Baadhi ya wajawazito wakisubiria kujifungua katika hospitali ya Butiama.
Baadhi ya wajawazito wanaojifungua kwenye hospitali ya Palestina, jijini Dar es Salaam wamedai hujigharamia vifaa vya kujifungulia, dawa pamoja na posho za wauguzi.
Walisema wanalazimika kubeba vifaa vya kujifungulia vikiwamo sindano, pamba, glovu, kidonge cha uchungu, dripu, sindano ya kushonea, dawa na fedha posho za wakunga wanaowahudumia.
Wajawazito hao waliliambia gazeti hili kuwa, inapotokea dharura wakati wa kujifungua, wauguzi bila kujali hali ya mgonjwa wamekuwa wakidai ‘chochote’ kwa ajili ya vifaa endapo vile alivyonunua awali havikutosha.
Mmoja wa wanawake hao, aliyejifungua hospitalini hapo (jina tunalo) alisema siku aliyokwenda kujifungua akiwa wodini aliulizwa kama amebeba mahitaji hayo.
“Nilikuwa na glovu, pamba na wembe, bila kutegemea nilitajiwa vitu vingine nilivyotakiwa kuwa navyo… muuguzi aliniambia wanahitaji kidonge cha uchungu na dripu,"
“Ilitakiwa sindano ya kushonea iwapo nitahitajika kushonwa na dawa ya sindano, pamoja na panadol nililazimika kutoa Sh. 20,000 ili akaninunulie, " alisema.
Alieleza kuwa hata hivyo mtoto wake alikuwa mkubwa akalazimika kuongeza Sh. 10,000 ya kununua dripu, mpira wa kutolea mkojo na sindano ya kuzuia kupoteza damu.
"Kitu ambacho sikwenda nacho hospitalini hapo ni kitanda ambacho nilikikuta wodini na kwenye chumba cha kujifungulia, vifaa vingine vyote nilinunua. Cha kushangaza zaidi niliambiwa nitoe hela za kununua panadol nilishangaa sijui nazo hazikuwepo," alisema.
RUSHWA
Kuhusu vitendo vya rushwa, mzazi mwingine alisimulia yaliyomkuta akiwa wodini baada ya kujifungua, kuwa mmoja wa wauguzi hospitalini hapo, alifika na kutangaza kuwa, "wale watu wangu wa jana nimekuja kuwaona," alipita kila kitanda kuchukua hela.
Alisema bila hofu alipitia kila mzazi aliyemsaidia kujifungua na kuchukua fedha za wanawake hao hata kama walikuwa hawana chakula.
WENYE VVU WALIA
Mwingine aliiambia NIPASHE kuwa wakati wa kupimwa alikutwa na Virusi Vya Ukimwi (VVU), lakini kilichomuudhi ni utoaji wa majibu aliosema haukumridhisha.
“Baada ya ushauri nasaha tulitolewa damu lakini muda wa majibu haukuwa mzuri kwangu,” alisema na akuongeza:
“Tuligawanywa makundi mawili la kwanza lilipewa majibu yao na kuondoka kwa nyuso za furaha, tuliobaki tuliitwa tukaambiwa mmeathirika, yaani haikuwa siri kati ya mgonjwa na mhudumu wa afya, ninachojua uwe umeathirika au la majibu ni siri,” alieleza kwa masikitiko.
MGANGA MKUU
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Palestina Dk. Benedict Luoga, alilitembeza gazeti hili maeneo yaliyolalamikiwa ikiwa ni pamoja na wodi za wazazi, kliniki na chumba cha dawa.
Kwa upande wa dawa zilikuwepo pamoja na vifaa tiba lakini ndani ya wodi ya wazazi mkuu wa eneo hilo, alithibitisha kuwa wajawazito huambiwa wabebe vifaa kama wembe, glovu na pamba ambavyo wakati mwingine hutumiwa.
Kwa upande wake Dk. Luoga akijibu malalamiko ya wanawake hao alisema hayajawasilishwa rasmi ofisi kwake.
“Ukipita kwenye majengo ya hospitali utaona matangazo kuhusu huduma zinavyotolewa, tangazo linaonyesha wapi pa kulipia huduma, upingaji vitendo vya rushwa na kuelekeza sehemu za kutoa malalamiko,” alisema.
Dk. Luoga aliwataka wagonjwa wanaofanyiwa vitendo hivyo alivyosema ni kinyume cha taratibu, kupeleka taarifa kwenye kitengo cha malalamiko ofisi ya ustawi wa jamii hospitalini hapo ili hatua zichukuliwe dhidi ya watuhumiwa.
“Hospitali hii inafuata sera ya afya inavyosema, kujifungua ni bure, wajawazito hawaambiwi waje na vifaa.Vifaa vinatoka serikalini na vingine hospitali inavinunua, kila mwaka tunapata fedha kutoka serikali kuu na zile za wafadhili.
Kwa mfano mwaka jana serikali ilitupatia ruzuku ya zaidi ya Sh. Milioni 113.6 na fedha ya wafadhili ilikuwa zaidi ya Sh. Milioni 500,” alisema Dk Luoga.
DHARURA
Aidha, alisema mjamzito anapoambiwa aje na vifaa ni kwa ajili ya tahadhari endapo itatokea dharura vinaweza kutumika lakini siyo wakati wote.
Alikanusha kuwa hospitali yake inawalazimisha wajawazito kununua kidonge cha uchungu, drip, sindano ya kushonea na dawa zake.
“Wakati mwingine tunawapokea baadhi ya wajawazito ambao hawajahudhuria kliniki hapa…Labda wanaambiwa wabebe vifaa hivyo kwenye kliniki walizohudhuria.”
Alisema pengine ndiyo sababu wanapokuja Palestina wanakuwa navyo na kusisitiza kuwa jambo hilo halipo na kama wapo walioambiwa wabebe wapeleke malalamiko yao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / WAJAWAZITO WAJINUNULIA VIFAA VYA KUJIFUNGULIA KATIKA HOSPITALI YA PALESTINA JIJINI DAR ES SALAAM, KAMA MJAMZITO HANA VIFAA......!!!!.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment