KUFUATIA VITISHO, CHAMA CHA NCCR-MAGEUZI WATAKA SERIKALI SASA IMLINDE MBUNGE WA KIGOMA KUSINI.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila akichangia mjadala bungeni mjini Dodoma hivi karibuni.
Dar es Salaam.
Chama cha NCCR-Mageuzi kimeitaka Serikali kumpa ulinzi wa kutosha mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kutokana na vitisho anavyopata baada ya kusimama kidete bungeni akitaka suala la uchotaji fedha kwenye akaunti ya Escrow kutoka Benki Kuu (BoT) lichunguzwe.
Kafulila aliingia kwenye mgogoro na Mwanasheria Mkuu Jaji Fredrick Werema mwezi uliopita wakati wa Bunge la Bajeti alipoibua tena suala la wizi wa fedha hizo. Wawili hao walizozana baada ya Kafulila kuomba mwongozo ambapo Jaji Werema kudiriki kumuita mbunge huyo “tumbiri”.
Neno hilo lilimfanya Kafulila amwambie Jaji Werema kuwa naye “ni mwizi” na ndipo baada ya kikao hicho, kigogo huyo wa serikali alimfuata nje akionekana kutaka kumpiga kabla hajazuiwa na wabunge wengine. Siku iliyofuata, Werema alikaririwa akisema “anataka kichwa chake (Kafulila).
Jana, NCCR-Mageuzi iliamua kuomba hadharani ulinzi wa mbunge wao na kumtaka Jaji Werema ajipime kutokana na vitendo vyake kama anastahili kuendelea kushika wadhifa huo.
“Kama chama tunapenda kurejea na kusisitiza kuwa tuna hofu na uhai wa mbunge wetu (Kafulila) hasa kutokana na mazingira yanayozunguka ajenda hii anayoisimamia ambayo inagusa vigogo na mafisadi wakubwa,” alisema katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alipozungumza na waandishi wa habari jana akiwa pamoja na Kafulila.
“Tunahofia usalama wa Kafulila kwa kuwa Spika Anne Makinda kashindwa kuchukulia kwa uzito mwongozo ulioombwa na mbunge huyo kuhusu kutishiwa maisha.
“Tunao uzoefu wa mazingira kama haya kama pale kijana Amina Chifupa alipozungumzia dawa za kulevya. Pia tunao uzoefu na kilichotokea kwa Dk Sengondo Mvungi alipokuwa mhimili imara wa serikali tatu ndani ya tume ya (Jaji Joseph) Warioba, wote tunafahamu kilichowakuta.”
Akaunti hiyo ya Tegeta Escrow ilifunguliwa baada ya kuwepo mgogoro wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa ajili ya kuhifadhi fedha ambazo zingetumika kulipia gharama na malipo mengine wakati na baada ya mgogoro huo kumalizika kwa maridhiano ya pande zote mbili.
Nyambabe, aliyekuwa ameongozana na Kafulila akiwa na nyaraka lukuki alizobainisha ni ushahidi wa ufisadi wa Escrow na IPTL, alisema jitihada zao za kupambana na ufisadi hazitakoma licha ya vitisho wanavyopewa.
“Tunataka Serikali kuchukua hatua madhubuti kuhusu ufisadi huu. Haturidhishwi na hatua zinazochukuliwa. Tutafanya utaratibu wa kuwasiliana na vyama ndani ya Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) kuona namna bora zaidi ya kulisukuma suala hili ili Watanzania waelewe namna nchi yao inavyotafunwa,” alisema.
“Kama chama, kwa kuwa Bunge na vyombo vya dola havioni umuhimu huo, tunamwachia Mungu, lakini chochote kikitokea tunafahamu ushiriki wa Serikali na vyombo vyake.”
Kwa upande wake Kafulila alisema hatishwi na mahakama wala wanaotaka ‘kumkata kichwa’ na yupo tayari kufungwa kwa sababu anachokifanya ni kwa masilahi ya umma.“Mimi naziomba taasisi zote zisizo za kiserikali, viongozi wa dini na wananchi waone kuwa hili jambo nao linawahusu.
Hii ‘assignment’ (kazi) siyo ya Kafulila pekee. Kama nchi nzima tutaungana, hao watakaokuwa wanaua, wataua wangapi?” alihoji Kafulila.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment