POLISI WAZIMA MAANDAMANO YA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DODOMA.
Polisi wakilinda Ofisi ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sinza jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwepo taarifa za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kutaka kufanya maandamano kwenda ofisi hizo kushinikiza kupewa fedha za mafunzo kwa vitendo. Picha na Rafael Lubava.
Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, lililazimika kupiga kambi kwa muda wa saa sita kwenye Jengo la Ofisi ya Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili kulinda usalama baada ya tetesi za kuwapo maandamano ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwenye ofisi hizo.
Sambamba na hilo, hiyo jana huduma zote zinazotolewa katika ofisi hizo zilisitishwa kwa muda kwa lengo la kuhami hali ya hatari.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kindondoni, Camellius Wambura alithibitisha kuwepo hali hiyo.
Wambura alisema walilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kupokea taarifa kuwa kuna vijana wa Udom walipanga kuandamana na kuleta fujo katika ofisi hizo.
“Tulipata taarifa kutoka kutoka idara yetu ya intelijensia kuwa hao vijana walitaka kufanya maandamano na vurugu kwenye ofisi za HESLB ili kushinikiza wapewe fedha,” alisema Wambura.
Alisema wakati wanaendelea kuhakikisha usalama wa jengo hilo, viongozi wa serikali ya wanafunzi walifanya mazungumzo ya amani na uongozi wa bodi na hakukuwa na vurugu wala maandamano.
“Walizungumza na kufikia muafaka mzuri. Lakini pia walibaini kuwa hakukuwa na mawasiliano mazuri baina ya uongozi wa Chuo, Bodi na wanafunzi wenyewe,” alisema.
Waziri Mkuu wa serikali ya wanafunzi, Philipo Mwakibinga alisema wamepanga kukutana pamoja kwenye ofisi hizo ili kupata ufafanuzi juu ya malipo ya fedha za mafunzo kwa vitendo (field).
“Sisi hatukuwa tumepanga kuandamana ila tulitaka tufike hapa kwa pamoja tupate taarifa stahiki juu ya mustakabali wa fedha za field,” alisema na kuongeza:
“Hadi sasa hakuna mwanafunzi aliyepata fedha wakati tulipaswa kuwa tumeshapewa kufikia Juni mwaka huu.”
Alisisitiza kuwa hatua yao haikulenga kufanya maandamano ila kufahamu hatima ya fedha hizo kwa vile muda umekwenda.
“Tumeona kimya na hakuna taarifa zinazoeleweka hadi sasa, tumeamua kuja kuuliza,” alisema Mwakibinga.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment