JESHI LA POLISI KUCHUNGUZA KIFO CHA BALOZI WA LIBYA.
JESHI la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, limeanza uchunguzi wa kifo cha Kaimu Balozi wa Libya nchini, Ismail Nwairat (39) kilichotokea Jumanne wiki hii baada ya kuruhusiwa kuingia katika eneo la tukio.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Alisema walishindwa kutoa taarifa haraka kutokana na kutokuwa na kibali cha kuingia ndani ya Ubalozi kufanya uchunguzi, ila kwa sasa wamekamilisha taratibu zote na hatua za upelelezi zimeanza kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa Libya.
“Suala la kuingia ndani ya ubalozi wa nchi ya mtu, ni kama kuingia katika nchi ya watu hivyo ni vyema kufuata utaratibu unaotolewa na wahusika,” alisema Kova.
Alisema kuwa uchunguzi watakaoufanya ni pamoja na kujua sababu za Kaimu Balozi huyo kujiua na kama alikuwa anatishiwa au alikuwa na tatizo la kifamilia.
Kova alisema wataalamu wa vifo vya aina hiyo kutoka Jeshi la Polisi, tayari wameanza kushirikiana na Ubalozi wa Libya na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ili kukamilisha upelelezi na hatua nyingine muhimu katika tukio hilo na watatoa taarifa mapema baada ya kukamilisha upelelezi.
Wakati Kova akielezea hatua za upelelezi, Serikali imeelezea kushitushwa na kifo hicho, kwa kuwa tukio hilo si la kawaida na ni mara ya kwanza kutokea nchini.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili kuhusu utaratibu wa kusafirisha mwili wa balozi huyo.
“Kwa kweli tukio hili limetushtua sisi kama Tanzania kwa kuwa kwanza si jambo la kawaida kwa mwanadiplomasia kujiua, lakini pia haijajulikana kwa nini kiongozi huyu amechukua uamuzi huo wa kujiua,” alisema Mkumbwa.
Alisema jambo la msingi kwa sasa ni hatua iliyochukuliwa na Ubalozi wa Libya nchini, ya kuihakikishia Tanzania kuwa kifo hicho hakina uhusiano na nchi kama mwenyeji.
“Tuna imani sasa baada ya kuhakikishiwa kuwa kama nchi mwenyeji hatuna lawama wala hatuhusiki kwa namna yeyote na kifo hicho, ushirikiano wetu baina ya Libya na Tanzania utaendelea kama kawaida,” alisema.
Kuhusu maandalizi ya kusafirisha mwili wa balozi huyo kwenda nchini Libya kwa maziko, Mkumbwa alisema bado taratibu zinaendelea kutafuta usafiri na zitakapokamilika, itabainishwa lini anasafirishwa.
Balozi huyo, alikufa juzi saa saba mchana baada ya kujifungia ofisini kwake na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto.
Baada ya kusikia mlio wa risasi, maofisa ubalozi walivunja mlango na kumkuta Balozi Nwairat ameanguka chini, wakamkimbiza hospitali ya AMI Oysterbay, ambako alitangazwa kuwa alishakufa kitambo.
Kwa sasa mwili wa kiongozi huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment