
SHUGHULI za kila siku ofisini, ziwe za kuajiriwa ama za kujiajiri huweza kuwa sababu ya matatizo fulani ya kiafya kwa watu. Baadhi ya matatizo haya ni madogo ama huonekana madogo lakini huweza kukua na kuwa makubwa kutokana na kujirudia rudia hadi kumletea mtu matatizo makubwa katika maisha.
Makala haya yaliyopatikana kwa msaada wa mtandao wa kompyuta inajadili kwa kina tatizo hili ambalo linapoanza watu hulidharau lakini baadaye huwa tatizo kubwa na kero kwa mhusika. Misuli kuuma Kwa vile siku hizi watu wengi maofisini,
wakiwemo waandishi wa habari hukaa sana mbele ya kompyuta,
uwezo wa kupata tatizo la kusumbuliwa na misuli ya
mwili, linaloitwa kitaalamu repetitive strain injury (RSI),
yaani kuumiza misuli kunakojiruda rudia, huongezeka
siku hadi siku. Kwa watu wengine, maumivu yatokanayo
na RSI huweza kuwa makubwa kiasi cha kuwazuia kabisa
kufanya kazi.
Hata hivyo, tatizo hili haliibuki siku moja tu na hivyo mtu
anapaswa kujua kwamba siku zote kuzuia tatizo mapema ni
bora kuliko kutibu na hivyo anaweza kusaka mbinu za
kulizuia kama itakavyoelezwa baadaye. RSI ni nini hasa?
Inachukuliwa kuwa maumivu ya misuli ya mwili, yatokanayo na
kazi na hasa mara nyingi maumivu haya huwa katika maeneo ya mikono, ikiwa ni pamoja na mabega na hata mgongo.
Kama kazi unayofanya ni ya kujirudia rudia na ni ya kila siku,
na inashughulisha vidole, mikono au mabega, unaweza kupata madhara katika misuli ya maeneo hayo ya mwili. Hii inaweza kuleta maumivu ama kero ambayo haiponi hata ukitibu kwa kuwa kila siku
utarudia kuumiza misuli husika.
Kinacholalamikiwa sana siku hizi kusababisha ugonjwa wa RSI ni
kibao cha kompyuta (keyboard) na kipanya (mouse) chake, lakini
wataalamu wanasema haifai kusema kuwa vitu hivyo ndivyo
sababu pekee ya kumpa mtu tatizo la RSI. Kwa kuanzia,
wataalamu wanakubaliana kwamba mwili haukuumbwa
kukaa tu muda wote. Hali ya mtu kukaa vibaya, yaani
namna anavyoweka mwili wake kwenye kiti, ama kiti
anachotumia kama pia si kizuri, huchangia kukua haraka kwa
tatizo hili.
Fahamu pia kwamba mtu anapokaa kwa muda mrefu
bila kupumzika huku akiwa ameweka mwili wake vibaya
kwenye kiti basi tatizo humkabili haraka. Mabadiliko
katika maisha yetu ya nyumbani na shughuli zingine za maisha
ama za kijamii zinachangia kwenye tatizo hili. Wakati kompyuta zikiendelea kuzagaa katika jamii yetu, vijana wadogo na watoto wanaozaliwa sasa wako katika hatari kubwa ya kukumbana na tatizo hili kadri maisha yanavyokuwa ya kisasa zaidi na matumizi ya kompyuta kuzidi kuongezeka.
Pamoja na kusubiri kupata RSI watakpoanza kazi, vijana wa
siku hizi huanza kupata tatizo hili kutokana na michezo
(games) iliyoko kwenye kompyuta, Tv, simu ama vifaa
vingine vyenye michezo hii vinavyouzwa madukani. Je,
tatizo la RSI ni jipya? RSI si kitu kipya, wachezaji tenisi na gofu
wamekuwa wakisumbuliwa kwa muda mrefu na tatizo hili.
Na pia kumekuwa na kazi nyingi ambazo watu hujikuta
wakitumia sana misuli ya eneo moja la mwili, hususan misuli ya
mikono, na kupata tatizo la RSI. Watu ambao wamekuwa
wakifanya kazi kwenye viwanda vya kuunganisha vitu,
wanamuziki, vinyozi, wasusi na hata wafagiaji wamejikuta
wakitumia zaidi misuli ya mikono kwa muda mrefu na kila
siku, kiasi cha kuzichosha huku wakiwa hawana namna ya
kuacha kazi hiyo inayowaingizia kipato na kujikuta wamekumbwa na RSI.
Lakini matumizi ya kompyuta ndio hasa yamehamasisha wanasayansi kuchunguza tatizo hili na kuanza kulizungumza
kama tatizo la kiafya. Utatambuaje kwamba tayari una RSI? Inaweza kuchukua miezi au hata mwaka mtu kuanza kusikia kero na maumivu ya RSI. Hii ni kwa sababu huchukua muda kwa
athari zinazojirudia rudia kufikia kiwango cha kuanza kuwa
tatizo.
