WATOTO WA SYRIA WAPO KATIKA HATARI YA MAISHA YAO
Shirika linalowahudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF linasema idadi ya watoto walioathiriwa na mzozKatika ripoti yake ya jana shirika la UNICEF limesema maelfu ya watoto wamenasa katika maeneo yaliyozingirwa nchini Syria, huku mzozo wa nchi hiyo ukikamilisha miaka mitatu leo.
Idadi ya watoto wa Syria iliongezeka maradufu mwaka jana. "Baada ya miaka mitatu ya vita na machafuko Syria ni mojawapo ya maeneo hatari kabisa duniani," imesema ripoti ya shirika la UNICEF.
"Kwa maelfu watoto wamepoteza maisha na viungo, pamoja na kila kitu kinachohusiana na maisha ya utotoni," imeendelea kusema ripoti hiyo.
"Wamepoteza madarasa na walimu, kaka na dada zao, marafiki, wahudumu, nyumba na uthabiti. Badala ya kusoma na kucheza, watoto wengi wamelazimika kwenda kazini, wanasajiliwa kupigana vitani au wanalazimika kukaa bila kazi."
Shirika la UNICEF limesema idadi ya watoto walioathiriwa ni kubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa katika mzozo wa miaka ya hivi karibuni kwenye eneo hilo. Limezinukuu takwimu za Umoja wa Mataifa kwamba watoto wapatao 10,000 wameuwawa katika vita vya Syria, lakini likatambua idadi halisi huenda ni kubwa kuliko hiyo.
Watoto wa Syria wamekuwa wakimbizi nchini mwao
Mkurugenzi wa shirika la UNICEF, Anthony Lake, amesema, "Vita hivi lazima viishe ili watoto waweze kurejea nyumbani kwao na kuyajenga upya maisha yao katika usalama pamoja na familia na marafiki zao. Mwaka huu wa tatu wa uharibifu kwa watoto wa Syria lazima uwe wa mwisho," akaongeza kusema kiongozi huyo.
Shirika la haki za binadamu la Syria lenye makao yake jijini London, Uingereza, limesema watu zaidi ya 140,000 wameuwawa na wengine 500,000 kujeruhiwa tangu uasi ulipozuka dhidi ya rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, mnamo Machi 11 mwaka 2011.
Hatari kwa watoto zinavuka kifo na majeraha. Ripoti hiyo imesema "vijana wadogo wa umri wa miaka 12 wamesajaliwa kusaidia kupigana, baadhi katika uwanja wa vita, wengine kufanya kazi kama wapashaji habari, walinzi au wasafirishaji wa silaha kinyume na sheria."
Watoto wa Syria wanahitaji msaada
Ripoti ya UNICEF imesema watoto milioni mbili wanahitaji aina fulani ya msaada wa kisaikolojia au matibabu. Jumla ya watoto milioni 5.5 wameathirwa na mzozo wa Syria, baadhi yao ndani ya nchi na wengine wakiishi nje ya nchi kama wakimbizi.
Hii ni mara mbili ya idadi ya watoto waliokuwa wameathiriwa na mzozo huo kufikia Machi mwaka uliopita, wakati shirika la UNICEF lilipokadiria mzozo huo ulikuwa umewaathiri watoto milioni 2.3 wa Syria.
Idadi ya watoto waliolazimika kuyahama makazi yao ndani ya Syria imeongezeka kufikia karibu milioni tatu kutoka 920,000 mwaka mmoja uliopita. Wakati huo huo, UNICEF imesema idadi ya watoto wakimbizi imeongezeka kufikia milioni 1.2 kutoka 260,000 tangu mwaka jana. Watoto 425,000 kati yao wana umri wa chini ya miaka mitano.
Watoto wa Syria katika kambi ya wakimbizi wa UNICEF
Ripoti pia imesema idadi ya watoto wanaokwenda shule imepungua kwa kiwango kikubwa mno. Leo karibu watoto milioni tatu nchini Syria na mataifa jirani hawawezi kwenda shule kama wanavyotakiwa. Hiyo ni takriban nusu ya idadi ya watoto waliofikisha umri wa kwenda shule nchini humo.
Shirika la UNICEF limesema kuna watoto 323,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano katika maeneo yaliyozingirwa au katika maeneo ambayo ni vigumu kwa wafanyakazi wa mashirika ya kutoa misaada kuyafikia.
Ripoti ya shirika hilo inasema watoto wa Syria wanalazika kukua haraka kuliko watoto wa kawaida - mmoja kati ya watoto kumi wakimbizi wa Syria sasa anafanya kazi huku mmoja kati ya wasichana watano wa Syria wanaoishi nchini Jordan wakilamishwa ndoa za mapema. http://www.dw.de/
0 comments:
Post a Comment