Dodoma.
Siri ya mvutano uliodumu kwa takriban wiki mbili baina ya Serikali na Kamati ya Bajeti, utawekwa hadharani leo wakati Bunge litakapoanza kujadili Bajeti Kuu.
Siri ya mvutano uliodumu kwa takriban wiki mbili baina ya Serikali na Kamati ya Bajeti, utawekwa hadharani leo wakati Bunge litakapoanza kujadili Bajeti Kuu.
Mjadala huo utaanza kwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge kusoma maoni ya kamati yake na kufuatiwa
na Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia ambaye atasoma maoni ya Kambi ya
Upinzani kuhusu bajeti hiyo.
Mbatia pia ni mjumbe katika kamati inayoongozwa na
Chenge, hivyo hoja zao huenda zitashabihiana katika baadhi ya maoni na
mapendekezo, kubwa ikiwa ni hoja ya kutozingatiwa kwa baadhi ya ushauri
kuhusu vyanzo vipya vya mapato.
Kadhalika, hoja kuhusu mzigo wa madeni unaoikabili
Serikali, kutokuwapo kwa miradi ya vipaumbele, kutotengwa kwa fedha za
kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuyumba kwa bajeti
inayoishia Juni 30 mwaka huu, zinatarajiwa kutawala mjadala huo.
Kuanza kwa mjadala huo ndani ya Bunge ni
mwendelezo wa kile kilichokuwa kikijadiliwa kwa takriban kwa wiki mbili
baina ya Serikali na Kamati ya Bajeti.
Awali kulitokea mabishano makali kutokana na
kutotengwa katika bajeti fedha za kulipa madeni ya makandarasi wa ujenzi
wa barabara ambayo hivi sasa yanafikia Sh800 bilioni, pamoja na
kutokuwapo kwa makadirio ya fedha za kugharimia mafuta ya kuendeshea
mitambo ya kufua umeme.
“Tumewauliza kwamba hizo fedha zitatoka wapi, kwa
kuwa katika mafungu ya wizara hizo (Ujenzi na Nishati na Madini)
hazikutengwa na hata kwenye bajeti kuu hazipo, sasa zitalipwaje, lakini
hawatujibu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho na
kuongeza:
“Tumekuwa na wasiwasi kwamba huenda fedha
wanachukua kwenye makusanyo ya kodi na kusababisha kushindwa kutekeleza
mahitaji mengine kwenye bajeti. Ndiyo hivyo si mnaona fedha hazikutoka
kabisa mwaka huu wa fedha?”
Taarifa Hazina iliyotolewa mbele ya Kamati ya
Bajeti inaonyesha kuwa kati ya Oktoba mwaka jana na Machi mwaka huu,
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lilipewa Sh578 bilioni kwa ajili ya
ununuzi wa mafuta, ikiwa ni wastani wa Sh96.33 bilioni kwa mwezi.
Akisoma bajeti ya Serikali ya 2014/15, Alhamisi
iliyopita, Waziri wa Fedha, Saada Nkuya Salum alitaja gharama kubwa za
uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme wa dharura na madeni makubwa ya
makandarasi, wazabuni na watumishi kuwa ni baadhi ya changamoto katika
utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Hata hivyo, alisema: “Kuhusu madai ya makandarasi
na wazabuni, Serikali inakamilisha utaratibu wa kuyasimamia na kulipa
madai yaliyohakikiwa kupitia Hazina kwa kushirikiana na wizara na
taasisi zinazohusika.”
Suala lingine ambalo lilionekana kuitisha Kamati
ya Bajeti ni ukuaji wa kasi wa deni la taifa ambalo limefikia Sh30.563
trilioni, ambalo kwa mtizamo wa wajumbe wengi ni sawa na asilimia 57.7
ya pato la taifa.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment