MWENYEKITI wa Kamati ya Bajeti, Andrew Chenge, ameibua madudu makubwa
kwenye bajeti ya mwaka 2014/2015 ambapo amesema ina pengo la sh
trilioni 4.9 sawa na asilimia 24.
Chenge alisema bajeti hiyo ina pengo la sh trilioni 2 ambazo
hazikupatikana mwaka 2013/2014 na sh trilioni 1.6 zilizoongezeka mwaka
2014/2015 kutokana na kuongezeka kwa bajeti kutoka sh trilioni 18.2 hadi
trilioni 19.8.
Aliibua madudu hayo jana bungeni alipokuwa akisoma taarifa ya kamati
yake kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2013 na mpango wa
maendeleo wa taifa kwa mwaka 2014/2015 pamoja na tathimini ya
utekelezaji wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2013/2014 na mapato na
matumizi ya serikali kwa mwaka 2014/2015.
Alisema bajeti ya mwaka jana ilikuwa sh trilioni 18.2, lakini mapato
yaliyopatikana hadi kufikia Aprili mwaka huu serikali ilikusanya sh
trilioni 12.8 sawa na asilimia 70 na inakadiriwa hadi kufikia Juni mwaka
huu makusanyo hayo yatafikia asilimia 93 ya lengo.
Alibainisha kuwa kutokana na makusanyo hayo, nakisi itakuwa ni sh
bilioni 728 sawa na asilimia 7, hivyo kamati yake inaona sera ya kodi
imeshindwa.
Alisema kuwa bajeti ya 2014/15 imeongezeka kwa sh trilioni 1.6
(asilimia 8.8), ikilinganishwa na mwaka 2013/14, lakini serikali imekuwa
ikijinasibu itafanikisha ukusanyaji mapato vizuri ilhali kuna tatizo
kwenye ukusanyaji.
Chenge aliongeza kuwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014, serikali
imetumia sh bilioni 115.81 tofauti na zilizoombwa na idara au wizara
husika.
Pia Chenge, ameishutumu serikali kwa kukosa ubunifu wa vyanzo vipya
vya kodi, kutoogopa deni la taifa pamoja na kupuuza ushauri wanaopewa
juu ya kuboresha bajeti.
Alisema kuwa katika bajeti ya mwaka 2013/2014, serikali ilifanya
utekelezaji wa baadhi ya mafungu kinyume na matarajio, kwamba baadhi ya
mafungu ambayo hayakutengewa fedha yalipewa nje ya bajeti za fungu
husika.
Alisema serikali imekosa ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na
haitaki kupokea ushauri uliotolewa na kamati yake juu ya vyanzo hivyo
hali inayowafanya waendelee kuwaumiza walipa kodi walewale kila mwaka.
“Sijui nisemeje, lakini hii ni dalili ya kuchoka kufikiri, yaani kila
siku nyinyi ni kutoza kodi kwenye juisi, soda, bia, pombe kali na
sigara… huu ni udhaifu mkubwa sana, mmezoea kutuletea vyanzo vyenu
vilevile vya kitamaduni mlivyovizoea,” alisema.
Alisema katika bajeti ya mwaka huu, serikali inatarajia kukusanya
mapato ya ndani ya sh trilioni 12.44 ambayo hayatoshi kugharimia
mahitaji ya mishahara (sh trilioni 5.317), deni la taifa sh trilioni
4.354 na matumizi yasiyoepukika ya sh trilioni 3.063.
“Ukiangalia kwa umakini utagundua makusanyo ya ndani ya sh trilioni
12.44 na matumizi yetu tuna upungufu wa kiasi cha sh bilioni 294…. huko
tuendako hakuonyeshi hali nzuri hata kidogo,” alisema.
Aliongeza kuwa kamati yake imebaini lipo tatizo tangu siku ya kwanza
bajeti hiyo inapoanza kutekelezwa ambapo inakuwa na upungufu wa sh
bilioni 968.
Chenge, alibainisha kuwa kamati yake haijaridhishwa na uamuzi wa
kupunguza kodi ya mshahara (PAYE) kwa asilimia moja kutoka 13 hadi 12,
hivyo kuitaka serikali katika bajeti ya mwaka 2015 ipunguze hadi kufikia
tarakimu moja.
Aliongeza kuwa serikali pia imeshindwa kupunguza matumizi yake kama
ilivyoshauriwa na Bunge pamoja na kamati yake na matokeo yake balozi 16
kati ya 32 zimebainika kutumia fedha nyingi zaidi kuliko zile
walizoidhinishiwa.
Alisema miongoni mwa balozi hizo ni ule wa Maputo uliotumia sh
bilioni 117.4 kwa ukarabati, fedha ambazo ni nje ya bajeti iliyotengwa.
Chenge alisema serikali inataharisha uhai wa mifuko ya jamii ambapo
licha ya kudaiwa deni kubwa linalozidi sh trilioni 3 kutoka kwa Mfuko wa
PSPF, bado ulipaji wake umekuwa wa kusuasua kwani inalipa sh bilioni 50
kwa mwaka kiasi ambacho ni kidogo.
Alisema serikali imekuwa na utaratibu wa kuficha madeni ya wazabuni
na makandarasi, na kuzifanya bajeti zinazotengwa katika wizara husika
kwa mwaka husika kutumika kulipa madeni ya nyuma na hivyo kuathiri
shughuli za maendeleo.
Deni la taifa
Chenge alibainisha kuwa deni la taifa hadi kufikia Machi 2014
lilikuwa ni sh trilioni 30 ikilinganishwa na sh trilioni 23.67 Machi
2013, na serikali imetoa sababu za kuonyesha deni hilo stahimivu.
Alisema kamati yake hairidhishwi na usimamizi wa deni hilo na inataka
kuharakishwa kwa uanzishwaji wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Taifa.TANZANIA DAIMA
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / CHENGE AIBUA MADUDU KATIKA BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA WA FEDHA 2014/2015 BUNGENI DODOMA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment