SEHEMU YA KWANZA.
Na Juma Mtanda, Morogoro.
UTAJIULIZA mara mbili mbili pale utakaposikia ama kuona binadamu wa
karne ya 21 tena katika ardhi ya Tanzania, nchi yenye amani na upendo ambayo
haijakumbwa na machafuko ya namna yoyote hivi karibuni yanayoweza kupelekea
wananchi wake kuishi maisha kama ya wakimbizi au kulala usingizi wenye mashaka
tele, tena chini ya mapango ya majabari ya mawe makubwa kama wanyama wasio na
makazi maalum.
Serikali imekuwa ikithamini maisha ya wananchi wake katika nyanja
mbalimbali ikijitahidi kwa kadrili ya uwezo wake kuhakikisha wananchi hao
wanaishi vizuri kwa angalau kutimiza mahitaji muhimu kama barabara, majisafi na
salama, afya n:k lakini kwa wakazi wa wilaya ya Ulanga kijiji cha Mbangayao na
kitongoji cha Lupanga hali imekuwa ndivyo sivyo.
Hayo ni maisha ya wakazi wa kijiji cha Mbangayao kilichopo kilometa 20
kutoka makao makuu ya wilaya ya Ulanga mkoa wa Morogoro, wananchi hao
yamewakuta ya kuwakuta na kushindwa kuamini kilichowatokea katika maisha yao
baada ya kuhamishwa na serikali katika kijiji hicho kupisha hifadhi ya msitu wa
asili wa taifa wa Mzelezi.
Katika historia ya maisha ya binadamu, inaelezwa kuwa enzi za mababu
zetu ndiyo waliowahi kuishi katika mapango lakini je utakaposikia ama kuona
binadamu wa karne ya 21, karne iliyojaa binadamu wasomi na wenye maarifa na
kuchambua mambo lipi linafaa na lisilofaa ?.
leo hii utashangaa na kutoweza kuamini pale utakapoona kwa macho yako
maisha ya wanakijiji hao wakiishi kwa kulala mapangoni kwa zaidi ya wiki mbili
huku wengine wakiendelea kuishi maisha hayo.
Nafunga safari ya kwenda wilayani Ulanga februari 18 mwaka huu nikitokea
Morogoro mjini na kulala Ulanga, asubuhi yake napanda pikipiki hadi
kijiji cha Mbangayao na kukutana na Victorian Manjoli kama mwenyeji wa
kuniongoza lakini kitu cha kwanza kuona ni majengo ya shule ya kijiji hicho
yakiwa yamebomolewa na kung’aza kushoto na kulia naona nyumba za wakazi nazo
zikiwa zimebomolewa kwa kuvunjwa na kung’olwa mabati na kupatwa na mshangao.
Mwenyeji wangu Manjoli alinieleza hali unayoina hapa huko tunakwenda
Isaka ndiyo utashangaa zaidi kwani watu huko wanalala katika mapango na kuanza
safari ya kupanda milima na miteremko mikali na kutembea kwa muda wa masaa 2:30
hadi matatu kufika kitongojini Isaka.
Majengo ya shule ya msingi Mbangayao baada ya kuezuliwa paa na serikali.
Ni takribani zaidi ya kaya 124 zinaziishi maishi duni na dhiki tele
isiyo na simulizi wakiishi kitongoji cha Isaka wakitokea kijiji cha Mbangayao
na kitongoji cha Lupanga ambao ili kupata huduma za msingi ni lazima watembea
umbali wa masaa matatu kufuata chakula ama kuifikia barabara kuu ya kwenda
wilayani kwa mahitaji muhimu kama huduma za afya na mahitaji mengine.
Ni hali iliyojitokeza wilaya ya ulanga kwa wananchi wake mapema mwaka
huu kwa kaya 177 zikiwa na familia mchanganyiko wa jinsia tofauti, watoto, watu
wazima wa kiume na akinamama kuishi katika mazingira magumu, huku tamaduni za
kuheshimiana zikitoweka ndani ya wiki mbili mfulululizo bila kujali kuna baba,
mtoto, shangazi, mjomba na kurudikana wakati wa kulala katika pango.
