Na Mtanda Blog, Morogoro.
“Ni mita 300 kutoka eneo ambalo gari lililokuwa limembeba Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine hadi zilipo nyumba zetu, ulisikia mshindo mkubwa wa ulioashiria kuna ajali imetokea katika Barabara Kuu ya Dodoma-Morogoro eneo la Kijiji cha Luhindo, Kata ya Dakawa siku ya Jumatano, Aprili 12 mwaka 1984 mchana ya saa 7. Kumbe ni ajali iliyosababisha kifo cha kiongozi wetu.” “Kitu cha kwanza kukiona kwa mbali ni ajali ya gari eneo hilo, huku nyanya, vitunguu, karoti, viazi mviringo, kebichi, ndizi zikiwa zimetapakaa barabarani,” Hamis Mpandachalo (74), mtunza mali za majengo ya Kumbukumbu ya Edward Sokoine anaeleza anavyokumbuka jinsi ajali iliyokatisha maisha ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine ilivyotokea.
Mhifadhi huyo alikuwa akinukuu simulizi kutoka kwa Ramadhan Dilolo na Mali Yatabu walioshuhudia ajali hiyo lakini kwa sasa wote ni marehemu.
Mwandishi wa makala haya alifunga safari kuelekea eneo alilopata ajali hayati Sokoine ili kujua kinachoendelea na alikutana na Hamis Mpandachalo anayeeleza mambo mbalimbali ikiwamo shughuli zake za utunzaji eneo hilo alizokabidhiwa, wadau wakuu ikiwa Serikali na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Kwanza aliteuliwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania hayati Julius Nyerere kuwa Waziri Mkuu, tangu tarehe 13 Februari 1977 hadi Novemba 7, mwaka 1980 na mara ya pili alishika wadhifa huo tangu tarehe 24 Februari 1983 hadi kifo chake kutokana na ajali hiyo.
Ilielezwa kwamba gari aina ya Marcedes Benz alilokuwa akisafiria Sokoine akitokea bungeni mjini Dodoma, liligongana na gari ina ya Toyota Land Cruiser, ambalo liliendeshwa na aliyekuwa mkimbizi wa Afrika Kusini, Dumisan Dube aliyeingilia msafara wa Sokoine.
Dube alikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na alishikiliwa, baadaye alipotolewa akarejeshwa nchini kwao, huku hisia za wananchi wengi kwa wakati huo kuwa ajali hiyo huenda ilipangwa.
Uongozi wa Sokoine aliyezaliwa mwaka 1938 ulionekana kuwa wa mfano wa kuigwa kwa jinsi alivyoonyesha uadilifu, akiwa mfuatiliaji utendaji kazi, pamoja na kukemea ulaji rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Kifo cha Waziri Mkuu huyo kilileta majonzi makubwa kwa Watanzania wa kawaida waliokuwa wakimtarajia kuwatetea wanyonge na kuinua hali ya maisha yao.
Mwili wa Edward Moringe Sokoine ulizikwa nyumbani kwao Monduli Juu, mkoani Arusha.
Chuo cha Kilimo na Mifugo Morogoro wakati ule kikaitwa Chuo cha Kilimo cha Sokoine; ambacho sasa ni Chuo Kikuu cha Sokoine (Sua).
0 comments:
Post a Comment