SERIKALI KUTUMIA BAJETI YA SHILINGI TRILIONI 19.7 KATIKA MWAKA WA FEDHA 2014/2015.
Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya .
SERIKALI imepanga kutumia Sh trilioni 19. 7 katika mwaka wa fedha 2014/2015, kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo, tofauti na Sh trilioni 18.2 ya mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 30.
Katika fedha hizo, matumizi ya kawaida yamepangwa kuwa Sh trilioni 14.2, ambapo kati ya hizo Sh trilioni 5.1 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali, taasisi na wakala wake.
Aidha Sh trilioni 4.4 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko Mkuu wa Serikali na Sh trilioni 4.4 kwa ajili ya matumizi mengine. Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akiwasilisha Mpango wa Bajeti ya mwaka ujao wa fedha kwa wabunge.
Matumizi ya Maendeleo
Alisema makadirio ya matumizi ya maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha ni Sh trilioni 7.7 sawa na asilimia 39.3 ya matumizi yote ya Serikali na kati ya kiasi hicho, miradi ya maendeleo imetengewa Sh trilioni 5.4 sawa na asilimia 27.7 ya matumizi yote ya Serikali, huku matumizi mengine ya maendeleo yakitengewa Sh trilioni 2.2.
“Kwa upande wa matumzi mengine ya maendeleo, a s i limia 63 inagharimiwa na fedha za ndani hivyo kuongeza kujitegemea,” alisema.
Alisema katika matumizi mengine ya maendeleo Sh bilioni 751.7 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, Sh trilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya malipo ya mikopo iliyokopwa na makusanyo ya Halmashauri ya Sh bilioni 138.7, yatatumika kwa ajili ya maendeleo.
Vipaumbele
Kwa mujibu wa Waziri Mkuya, katika matumizi ya maendeleo, Bajeti itazingatia kutekeleza Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (Mkukuta II), Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano 2011/2012 mpaka 2015/2016 na Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Katika BRN, Waziri Mkuya alisema Bajeti itajielekeza katika maeneo sita ya kitaifa ambayo ni kilimo, elimu, maji, utafutaji rasilimali fedha, nishati na uchukuzi na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara.
Kilimo
Katika Kilimo, Serikali inapanga kuhamasisha kilimo cha kibiashara cha ngano na miwa ya kuzalisha sukari katika Mto Wami, Ruvu, Kagera, Kilombero na Malagarasi.
Pia inalenga kuboresha skimu za masoko na umwagiliaji wa mpunga kwa ajili ya wakulima wadogo, kujenga skimu za pamoja kwa ajili ya kuwaunganisha wakulima wa mahindi na masoko na kuongeza upatikanaji na utumiaji wa pembejeo, zana za kilimo na huduma za ugani.
Elimu Serikali katika elimu, imepanga kuweka mkazo katika maeneo yaliyokubaliwa kutekelezwa chini ya BRN, ambayo hata hivyo hayakufafanuliwa.
Maji Waziri Mkuya alisema katika sekta ya maji, Serikali inapanga kuwezesha kudumu kwa miradi iliyopo ya maji kwa kuhakikisha jamii inashirikishwa ipasavyo katika kuisimamia.
Pia Serikali imepanga kuongeza vituo vya upatikanaji maji vijijini kwa kupanua, kukarabati pamoja na kujenga vituo vipya vya usambazaji maji.
Malengo mengine ya kipaumbele ni kuendelea na utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya maji ikiwa ni pamoja na Kimbiji, Mpera na bwawa la Kidunda na kuboresha miradi ya usambazaji maji safi na taka katika maeneo ya mijini.
Madini
Katika sekta ya madini, msisitizo uliwekwa katika kuhakikisha Serikali inapata mapato ya kutosha kutoka sekta ya madini kwa kuzijengea uwezo ofisi za kanda na kuhamasisha uongezwaji wa thamani wa madini ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Miundombinu
Sekta ya miundombinu katika malengo hayo ya kipaumbele, imegawanywa katika makundi sita ambayo ni reli, barabara, madaraja na maghati, bandari na usafiri wa majini, usafiri wa anga, utabiri wa hali ya hewa na nishati.
Katika nishati, Serikali imelenga kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam na kuendeleza utekelezaji wa miradi mingine 28 ya umeme chini ya mfumo wa BRN.
Pia Serikali imelenga kuendelea kuimarisha miundombinu ya uzalishaji nishati ya umeme iliyopo pamoja na kupeleka umeme vijijini na kuhamasisha uwekezaji katika nishati jadidifu.
Katika eneo hilo la miundombinu, Serikali imejipanga kuboresha miundombinu ya utabiri wa hali ya hewa pamoja na kujenga uwezo wa watumishi na taasisi ya utabiri wa hali ya hewa.
Katika eneo la usafiri wa anga, Serikali imepanga kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, kujenga viwanja vya ndege katika maeneo ya kimkakati pamoja na kukarabati vilivyopo na kuboresha mazingira ya kibiashara ilikuvutia wawekezaji.
Reli, barabara, bandari
Kuhusu reli, Serikali imejipanga kuweka mkazo katika kuendelea kuimarisha Reli ya Kati, kukarabati na kutengeneza reli zilizopo, ununuzi wa vichwa vya treni, mabehewa na vifaa vingine.
Pia Serikali imejipanga kukarabati na kutengeneza mifumo ya mawasiliano ya simu pamoja na mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo na kuendelea na utekelezaji wa miradi mipya ya reli katika maeneo ya kimkakati.
Kwa upande wa barabara, Serikali imejipanga kujenga na kukarabati barabara zinazofungua fursa za kiuchumi pamoja na kupunguza foleni katika maeneo ya mijini, kujenga na kuimarisha mizani, kutekeleza miradi mingine 23 ya barabara iliyoainishwa chini ya mfumo wa BRN na kuendeleza na kuimarisha barabara zinazounganisha mikoa, wilaya na vijiji, kujenga madaraja, maghati na ununuzi wa vivuko.
Katika bandari, Serikali imejielekeza kujenga bandari mpya katika maeneo ya kimkakati pamoja na kuimarisha zilizopo, kuongeza uwezo wa kubeba mizigo katika bahari, maziwa na bandari kavu na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi katika bandari na kuweka mazingira stahiki kwa ajili ya sekta binafsi kuwekeza.
Kipaumbele cha sita katika mfumo wa BRN, kitakachozingatiwa na Bajeti ijayo, ni utafutaji wa rasilimali fedha, ambapo Serikali imejipanga kupanua wigo wa ukusanyaji kodi ikiwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa ushuru wa forodha.
Pia Serikali imejielekeza kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi, pamoja na kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kuwezesha ubia kati ya serikali na sekta binafsi.
Serikali pia imejipanga kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kuwezesha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, kuhimiza malipo kwa njia ya mtandao na kupunguza misamaha ya kodi.
Mapato
Waziri Mkuya alisema sera ya mapato kwa mwaka 2014/2015, inalenga kuimarisha utaratibu wa kukusanya mapato pamoja na kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia moja ya Pato la Taifa.
Serikali pia imepanga kukamilisha utungwaji wa sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kuongeza wigo wa kodi kwa kuimarisha vyanzo vilivyopo na kuainisha vyanzo vipya pamoja na kurasimisha sekta isiyo rasmi, ili iingie kwenye mfumo rasmi wa kodi.
“Serikali imekamilisha utafiti wa mfumo wa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi ambapo utafiti umelenga kuhuisha na kuwianisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato hayo ambapo matokeo yake yatajumuishwa katika maboresho ya mfumo wa kodi kwa mwaka huu,” alisema.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment