BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

BAKWATA YAKATAA SERIKALI TATU.


BARAZA Kuu la Waislamu Tanzania(BAKWATA) limesema Waislamu wanataka Katiba itakayojali maslahi kwa wananchi wa pande zote mbili Bara na Visiwani na kuhakikisha Muungano unadumu. Aidha, Baraza hilo limeunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyotoa wakati wa ufunguzi wa Bunge Maalum la Katiba kuwa imewapa Watanzania upeo mpana zaidi katika kutafakari suala la upatikanaji wa Katiba.

Mufti wa Tanzania Shehe Issa Bin Shaaban Simba, alisema hayo jana wakati akitoa tamko la BAKWATA kuunga mkono hotuba ya Rais Kikwete.

Simba alisema hivi karibuni wamejitokeza baadhi ya wasemaji wa upande wa Waislamu wakidai kwamba mfumo wa Muungano wa serikali tatu ndio maoni ya Waislamu wote nchini.

“Baraza la Ulamaa la Bakwata linaona si sahihi Waislamu wote kubebeshwa fikra na mtazamo wa serikali tatu, sisi kama viongozi wa Kiislamu tunasema Katiba tunayotaka ni ile itakayoleta maslahi kwa wananchi wa pande zote mbili na kuhakikisha Muungano wetu unadumu,” alisema.

Alisema Rais Kikwete alilipatia mwanga suala la mfumo wa Serikali ya Muungano ambao utawezesha wale wote waliopewa dhamana ya kuendeleza mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya kupata vigezo na baadaye uamuzi.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alieleza ugumu wa utekelezaji wa serikali tatu na kuonesha kero za Muungano zinaweza kutatuliwa katika mfumo wa serikali mbili ambapo mpaka sasa sehemu kubwa ya kero hizo zimeshatatuliwa.

Hata hivyo wakati Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba anawasilisha rasimu bungeni alisema suluhisho la kero za Muungano ni muundo wa serikali tatu.

Mufti alisema wajumbe na wananchi wanaweza kutumia vigezo alivyotoa Rais Kikwete kuwezesha mchakato huo wa Katiba kuisha salama.

Mufti alisema Baraza la Ulamaa linawaomba waheshimiwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuzidi kuvumiliana, kustahamiliana na kuheshimiana katika mchakato huo wa kujadili rasimu ya Katiba.

“Aidha Baraza hili linamuomba Allah( Mungu) awazidishie wajumbe hekima, busara na utulivu katika kujadili mjadala wa Rasimu hiyo ili hatimaye tuweze kupata Katiba itakayokidhi matakwa ya Watanzania wote katika ustawi wa taifa letu sasa na baadaye,” alisema.

Tamko hilo la Muft linakuja siku chache baada ya kuwepo kwa mijadala mbalimbali kuhusu muundo wa serikali mbili au tatu wakati Bunge Maalum la Katiba likiendelea mkoani Dodoma.

Mijadala hiyo imekuja wakati Jaji Warioba alipotoa ufafanuzi kuhusu muundo wa serikali tatu na faida zake ikiwemo maoni ya wananchi kuhusu serikali hizo.

Pia siku chache baadaye Rais Kikwete alizungumzia mfumo wa serikali mbili na faida zake katika kuulinda Muungano na kuonesha jinsi serikali tatu zisivyotekelezeka ikiwemo ukosefu wa vyanzo vya fedha kuendesha serikali ya tatu.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: