DAR ES SALAAM.
Ingawa kuna usemi kuwa binadamu wote ni sawa, na kwamba wana haki ya kuheshimiwa, kupendwa na hata kulindwa, imebainika kuwa watu wenye ulemavu wa akili wanakosa haki hizo.
Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Katibu wa Chama cha Wenye Ulemavu Tanzania (TAMH), Abdallah Mng’obwa anasema kuwa baadhi ya watu wanatumia udhaifu wa wanawake wenye ulemavu wa akili kuwanyanyasa kimapenzi kwa kuwabaka, kuwalawiti na wengine kuzuiwa kuolewa.
“Jamii imeathiriwa sana inaamini kuwa watu hawa unaweza kuwafanya kitu chochote unachotaka, tuna kesi nyingi zinazohusiana na unyanyaswaji wa kimapenzi. Kundi hili linaathirika zaidi kwa sababu mtu akiona hana hela au uwezo wa kwenda kuwachukua watu wazima basi anamchukua mtu mwenye ulemavu wa akili wakiamini kuwa hawezi kutoa taarifa kwa mtu yeyote,” anasema Mng’obwa.
Akitoa mfano wa matukio ya unyanyasaji, Mng’obwa anasema kuwa mwaka 2008 mwanamume mmoja ambaye hakumtaja jina lake, aliyekuwa akiishi Temeke, Dar es Salaam, alikamatwa baada ya kumbaka na kumlawiti msichana mwenye ulemavu wa akili aliyekuwa akiishi naye nyumba moja.
Anasema kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida mtuhumiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani lakini aliachiwa huru kwa madai kuwa hakuhusika na tukio hilo.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Taifa wa TAMH, Shani Zuberi ambaye alisimamia kesi hiyo, anasema kuwa Hadija Nuhu ambaye hivi sasa ni mjamzito, alibakwa na kulawitiwa na mwanamume huyo ambaye ndugu wa binti wanasema alikuwa akionyesha kuwa karibu na binti huyo kumbe alikuwa akifanya naye mapenzi.
Anasema alikutana na binti huyo, ambaye kutokana na matatizo aliyonayo anaweza kuzungumza maneno machache tu, baada ya mama mzazi wa msichana huyo kutoa taarifa katika kituo cha TAMH.
Shani anasema mama mzazi wa binti huyo alibaini tukio hilo wakati anamwogesha kwa kuwa hawezi kuoga mwenye kutoka na matatizo ya akili aliyonayo.
Mng’obwa anaongeza kuwa baada ya mama yake kumuuliza Hadija, alimtaja mpangaji wao, ambaye wakati huo alikuwa akifanya kazi jeshini.
Shani anasema wakati wa kufuatilia kesi, mmoja wa waendesha mashtaka ambaye hakumfahamu jina lake alimwambia kuwa, kitendo kilichofanyika hakikuwa kosa kwa sababu binti ni mtu mzima ambaye pia ana mahitaji ya kimapenzi.
“Akaniambia lakini hii nakwambia tu kama mzazi nje ya mahakama, lakini mimi nikamwambia kama angemfanyia kitendo cha kawaida tungesema hivyo, lakini alimlawiti!” anasema Shani na kuongeza kuwa:
“Binti aliharibiwa vibaya sana sehemu zake za siri, kwa kweli sikudhani kama angeweza kupona na kuwa katika hali ya kawaida tena,”.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment