BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

UKAWA TAFAKARINI USHAURI WA ASKOFU WA KANISA KATOLIKI, SI JAMBO ZURI KUPIGA KELELE NJE YA BUNGE.

 
By Shadrack Sagat.
WAZO LANGU !!.

KATI ya mambo makubwa kufanyika nchi hii, ambayo yanasubiriwa kwa hamu na Watanzania, ni kuwepo kwa Katiba mpya ambayo inatarajiwa kuandikwa pindi itakapopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Lakini, kuandikwa kwa katiba hiyo, kumeingia shaka kutokana na kundi moja muhimu, ambalo linaundwa na wajumbe wa Bunge hilo kutoka vyama vya upinzani kususia Bunge hilo, kwa kile wanachodai kuwa Chama Cha Mapinduzi kimeteka mchakato huo wa Katiba.

Kundi hilo ambalo wanajipambanua kama Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), baada ya kususia Bunge waliamua kwenda kwa wananchi, kufanya mikutano kuwaambia sababu ya kususia Bunge hilo.

 
Na tumeendelea kuwasikia viongozi wa kundi hilo, Profesa Ibrahim Lipumba, Freeman Mbowe na James Mbatia, wakijinasibu kuwa kamwe hawatarudi kwenye bunge hilo hadi hapo maoni ya wananchi, yatakapoheshimiwa na wajumbe wa CCM.

Uamuzi wa Ukawa umepokelewa kwa maoni tofauti na Watanzania. Wapo wanaowaunga mkono kuwa hatua waliyofanya ni sahihi, kwa vile kuna watu hawaheshimu maoni ya wananchi yaliyoko kwenye rasimu ya Katiba mpya.

Lakini, pia kuna kundi ambalo linawaona Ukawa kama watu ambao sio wazalendo, wabinafsi na waroho wa madaraka kwa kujiondoa kwenye bunge hilo, kwa vile tu msimamo wao wa serikali tatu, unapingwa na wajumbe wa CCM.

Binafsi nimekuwa nikifuatilia kwa makini malumbano yanayotolewa kati ya CCM na UKAWA, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kuwa ndio chanzo cha kutaka kuvuruga upatikanaji wa Katiba mpya.

Juzi Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad amesikika akisema kuwa kuna umuhimu wa Katiba mpya, kupatikana na itawezekana tu iwapo kutakuwa na mazungumzo ya pande zinazohusika kwenye mchakato huo.

Kwa maoni ya Maalim Seif ni kwamba tayari Serikali imetumia fedha nyingi za walipa kodi, hivyo mchakato huo usipopatikana itakuwa ni hasara kubwa kwa taifa.

Lakini, pia juzi Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Severine Niwemugizi, amewashauri UKAWA kurejea bungeni bila masharti yoyote, badala ya kuendelea kupiga kelele nje ya Bunge.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda naye amekuwa anasihi wapinzani hao kutambua dhamana yao ya kuwapatia Watanzania Katiba mpya. Kitu cha msingi ambacho askofu huyo, aliwatahadharisha UKAWA na CCM ni kuhakikisha wanaheshimu maoni ya wananchi, badala ya kuyapiga teke.

Pia, askofu huyo alikemea wabunge hao, kudharau kazi kubwa iliyofanywa na Tume ya Marekebisho ya Katiba, iliyoundwa na wasomi na Watanzania wazalendo.

Binafsi nawaunga mkono askofu pamoja na Maalim Seif, kwamba mazungumzo yanahitajika kuhakikisha Katiba mpya inapatikana. Lakini, pia wajumbe wa Bunge hilo, sio vizuri kupiga kelele nje ya jukwaa la Bunge badala yake wapambane ndani.

Kitendo cha UKAWA kuendelea kuwa nje ya Bunge, kutatoa fursa kuwa na Katiba yenye mtazamo wa chama kimoja tu nyakati ambazo kwa sasa hatuko huko.

Lakini, pia hili la kuheshimu maoni ya wananchi, nalo ni la msingi, rasimu ya Katiba imetokana na maoni ya Watanzania, sio vizuri kuyabeza kwa sababu mwisho wa siku ni Watanzania ndio watakaoenda kuipigia kura Katiba, itakayopitishwa na bunge hilo.

Hili litafanikiwa tu iwapo wajumbe wa bunge hilo, watavaa uzalendo na kuhakikisha kuwa katiba itakayoenda kuandikwa, sio ya CCM na UKAWA, bali ni Katiba ya Watanzania itakayotumika kwa miaka mingine 50 ijayo.

Hivyo kuna haja ya makundi haya mawili, kuanza kufanya mazungumzo kabla ya vikao vya Bunge, kuanza ili pale ambako kuna tofauti wazirekebishe ili wanapoenda kujadili rasimu hiyo ya Katiba, kuwe na maridhiano ya kujenga nchi na sio kubomoa umoja wetu.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: