengine twafatia,
Vikao tunavijua, na hatua kwa hatua,
Uchama kufanikiwa, budi chamani kukaa,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Mashabiki twawajua, nje wanaojikalia,
Waweza kukusifia, kichwa wakakupatua,
Kinapozidi kukua, huweza kukuumbua,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Unyenyekevu ni dawa, lazima kuitumia,
Hii ukishajinywea, nafasi huitambua,
Hutokubali hadaa, vichwani kutupandia,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Chama chataka ridhaa, ya wengi iliyokuwa,
Hoja zikishatolewa, na kura kuzingatiwa,
Nje ukenda yazua, kitu gani yakufaa?
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Wazaini wamejaa, wajua watu tumia,
Mbegu wakajipandia, kusambaratisha nia,
Watu wakijidhania, stahili wafikia,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Kumbe wanachotakiwa, ni chama kukisumbua,
Au kiende umia, na pengine kulemaa,
Au hata kukiua, yao yakafanikiwa,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!

Tunakuomba Jalia, chama kukiangalia,
Mkombozi mtegemewa, Tanganyika angojewa,
Uongozi kuutwaa, hali zetu bora kuwa,
Huwa ana sura nyingi, kawaida ya adui!
S.M. Januari Mosi, 2014,
Dar es Salaam.

Unknown said...

hapana