Waswahili husema tembea uone na ukistajabu ya Mussa basi utayaona ya
filauni, itakuhitaji kupanda pikipiki ama kupata usafiri wa gari kukifikia
kijiji cha Mbangayao ambacho kwa sasa utakutana na mahame ya nyumba na majengo
ya shule yakiwa yamebomolewa hapo ndipo utaanza kupata picha ya wananchi hao
wamehamia wapi ?, wazazi, watoto, wanafunzi na wanaume ?.
Kijiji cha Mbangayao na kitongoji cha Lupanga kipo ndani ya hifadhi ya
msitu wa asili wa taifa wa Mbangayao-Mzelezi wakivamia hifadhi ya msitu huo
tangu mwaka 1954 kinyumbe na sheria za nchi na wakati huo huo serikali ikiwa imetoa
notisi ya kwanza ya kuwataka kuondoka eneo hilo.
Dalili za mateso, shida na karaha za kila aina hasa za kukosekana kabisa
huduma za kijamii pamoja na kuishi katika mapango ya mawe kwa wananchi hao
yalianza rasmi mara baada ya shule za msingi kufungwa desemba 6 mwaka jana na
siku ya pili yaaani desemba 7 mwaka huo huo, serikali iliagiza askari mgambo
kufanya doria katika kijiji hicho na kuanza kubomoa majengo ya shule ili
kupisha hifadhi ya msitu huo wa asili wa Mbangayao-Mzelezi kuwa huru kwa
shughuli zozote zile za kibinadamu.
Mwajuma Koya.
Mkazi wa kijiji cha Mbangayao anaelezea mateso, shida na karaha za kila
aina walizopata baada ya kuhama Mbangayao na maisha ya kitongoji cha Isaka
yalivyo hivi sasa anaeleza kuwa kukosekana kabisa huduma za kijamii sambamba na
kuishi katika mapango ya mawe maisha yao hayataweza kusahaulika kiurahisi
katika maisha yao yaliyosalia hapa duniani.
Koya anamweleza mwandishi wa makala haya ya uchunguzi aliyefika katika
kitongoji cha Isaka na kutembezwa eneo la pango kuu la mashineni kuona maisha
mapya ya wakazi hao yaliyojaa kila aina ya changamoto za mahitaji ya kila siku
kwa binadamu.
Anataja changamoto hizo kuwa ni zile za kukosa kabisa barabara, huduma
ya majisafi na salama, afya, elimu duni na makazi ambapo hali hiyo imekuwa kero
kubwa kwa wananchi hao ukilinganisha na sehemu waliyohama. Anasema Koya.
“Shida iliyopo hapa Isaka kwa sasa ni ukosefu wa majisafi na salama,
hakuna barabara, hakuna huduma ya afya na tatizo hili la barabara ndiyo
limekuwa kero kubwa ambalo lina tulazimisha wagonjwa kubebwa katika machela ya
miti na kutembea nayo umbali mrefu wa masaa mawili mpaka matatu ili kuifikia
barabara na hatimaye kuwapelekwa wagonjwa hospitali ya wilaya Ulanga kwa ajili
ya matibabu”. Alisema Koya.
Aliongeza kuwa adha na karaha inatokea pale pindi mgonjwa anapojitokeza
ameshikwa na homa kali na hajiwezi kutembea mwenyewe iwe asubuhi, mchana ama
usiku ni lazima abebwe tu katika machela hayo kwa kupita katika milima na
mitelemko mikali”. Alisema.
Koya alisema kuwa wakazi wa kitongoji cha Isaka kwa sasa wanakosa
mahitaji ya chakula kama ndizi, mihogo na mapapai na badala yake wamekuwa
wakilazimika kutembea umbali huo huo hadi kwenye makazi yao ya zamani ili
kuchukua chakula hicho ambapo hali hiyo inatokana na makazi mapya kukosekana
kwa mazao ya kudumu ambayo yamekuwa mwokozi katika maisha ya kila siku.
