MFUMO MBOVU NDIYO UNAOATHIRI ELIMU YA TANZANIA.
MFUMO mbovu wa elimu hapa nchini, umetajwa kusababisha wanafunzi katika shule za umma kusoma kwa mtindo wa kupenya, hali inayosababisha kuwepo kwa idadi kubwa ya watu walioenda shule, lakini idadi ya wanaoelimika kushuka.
Ubovu wa mfumo huo pia umesababisha kukosekana kwa elimu ya kujitegemea na matokeo yake vijana wengi wanaomaliza masomo hawawezi kupata ajira kutokana na kupata mafunzo hafifu.
Akitoa mada yake inayosema “Elimu Tanzania; Nini Kifanyike”, katika kongamano la elimu lililofanyika Dar es Salaam, Mhadhiri wa Chuo Kikuu, Dk Kitila Mkumbo alisema Tanzania ina idadi kubwa ya watu wanaokwenda shule, lakini idadi ya wanaoelimika imeshuka.
“Kwenda shule na kuelimika ni vitu tofauti, watu walioelimika utawapima kwa vitu vidogo tu. Kuna mambo madogo tu ya kistaarabu watu wanashindwa, wako watu wamesoma lakini wanashadadia Sheria eti mtu akiua naye auawe huku sio kuelimika, mwenye elimu anaona umuhimu wa kupiga kura hii ni mifano michache ukiangalia utaona kama watu wamekwenda tu shule au wameelimika,” alisema.
Alisema pia kuondolewa kwa elimu ya kujitegemea, kumechangia matatizo kwenye sekta ya elimu, kwa kile alichoeleza vijana wanamaliza kusoma hawaajiriki.
Alibainisha kuwa utafiti wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Afrika, unaonesha kati ya vijana 10 wa Tanzania, wanne tu ndio wanaoweza kuajirika, kutokana na kupata mafunzo hafifu.
Dk Kitila alisema pia ili kuwa na elimu bora, lazima wawepo walimu bora na kuwataka Watanzania kuwaheshimu na kuwathamini walimu.
“Tukitaka kubadilisha mfumo mbovu wa elimu hapa nchini, lazima kwanza tuanze kwa kuwaheshimu na kuwathamini walimu...jamii ya sasa inawadharau sana walimu tofauti na miaka ya nyuma,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Alphonce Kessy, akitoa mada kuhusu elimu hapa nchini, alisema mfumo wa elimu uliopo sasa lazima ubadilishwe na uwe mfumo ambao unamwezesha mwanafunzi akimaliza aweze kujitegemea.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment