BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

DENI LA TAIFA LA TANZANIA LAONGEZEKA KWA KASI.

WAZIRI Kivuli wa Fedha, Bw. James Mbatia, amsema deni la Taifa limeongezeka kwa kasi ya hatari na kufikia sh. trilioni 30.5 kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi sasa.

Bw. Mbatia aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na kuongeza kuwa, mwaka 2013 deni hilo lilikuwa sh. trilioni 23. 


Alisema kambi hiyo inashangazwa na ongezeko hilo sawa na bajeti ya mwaka wa fedha 2007/8 ambalo ni vigumu kulipika kutokana na ukweli kwamba, haliendani na kasi ya ukuaji wa uchumi. 


“Kambi ya Upinzani imebaini kuwa, Serikali ilishindwa kufuata mapendekezo tuliyoyatoa na kusababisha ongezeko kubwa la bajeti ambalo ni sh. trilioni 12 kuanzia mwaka 2008 hadi sasa. 


“Serikali imekuwa ikijitamba kukopesheka na kuchukua mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa...tunaitaka Serikali ifafanue matumizi ya fedha zilizokopwa kwa miaka saba, zimeleta faida gani kwa nchi,” alisema Bw. Mbatia. 


Kwa upande wake, Mbunge wa Mbozi Magharibi, Bw. David Silinde, alisema tatizo kubwa la Serikali ni kutofanya utafiti kuhusu matatizo ya wananchi ndio maana inapeleka bajeti isiyotekelezeka. 


“Katika taarifa ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwenye ripoti ya 2011, wameeleza kuwa, Watanzania tunaopaswa kulipa kodi milioni 13.5, lakini wanaolipa kodi ni milioni 2.5 hivyo watu milioni 11 hawalipi kodi,” alisema Bw. Silinde. 


Aliongeza kuwa, tatizo lililopo si vyanzo vya mapato wala bajeti ndogo, bali ni uzembe wa serikali kukusanya mapato ambapo uzembe huo hauwezi kuvumilika hata kidogo. 


Bw. Silinde alisema, ili kuongeza vyanzo vya mapato ya Serikali, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) thamani ya majengo yake yanaweza kusaidia kulipa kodi. 


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Bw. Andrew Chenge, alisema deni la Taifa ni mzigo mkubwa kwa Serikali kwani halivumiliki kwani haliendani na kasi ya ukuaji wa uchumi ambapo umaskini haupungui kwa kiwango cha kuridhisha. 


Aliitaka Serikali ihakikishe uchumi wa nchi unakua kwa asilimia nane kwa kipindi cha miaka 10 mfululizo ili kupunguza kiwango cha umaskini kwani ukuaji wa uchumi kwa sasa ni asilimia 6.1 hali ambayo haiendani na hali halisi ya maisha. 


Kamati hiyo ilishauri kuwa, nidhamu ya matumizi ya fedha za umma izingatiwe ili kuleta mabadiliko na kuangalia mfumo wa kodi kwani baadhi ya mapendekezo yaliyowasilishwa kwenye bajeti yana ugumu wake.MAJIRA
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: