BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SAMWEL SITTA AMWAGA AHADI KIBAO, ATAEPUKA KUWA MWENYEKITI OVYO ENDAPO ATACHAGULIWA LEO KUONGOZA BUNGE MAALUM LA KATIBA MJINI DODOMA.

SAMUEL Sitta ambaye ni miongoni mwa wajumbe watatu wa Bunge Maalumu la Katiba ambao walichukua fomu jana, ameahidi kusimamia utaratibu ambao hauna upendeleo utakaowezesha Watanzania kupata Katiba bora. Waliochukua fomu hizo jana ni Dk Terezya Huvisa, John Lifa Chipaka na Hashimu Rungwe ambao wanatarajia kurejesha fomu hizo leo saa nne asubuhi na uchaguzi wa Mwenyekiti utafanyika leo jioni.

Sitta alisema anaamini kuwa ndani ya Bunge, kuna watu wenye itikadi mbalimbali hasa kuhusu mtazamo wa Muungano unaostahili, lakini licha ya chama chake kuweka msimamo wa kutaka serikali mbili, yeye atakuwa mwamuzi atakayesimamia hoja zote na hoja bora ndiyo itakayopita.

Mwenyekiti ovyo
Sitta, ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki, alisema itakuwa heshima kwake iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo na akaahidi kulinda heshima kwa kuepuka kuwa Mwenyekiti wa ovyo.

“Najua dunia nzima inaangalia mchakato huu, mimi naogopa kuwa Mwenyekiti wa ovyo, ndio maana nasema nitatumia akili zangu na uzoefu wangu na nitamwomba Mungu aniwezeshe niwe msimamizi bora,” alisema Sitta baada ya kuchukua fomu.

Suala kubwa ambalo ameahidi kutoa, ni Katiba nzuri itakayoondoa kero za Muungano, lakini Katiba ambayo itawezesha kufutwa kwa sheria mbovu ambazo zinatoa mianya ya waovu kuachiwa huru na Mahakama.

Sitta alichukua fomu hizo jana mchana katika ofisi za Bunge na kukabidhiwa na Ofisa wa Bunge, Lydia Mwaipyana huku akiwa ameambatana na wapambe wake ambao ni Paul Makonda na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalah.

Sitta, ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge na kauli mbiu yake ya spidi na viwango, aliahidi kuendeleza mfumo huo kwa kuhakikisha wabunge wote ambao wako ndani ya Bunge hilo, wanapata nafasi ya kuchangia wakiwemo wateule 201 wa Rais.

Sitta alisema amechukua fomu hiyo kwa vile anaamini kuwa uzoefu wake akiwa Spika wa Bunge la tisa na kwa kuwa umri wake ambao umeongezeka, ni wazi kuwa busara itakuwa imeongezeka mara dufu.

Vyama, maslahi.
Aliahidi kufanya vizuri zaidi ya alipokuwa Spika na kwamba atatumia nafasi hiyo na kuendesha mijadala kwa haki na usawa, bila kutawaliwa na hisia za vyama vya siasa wala matakwa ya watu binafsi kwa maslahi yao.

“Ninajua wazi wapo wajumbe humu ndani ya Bunge ambao sio wazoefu wa mambo ya kibunge; lakini kutokana na jinsi walivyoona mijadala ilivyokuwa ikifanyika wakati wa kujadili kanuni, wamepata uzoefu. “Nitajaribu kuwapa kipaumbele waliokosa nafasi ya kuzungumza mara kwa mara katika vikao, ili kutoa nafasi kwa mawazo yao na michango yao isikike,” alisema Sitta.

Alisema uendeshaji wa Bunge hilo utakuwa ni rahisi kutokana na kuwepo kwa kamati mbalimbali za Bunge zenye wajumbe 53, zitakazokutana na atazisimamia ili kuhakikisha kunakuwepo mijadala mizuri zaidi.

Sitta alisema anaamini kuwa mijadala mingi itapata ufumbuzi ndani ya Kamati zenyewe na Bunge litapokea mawazo ambayo tayari yameshafanyiwa kazi kutokana na michango ya wajumbe.

Misimamo ya vyama
Alipoulizwa kama ataweza kuendesha Bunge hilo bila kuyumbishwa na shinikizo kutoka katika chama chake na vyama vingine vya siasa, alisema kamwe atasimamia haki na hataegemea upande wa chama chake.

“Kamwe siwezi kufanya hivyo kwani kanuni zinazoendesha Bunge Maalumu haziniruhusu kushiriki katika vikao vya chama changu cha CCM hasa ninapokuwa nimechaguliwa kuongoza chombo hiki kama Mwenyekiti wa Bunge,” alisema.

Alisema pamoja na kuwa ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), atajitahidi kusimamia mijadala yote kwa ufasaha zaidi. “Sasa CCM sijui wataniletea hizo hoja kwa njia gani…ila ikumbukwe kuwa kinachoshindanishwa si masuala ya uchama, bali ni masuala ya msingi ambayo ni kwa maslahi ya Taifa kwa watu wote,” alisisitiza Sitta.

Siri na uwazi
Alipoulizwa kuhusu namna atakavyosimamia mgawanyiko uliojitokeza juu ya kura ya siri na wazi, Sitta alisema atatumia Kamati ya Maridhiano na Kamati ya Uongozi kulipatia ufumbuzi suala hilo.

Alisema anaamini kuwa wiki hii kamati iliyoundwa na Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho, itakutana kujadili suala hilo na kupata ufumbuzi.

Sitta ambaye ni mgombea anayepewa nafasi kubwa ya kuibuka kidedea katika uchaguzi huo wa Mwenyekiti, alisema anaamini busara ya kamati hiyo italiwezesha Bunge kupata muafaka wa jambo hilo.

Alipoulizwa kuhusu msimamo wake kama hautaathiri kuongoza kiti hicho, Sitta alikiri kuwa anaamini katika serikali mbili kwa vile wanaotaka serikali tatu wanataka kupanua wigo tu wa kujipatia madaraka.

Kampeni
Kampeni za Sitta kuwania nafasi hiyo zilianza muda kidogo baada ya Bunge la Katiba kuanza ambapo wapambe wake walikuwa wakishindana na wapambe wa aliyekuwa mshindani mkubwa ndani ya CCM, Mwanasheria Mkuu wa zamani, Andrew Chenge.

Wakati wapambe hao wakipiga kampeni, Sitta alijitokeza hadharani na kuelezea nia yake ambapo baada ya muda, wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya wabunge wa CCM, waliafiki Sitta kuwa mgombea wa nafasi hiyo kutoka katika chama hicho, huku Chenge akiondoa jina kwa hiari yake.

Jana kulisambazwa kipeperushi cha Sitta cha kuomba kura ambapo katika mtazamo binafsi wa Silla, ilisomeka: “Ni mpenda demokrasia, mtetezi wa haki na maslahi ya anaowaongoza, mzalendo asiyetumia vibaya madaraka anayokabidhiwa, mtetezi wa maendeleo ya wanawake, wanyonge, walemavu; asiyependa ubaguzi wa aina yoyote.

Dira iliyoandikwa katika kipeperushi hicho inasomeka: “Bunge la Katiba lenye mjadala wa kushindanisha hoja kwa hoja, kwa maslahi ya Taifa, ili kuwaletea Watanzania ndani ya muda, Katiba maridhawa inayokidhi matarajio ya wengi na inayojenga matumaini yao ya utawala bora na maendeleo endelevu kwa wote.

Uchaguzi
Bunge Maalumu la Katiba leo watapiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Bunge hilo atakayeongoza hadi kumalizika kwa Bunge na kupatikana kwa Katiba itakayopelekwa kwa wananchi kuipigia kura.

Akitangaza utaratibu wa uchaguzi huo, Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho alisema fomu zimeanza kutolewa jana kwenye ofisi ya Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na Katibu wa Baraza la Wawakilishi ambapo mwisho ni leo saa 4:00 asubuhi na saa 10:00 jioni kutafanyika uchaguzi.

Alisema fomu kwa ajili ya kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti zitatolewa baada ya kupatikana kwa Mwenyekiti.

“Nafasi ya Makamu Mwenyekiti itasubiri apatikane Mwenyekiti, ili tuzingatie jinsia kama ilivyo kwenye makubaliano lakini pia kujua Mwenyekiti ametoka upande gani wa Muungano, ili Makamu atoke upande wa pili kama sheria inavyoagiza,” alisema.HABARILEO.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: