UKICHAGULIWA MCHUMBA NA WAZAZI TUMIA BUSARA ZA KUMKATAA...!
NI tatizo linalowasonga vijana wengi hususani wale ambao wako katika ngazi mbalimbali za vyuo na vyuo vikuu, kupata mchumba. Kuna changamoto nyingi katika kusaka na hatimaye kumpata mchumba muafaka atakayekuwa mke au mume katika maisha.
Changamoto hiyo ilimpata pia rafiki yangu mmoja miaka ya 1980, wakati huo alikuwa anasoma katika moja ya vyuo vya serikali jijini Dar es Salaam lakini kwa sababu za wazi za kitaaluma nisingependa kulitaja jina lake wala chuo husika.
Alinisimulia kwamba siku moja akiwa chuoni kwake alitembelewa na dada yake toka kijijini kwao aliyefika jijini Dar es Salaam kusafisha macho na kisha arejee kijijini.
Katika mazungumzo yao, dada yake alimweleza kuwa baba na mama yao wanaharakati za aina yake juu ya msichana mmoja hapo kijiji ambaye sasa amefikia kiasi cha kutokwenda kanisani Jumapili hadi apitie hapo nyumbani kwao, kuwasalimia wazee hao na wakati mwingine huongozana na mama yao kwenda na kurudi kanisani.
Kaka mtu alijaribu kumdadisi dada yake kwa kumwuliza kwani kufanya hivyo kuna tatizo gani? Bila kupoteza maneno alimweleza kuwa msichana huyo ndiye aliyekuwa anaandaliwa kuwa mchumba wake.
Taarifa hiyo kwa mujibu wa rafiki yangu, ilimshitua sana kwa sababu nyingi ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kutokuwa tayari kujitumbukiza katika uhusiano wa aina hiyo kwa kuwa bado yuko masomoni lakini pia hawajawahi kumwona mchumba mwenyewe na hata akija kumwona hapo baadaye alisema hana uhakika kama ndiye atakayekuwa chaguo lake.
Wakati kaka anajiuliza maswali mengi, dada yake alimhadharisha kwamba asipochukua hatua, atajikuta analetewa mrembo huyo kabla ya mwisho wa mwaka. Hapo alilazimika kufikiri haraka ili kulikabili jambo hilo kwa busara na hekima bila kuwaudhi wazazi wake ambao alikiri kwamba alikuwa anawapenda na kuwaheshimu ipasavyo.
Alimshukuru dada yake kwa kumpatia taarifa hizo muhimu naye kwa upande wake aliahidi kuchukua hatua za kudhibiti hali hiyo kabla hajachelewa.
Rafiki yangu alibahatika wiki moja baadaye kutembelewa tena chuoni hapo na binamu yake ambaye alimuaga pia kwamba anakwenda likizo nyumbani kwa maana ya kijijini kwao.
Ndipo alipotumia nafasi hiyo kumwomba awapelekee wazazi wake barua ambayo alikuwa ameshaiandaa kwenda kwa wazazi wake kuwaeleza msimamo wake juu ya suala la mchumba wanayemwandaa.
Alinieleza kwamba ilimchukua saa mbili kuiandika barua hiyo ya kurasa mbili lakini ikieleza kwa makini na busara juu ya hoja yake kwa wazazi wake.
Alimwomba binamu yake siyo tu aifikishe barua hiyo, bali pia yeye mwenyewe awasomee barua hiyo wakiwapo wote wawili, baba na mama ili kuhakikisha kwamba ujumbe umefika inavyotakiwa.
Kwa kifupi aliwashukuru kwanza wazazi wake kwa kumlea lakini pia aliwaeleza juu ya mafunzo yake aliyokuwa anachukua chuoni ya muda wa miaka miwili lakini pia baada ya muda huo alikuwa anatakiwa kwenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa muda wa mwaka mmoja.
Kwa maneno mengine alikuwa anahitaji miaka mitatu ya kukamilisha zoezi hilo na baada ya hapo kusaka kazi kabla ya kufikia hatua ya nyingine ya kumtafuta mchumba wa chaguo lake.
Aliwaomba pia wamruhusu ''mchumba'' huyo waliyekuwa wanamtafutia aolewe na mtu mwingine yeyote kwani muda wa kuweza kumsubiri lolote linaweza kutokea.
Alihitimisha kisa hicho kwa kunieleza kuwa Mungu alikuwa upande wake kwa sababu wazazi wake walimwelewa na wakakubaliana na mawazo yake. Alikabiliana na changamoto iliyompata vilivyo bila kuharibu au kuwaudhi wazazi wake.
Baada ya masomo na JKT alipata mchumba wa chaguo lake. Kwako kijana wa siku hizi ungechukua hatua gani? Jibu unalo mwenyewe.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment