BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BAADA YA KUANZA KUTIMUA MBIO ZA KAMPENI YA URAIS 2015, SASA ERDWARD LOWASSA BAADHI YA WANACCM WATAKA AWEKWE KATIKA KIKAANGO NDANI YA CCM NA KUADHIBIWA.

Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, John Malecela.
EDWARD LOWASSA.

DODOMA. 

VITA ya urais kupitia CCM inazidi kushika kasi baada ya Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, John Malecela kuutaka uongozi kumchukulia hatua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kuanza mapema kampeni.


Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul Makonda kumtuhumu Lowassa kuwa anakiyumbisha chama hicho kutokana na kampeni za kutaka kuwania urais wa 2015.


Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake mjini Dodoma jana, Malecela alisema Sekretarieti ya CCM inapaswa kuwachukulia hatua kali makada wanaojipitisha maeneo mbalimbali nchini kwa nia ya kusaka urais, kabla ya chama hicho kupanga muda.


Aliwafananisha walioanza mbio za urais kupitia CCM na watu wanaowahi kukimbia kabla ya kipenga kupigwa na kusema hawawezi kupimwa sawa na wale wanaosubiri kuanza rasmi kwa kampeni. Alimpongeza Makonda kwa ujasiri wa kukemea hatua hiyo ya Lowassa bila woga.


Alipoulizwa juu ya suala hilo, Lowassa alijibu kupitia msaidizi wake kuwa hana la kusema. “Nimezungumza na Mheshimiwa Lowassa juu ya suala hilo lakini amenituma niwaambie kuwa hana ‘comment’ (hana la kusema),” alisema msaidizi wake huyo.


Fulana hadharani
Alipoulizwa swali la kwa nini ameamua kumtaja Lowassa pekee huku kukiwa na makada wengi wanaojipitisha kupiga kampeni za urais, kabla ya kujibu, Malecela ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu, aliingia ndani ya nyumba yake na kutoka akiwa ameshikilia mfuko uliokuwa fulana mbili.


Alitoa fulana hizo, moja ikiwa na rangi nyeusi na kahawia na nyingine yenye rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimeandikwa ‘Friends of Edward Lowassa’ (Marafiki wa Edward Lowassa).


“Hivi kuna mwingine aliyefanya hivi? Na hizi zimegawiwa nchi nzima. Ehhh! Hivi kuna mwingine kafanya hivi? Sijui, niongezee nini tena zaidi ya hapo,” alisema Malecela huku akionyesha fulana hizo.


Malecela ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ushauri la Taifa la CCM, alisisitiza kuchukuliwa kwa hatua haraka kwa vitendo hivyo akisema harakati za Lowassa kuwania urais kupitia chama hicho zimesababisha mgawanyiko.


“Jinsi tunavyochelewa kuchukua hatua ndivyo tunavyoweza kuleta mpasuko ndani ya chama. Hapa najiuliza, ile misingi imara ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi iko wapi? Mpaka tumwachie mtoto (Makonda) akemee haya? Je, hapa chama kiko wapi?” alisema.


Alitahadharisha kuwa chama kisipotoa karipio au tamko kuhusu suala hilo, wanaotumia fedha kwa lengo la kutafuta umaarufu na ushawishi ili kupata madaraka wataharibu misingi bora ya uongozi iliyowekwa na waasisi wa CCM.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

1 comments:

Anonymous said...

Nafikiri chama kitumie hekima kwa mambo kama hayo. Hao wapiga kampeni wanakubalika vipi ni swala muhimu sana. Vinginevyo hatua mbaya zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa chama. Ni ushauri tu