HOJA yangu kuu kwenye mada hii tangu wiki iliyopita ni kuhusu
vyeti kama kigezo pekee cha kuajiri wafanyakazi. Wafanyakazi wengi
wanashindwa kuleta tija kwenye taasisi zetu hasa za Serikali, kutokana
na mtindo wa kuajiri vyeti badala ya ujuzi, maarifa na ubunifu.
Mathalan, Kwa sasa hata dereva anayebeba roho za
watu kwa anatakiwa awe na vyeti vya kidato cha nne na vyeti vya udereva,
hata kama hajui kuendesha gari na hana uzoefu wa kazi hiyo.
Kila siku Taifa linapoteza maelfu ya Watanzania
kwa vifo vinavyotokana na ajali ya magari kutokana na dhambi hii
kuendelea kutawala kwenye sekta ya ajira, kuajiri vyeti badala ya ujuzi,
utalamu na maarifa.
Madereva wataendelea kuua Watanzania kwa sababu
wanaajiriwa kwa vyeti vya kidato cha nne pasipo ujuzi. Na wengine
wanaajiriwa kutokana na “vyeti mabosi (vimemo kutoka kwa viongozi
wakubwa).
Huwa najiuliza unahitaji mtu wa kujenga daraja,
cheti cha nini badala ya kumpeleka kwenye eneo la daraja ajenge?
Unahitaji mtu wa kurekebisha umeme, cheti cha nini badala ya kumkabidhi
eneo lenye hitilafu ili atengeneze? Unahitaji ofisa kilimo, cheti cha
nini? mpeleke shambani aonyeshe ujuzi wake.
Mbona Wamachinga wanafanya biashara nzuri kila
mahali nchini bila kuonyesha vyeti vya kuhitimu masomo ya biashara?
Mbona babu na bibi zetu vijijini wanafuga ng’ombe kwa maelfu bila kuwa
na cheti cha kuhitimu mafunzo ya ufugaji?
Kwanini kwenye ajira tunakusanya vyeti badala ya
kukusanya ujuzi? Kwanini tunakusanya lundo la makaratasi badala ya
kukusanya lundo la ubunifu na maarifa? Kwa nini tunakusanya A na GPA
nzuri ofisini badala ya kukusanya uvumbuzi na ubunifu? Kwa nini tunalipa
mishahara vyeti badala ya kulipa mishahara kazi, ujuzi, maarifa na
jitihada za watu?
Ieleweke siku zote kuwa; nguvu inayoendeleza taasisi au Taifa lolote haiko kwenye idadi ya digrii na vyeti vya watu wake.
Maendeleo yote duniani yameletwa na maarifa,
ujuzi, ubunifu, uvumbuzi, jitihada ya kazi na kujituma. Kila mwenye sifa
hizi hata kama hajawahi kuingia darasani lazima awe na mafanikio.
Ushahidi tunao; wako babu zetu vijijini hawajui A
wala B. Lakini wanajitosheleza kwenye mahitaji ya msingi na kubaki na
ziada. Wachina wanaoingia nchini hawana vyeti lukuki kama tunavyodhani.
Wana ujuzi na maarifa ndiyo maana wanaajirika kila mahali.
Nazipongeza taasisi na kampuni ambayo
zilizositisha kuita vyeti kwenye usaili wa ajira. Wao wanaomba wasifu
(CV) wa mwombaji kisha anaitwa kwenye usaili. Wamefanikiwa. Wanapata
wafanyakazi wazuri kwa sababu hawana ulevi tena wa kukusanya vyeti kama
ilivyo katika sekta ya utumishi wa umma ikiratibiwa na sekretariati ya
ajira.
Kulundika vyeti lukuki vya wafanyakazi na mafaili
makubwa hakuna tija kwa maendeleo. Kujaza wafanyakazi wenye digrii
nyingi na diploma kibao hakuwezi kuleta tija ofisini. Vyeti havifanyi
kazi. Kinachofanya kazi na kuleta tija kubwa ni maarifa, ujuzi na
ubunifu. Kujituma, uvumbuzi na jitihada ya kufanya kazi kwa malengo. MWANANCHI
1 comments:
Yani kuanzia elimu jinsi vyiti vinavyopatikana ni utata na ajira pia utata. tena siku hizi hawaangalii hata vyiti wanaangalia nani wanamjua.
Post a Comment