“Ni lazima utembee umbali ule ule wa masaa mawili ama tatu kufuata
chakula zikiwemo ndizi, mihogo mapapai na magimbi ndani ya wiki mara mbili ama
tatu kwa sababu huku tulikohamia hakuna mazao ya kudumu na kule Mbangayao ndiko
kuna mazao hayo pengine yangekuwa yanahamishika kero hii ya kushinda na njaa
wakati mungine ingeondoka ”. Alisema Koya.
Aliongeza kuwa hali ilikuwa mbaya wakati wanahamia katika mapango hayo
kwani hakukujali kuna mkubwa, mtoto, shemeji wote walirundikana katika mapango
yam awe kwa wiki mbili huku wengine wakiendelea kuishi katika mazingira hayo
lakini hali hiyo ilipungua kufuatie sehemu kubwa ya wakazi hao kujenga vibanda
vya kujisitiri.
Mzee Phidoline Mbangayao.
Anasema kuwa eneo hilo la kijiji cha Mbangayao ni eneo lao la asili na
wameishi tangu enzi na enzi za mababu zao katika eneo hilo ambalo kwa sasa
ni msitu wa asili wa asili Mzelezi kuwa wakati huo haukuwa na miti zaidi
ya kuwepo jangwa tu huku kazi kubwa ya wazazi wao enzi hizo wakitoa huduma ya
kuzima moto ili isiteketee na kuweza kuathiri ukuaji wa miti ambayo kwa sasa
imetengeneza msitu mnene.
Mbangayao alisema kuwa kitendo cha serikali kuwahamisha eneo hilo ambalo
kwao lina kila huduma za kibinadamu za usafiri, vyakula na urahisi wa kupata
huduma za kiafya na wao kuhama na kuhamia kitongoji cha Isaka ambako hakuna
huduma za kijamii kimewasababishia siku za mwanzo wa kuhama kwao kulala kwa
kurundika katika mapango kwa kaya zaidi 120 kulala pamoja katika mapango.
“Hali bado ni ngumu kwani mpaka leo watu wanalala katika mapango
na wengine wenye uwezo wakiwa wamejenga vibanda vya kuishi na vibanda hivyo
vinakuwa kero wakati mvua ikinyesha kwani vinavujisha maji ndani kutokana na
kuezekea nyasi”. Alisema Mbangayao.
Alisema wakazi wa kijiji cha Mbangayo wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya
kuulinda msitu huo kwa kila mbinu mpaka leo unaonekana msitu na serikali kuwapa
jeuri ya kuwaondoa eneo hilo waliloishi maisha yao yote sambamba na mababu zao
wamekuwa wakitoa ulinzi wa mazao yote na kuzia uharibifu kwani hata wao
wamekuwa wakitegemea kwa kupata faida za upatikanaji wa mvua zinachangia wao
kupata mazao ya kilimo. Alihoji Mbangayao.
“Baba wakati wa uhai wake alinielezwa kuwa babu yake
amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 100 mwaka 1966 na wakati huo baba yangu
mzazi amekuwa ameisha kijiji cha Mbangayao, na koo na koo hadi leo wao
wakiendeleza kuishi kijiji hicho. Alisema Joseph Simba Kayawa.
Kijiji cha Mbangayao enzi hizo hakukuwa na miti zaidi ya kushamili nyasi
katika milima iliyotengenisha kijiji hicho huku ikieleza kuwa milima hiyo
ilitumika kukamata kumbukumbi kwa ajili ya chakula lakini kizazi chetu ndiyo
tumezaliwa na kuona msitu. Alisema Kayawa mwenye umri wa miaka 30 hivi sasa.
“Mkuu wa wilaya alifanya mkutano wa hadhara kijijini kwetu 6/11/2013
akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Ulanga na katika mkutano ule
alieleza kuwa ifikapo desemba 6 mwaka huo alitamka kuwa hataki kuona mtu
kijijini hapo na shule tarahe hiyo itabomolewa na serikali, na baada ya maneno
yale kila mwananchi aliangalia mwelekeo wa kusaka mapango ya kuishi Isaka kwani
muda wa miezi mitatu ulikuwa mdogo kwao kujiandaa”. Alisema Kayawa.
Itaendelea kesho kuona namna maisha yanavyoendelea.
0 comments:
Post a Comment