Maumivu madogo ya leo anayoweza kuyapata mtu, lakini
yeye akawa hajali, anayasikia tena kesho na kuendelea tu na
kazi akiyaona kama si kitu na kudharau kwa vile kwa watu
wengi ugonjwa kwao ni malaria, shinikizo la damu,
kuhara, kifua kikuu, mafua makali, kaswende ama
magonjwa mengine kama hayo.
Lakini kadri siku zinavyokwenda ndipo athari zinavyozidi kuwa
kubwa na dalili huja pale mtu anapokuwa akiendelea na kazi
zake za kujirudia rudia, yaani anapokuwa anaandika kwa
keyboard kwa mfano. Lakini tatizo linapozidi kuwa kubwa,
mtu anaweza kusikia maumivu muda mwingi wa ofisini au hata
anapofanya jambo dogo tu. Moja ya eneo la mikono ama
mabega huathirika kutegemeana na ni lipi analolibebesha zaidi mzigo wa kazi za kujirudia rudia kila siku.
Kuna ripoti ambazo tatizo la RSI limepelekea watu kushindwa
kuona vyema ama kutetemeka mikono kiasi cha kushindwa
kushikilia kitu vyema na hivyo kuanguka, na kama ni glasi
huvinjika.
Jihadhari na RSI Mtu huwa katika athari ya kupata tatizo la RSI kama kazi yake inahusisha hali ya kufanya kazi hiyo hiyo kwa kujirudia. Na uwezekano wa kuugua huwa mkubwa zaidi kama anatumia muda mwingi akiwa amekaa kwenye kiti kibaya, au katika kituo kilichopangwa vibaya bila kupata muda wa kupumzika. Kuzuia siku zote ni bora kuliko kuponya na ndio maana mtu anashauriwa kuzungumza na mwajiri wake ili kufanya tathmini kuona kama viti vya kutendea kazi ama kituo cha kazi kimepangwa vyema na kwamba hakitaathiri mwili kutokuwa sawa sawa wakati wa ukaaji unaochukua muda mrefu. Inaweza kushangaza, lakini si kitu cha ajabu sasa watu wameanza kuweka sponji kufanya mikono iwe imelala juu yake wakati wa 'kutaipu' kompyuta.
Vilevile inashauriwa mtu asikae zaidi ya dakika 20 bila kupata muda hata wa dakika tatu kupumzika ili kunyoosha misuli na kuifanya ipumzike. Mazoezi mepesi na michezo kama yoga inaweza kuwa kitu kizuri katika kusaidia mtu kupunguza athari za RSI.
Mazoezi yawe yale yanayonyoosha misuli. Dawa za kuchua, maji ya moto ama barafu, dawa za kuondoa maumivu kama vile paracetamol; ibuprofen, gels, na dawa zingine zilizo katika mfumo wa krimu kwa ajili ya kupaka yanaweza kumpunguzia mhusika kero.
Wengine pia wamekuwa wakitumia bandeji kufunga mikono yao na kujisikia vyema. Hali inapokuwa mbaya zaidi dawa zenye nguvu kubwa zinaweza kuhitajika kutoka kwa daktari ambaye anaweza kushauri mgonjwa afanyiwe tiba mbadala kama acupuncture au nyingine ambazo zinaweza kusaidia kupunguza ama kuondoa maumivu kabisa. Kichwa kuuma kazini au kipandauso Kichwa kuuma ni tatizo kubwa la kiafya na hivyo si kitu kigeni na ni tatizo ambalo huwapata watu wengi wanapokuwa kazini.
Tofauti na vichwa vingine vya kawaida vinavyouma. Kunaweza kukawa na sababu maalumu inayofanya kichwa kuuma inayohusiana na mazingira ya kazi. Maimivu ya kichwa yatokanayo na mazingira ya kazi kama tutakavyoangalia kwa kina baadaye, yanaweza kumfanya mtu kushindwa kufanya kazi sawasawa. Inaelezwa kwamba zaidi ya masaa milioni 18 ya kufanya kazi mchana hupotea kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kipandauso (migraines).
Hii ni aina moja ya maumivu ya kichwa ambayo inaweza kusababisha dalili mbaya zinazoweza kumsumbua mtu kwa siku tatu na mara nyingi kichwa huwa kinauma kiasi cha kumfanya ashindwe kuwa makini (kutuliza akili) kwenye kazi na hivyo kuwa vigumu kuendelea na kazi. Katika hali mbaya zaidi, tatizo la kuumwa kichwa kazini linaweza kusababisha mtu kuchukuliwa kwamba ni goigoi na hivyo kutopandishwa ngazi ya kikazi.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba waajiri wanaweza kuchukulia kwamba mhusika ama wahusika hawafanyakazi inavyostahili huku wale wenye matatizo ya kuumwa kichwa nao wakifikiria kwamba wanaonekana wategeaji ama kuwafanya wenzao wawafanyie kazi zao kutokana na kuomba ruhusa mara kwa mara. Wengine hulazimisha kukaa kazini huku wakiwa hawajisiki vyema lakini hawawezi kufanya kazi kwa ufanisi kwa vile hawawezi ama kuhofia kuongeza tatizo la kuumwa kichwa.
Nini huchangia tatizo ka kuumwa kichwa kazini? Aina zote za kuumwa kichwa, hususan zinazotokana na mazingira ya kazi pamoja na kipandauso, ni kitu cha kawaida katika maeneo ya kazi kama ilivyodokezwa hapo juu. Wataalamu wanafikiri kuna sababu kadhaa zinazosababisha hali hii. Matatizo haya ya kichwa kuuma kazini yanagawika katika makundi yafuatayo:
Kundi la kwanza ni mambo yahusuyo kazi yenyewe kama vile: fadhaa au msukumo mkali wa kazi (tension), woga, wasiwasi, dukuduku na kadhalika; ukubwa au ugumu wa kazi, muda mchache wa kumaliza kazi (deadlines), na mahitaji ya kazi au hofu kuhusu hali ya familia nyumbani.
Kundi la pili ni mahusiano yasiyoridhisha kazini kama vile mfarakano baina ya mfanyakazi na wafanyakazi wenziye, majungu, ama kutoelewana baina ya mfanyakazi na mwajiri ama kutoelewana na mteja au wateja. Kundi lingine ni mazingira ya kazi kuwa mabaya kama vile joto, makelele, moshi au mwanga hafifu, kiti kibaya ama kukaa vibaya kwenye deski (hali ambayo inaweka mtutuko kwenye uti wa mgongo na shingo. Kingine ambacho kimegunduliwa kwamba husababisha kichwa kuuma wakati wa kazi ni kukaa muda mrefu kwenye kompyuta (mara nyingi pia huambatana na tatizo la macho).
Mambo mengine yanayoweza kusababisha kichwa kuuma ni kukaa sana ukifanya kazi moja kwa masaa mengi au kutopata muda wa kupumzika. Pia kutopata kifungua kinywa cha maana au kukosa mlo wa mchana ni mambo yanayosababisha kichwa kuuma pia. Kadhalika kutopata usingizi mzuri usiku (na hii mara nyingi huwapata wafanyakazi walioko shifti za usiku), unywaji pombe wakati wa chakula cha mchana na kuamka na pombe za jana, navyo vimetajwa kama sababu ya kichwa kuuma. Matatibu Namna ya kupunguza ama kuepuka mambo yaletayo kichwa kuuma kazini ni kuepuka mambo tuliyoyataja hapo juu. Mtu anayeumwa umwa kichwa kazini atafute chanzo na akishakifahamu ni rahisi kuchukua hatua stahili za kuondokana na chanzo hicho.
Pia inashauriwa kuwaona madaktari, hususan wa magonjwa ya vichwa na saikolojia ili kutoa ushauri wa kitalaamu. Kingine ambacho kinawasaidia sana wagonjwa wa vichwa makazini ni kusaka muda mwingi wa kupumzika na kutojihusisha na mambo yanayoleta hasira ama kufikirishwa kichwa.
Kufanya mazoezi mepesi pia husaidia kupunguza tatizo hili. Moja ya mazoezi hayo ni kama hili: Lala chali, nyoosha miguu na mikono yako sambamba na mwili wako, kisha pumzika kidogo.
Baada ya hapo nyanyua miguu yako kuelekea kichwani, isindikize na mikono yako kwa kuishika sehemu ya mapaja kwa nyuma na upeleke mpaka vidole viguse chini (vipite kichwa na kugusa chini).
Rudisha miguu yako ilipokuwa, kisha pumzika tena halafu urudie mpaka usikie misuli ya shingo inafanya kazi (yaani kupata maumivu ya kimazoezi) ndio uache.
.
Usifanye zoezi mara tu baada ya kula chakula. Tatizo la kuumwa mgongo Swali la msingi la kujiuliza ni: Kwa nini huwa tunapata maumivu ya mgongo tunapokuwa kazini? Maumivu ya mgongo ni tatizo linalowakumba watu wengi duniani. Baadhi ya watu wanasema hili ni tatizo linalotokana na maendeleo ya sasa.
Inaelezwa kuwa mazingira mengi ya kazi yanasababisha mgongo usikae wima na kusababisha misuli ishindwe ya mgongo kufanya kazi sawasawa.
Matatizo ya mgongo mara nyingi huanzia kazini. Hebu chukulia mfanyakazi wa ofisini ambaye hukaa karibu masaa 40 kwa wiki akiwa ameketi kwenye deski lake, muuguzi (nesi) ambaye mara kwa mara ananyanyua ama kusukuma baiskeli za wagonjwa, dereva teksi ambaye hujikunja kwenye kiti chake cha gari kwa zaidi ya maili 25,000 kwa mwaka,
mkulima ambaye kila mara ananyanyua magunia ya mazao au msusi ambaye anashinda masaa kadhaa akiwa anasuka nywele saluni huku pengine akiwa kwenye kiti kibaya.
Migongo yetu mara kwa mara inakuwa katika mgandamizo
mkali muda mrefu na hivyo husababisha musuli ma mifupa kushindwa kuleta uwiano wa sawasawa na hivyo kuleta athari kwenye mgongo. http://www.manyandahealthy.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment