BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WALIPULIWA NA BOMU WAKATI WAKILA CHAKULA CHA USIKU KATIKA MGAHAWA TANZANIA.

 
Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha, Catherine Magige akiangalia kidonda cha Deeptak Gupta, ambaye ni mmoja wa majeruhi nane wa mlipuko wa bomu, uliotokea usiku wa kuamkia jana katika mgahawa wa Vama Traditinal Indian Cuisine jijini Arusha. (Na Mpigapicha Wetu).

WATU wanane, wanne wakiwa wa familia moja, wamelipuliwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni bomu na kujeruhiwa vibaya wakati wakipata chakula cha jioni katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine, jijini Arusha.


Mgahawa huo ulioko mtaa wa Uzunguni jirani na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, ulilipuliwa saa 4.30 usiku wa kuamkia jana.

Tukio hilo limekuja siku nne tangu Shehe na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kiislamu ya Answar Muslimu Youth Centre Kanda ya Kaskazini, Sheikh Sudi Ally Sudi na mgeni wake Muhaji Kifea walipolipuliwa kwa bomu nyumbani, eneo la Majengo Chini jijini Arusha wakati wakila daku.

Familia yajeruhiwa
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Selian, mjini hapa, Dk Poul Kisanga alisema miongoni mwa majeruhi, mmoja yuko katika hali mbaya na yuko katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Majeruhi huyo, Deepak Gupta (25) , kwa mujibu wa mganga huyo, amepoteza mguu wa kushoto kutokana na bomu hilo. Majeruhi huyo, ni mmoja wa wanafamilia iliyokuwa ikipata chakula ndani ya mgahawa huo.

Alikuwa na mama yao, Manisha Gupta (36), baba Mahush Gupta (42) na mdogo wake wa kike, Manci Gupta (14). Majeruhi wengine Mganga Mkuu huyo alisema katika majeruhi hao pia kuna mtoto mwingine wa kiume aliyetambuliwa kwa jina la Ritwik Khaalelwal (13).

Wengine ni Vinod Suresh (37) ,Raj Rajin (30) na Prateek Javel ambaye umri wake haukufahamika mara moja. Dk Kisanga alisema kuwa majeruhi wote ukiachilia mbali aliyekatwa mguu, wana vipande vingi vya chuma mwilini ambapo madaktari wanaendelea kuvitoa na hali zao zinaendelea vizuri.

Kisanga ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Tiba katika Hospitali hiyo, alisema majeruhi hao walifikishwa hospitalini hapo juzi saa 5 usiku.

Watano kati yao walikuwa na hali mbaya na walipelekwa moja kwa moja katika chumba cha upasuaji na upasuaji huo ulifanyika hadi alfajiri ya jana.

Mashuhuda
Wakisimulia tukio hilo, baadhi ya watu waliokuwa katika mgahawa huo wakipata chakula cha usiku walisema ghafla walisikia kishindo kikubwa cha kitu hicho kinachodaiwa ni bomu kikitokea dirishani na kutua chini ya meza mojawapo.

Katika meza hiyo ambayo majeruhi walikuwa wamekaa, chembe chembe za bomu hilo zilisambaa na mguu wa mmoja wao, ulikatika papo hapo.

Kwa mujibu wa shuhuda ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema baada ya mlipuko walipiga kelele kuomba msaada kwa kupigia marafiki simu ambao walifika kwa wakati na kuwapeleka majeruhi katika Hospitali ya Rufaa ya Selian.

Ilielezwa kwamba muda mfupi baadaye, polisi na vyombo vingine vya usalama vilifika eneo la tukio kufanya kazi ya uchunguzi wa awali.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, walifika hospitalini Selian usiku kujulia hali majeruhi.

Tukio la sita
Tukio hili la bomu, ni la sita kutokea jijini Arusha ndani ya kipindi cha mwaka na nusu. Katika matukio hayo, watu wanane wamepoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu.

Mfululizo wa matukio hayo katika jiji hilo hilo ambalo ni kitovu cha utalii nchini, umesababisha sintofahamu miongoni mwa wakazi wake ambao katika mahojiano, wametaka Kamati ya Ulinzi na Usalama chini ya Mkuu wa Mkoa pamoja na vyombo vya dola kutoa majibu juu ya sababu za mji huo kuandamwa na mabomu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema, ‘’Kwa leo siwezi kuzungumzia tukio hili kwa kuwa DCI atalizungumzia jijini Dar es Salaam pamoja na kwamba tukio lenyewe limetokea mkoani kwangu.’’

DCI azungumza
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Kamishina Issaya Mngulu, alisema Polisi inashikilia watuhumiwa wawili kwa uchunguzi zaidi kwa tuhuma za kuhusika na mlipuko huo wa juzi.

“Katika mlipuko huo uliotokea maeneo ya Uzunguni katika mgahawa wa Vama Traditional Indian Cuisine jirani na viwanja vya Gymkhana watu wasiojulikana walirusha bomu ndani ya mgahawa huo kupitia mlangoni na kujeruhi watu wanane,” alisema.

Alisema watu hao wanaendelea kupatiwa matibabu na mmoja hali yake ni mbaya na inasadikiwa amepelekwa kutibiwa Nairobi. Hata hivyo alisema pamoja na juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanywa na jeshi hilo kuhakikisha kwamba nchi inaendelea kuwa salama na yenye utulivu, bado kumeendelea kuwa na matukio ya kiuhalifu yakiwemo ya milipuko.

“Kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi nchini linaendelea na upelelezi wa kina ili kuhakikisha kwamba wote walioko kwenye mtandao huo wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.” alisema.

25 washikiliwa
Hata hivyo akizungumzia pia matukio mengine ya milipuko ya mabomu yaliyotangulia jijini Arusha na Zanzibar, Mngulu alisema watu zaidi ya 25 wanaosadikiwa kujihusisha na vitendo hivyo wamekamatwa.

Alisema watuhumiwa hao wamekamatwa maeneo mbalimbali nchini. Kati ya hao, 14 wamekamatwa wakihusishwa na tukio la Zanzibar na sita wakihusishwa na mlipuko uliotokea Julai 3 nyumbani kwa Shekhe Sudi Ally Sudi mkoani Arusha.

Mngulu alitaka wananchi kuchukua hadhari kwa kuepuka mikusanyiko isiyokuwa ya lazima. Aidha alitaka wawe makini na mtu ama kitu chochote watakachotilia shaka.

Pia alitaka wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia kubaini na kukamata wahalifu wote walioko kwenye mtandao huo. Wanaoandaa mikusanyiko wameshauriwa kuweka vifaa vya kisasa vya kuzuia uhalifu kwa kuwa imebainika wahalifu wanalenga maeneo yenye mikusanyiko.

Katika hatua nyingine Mngulu akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua endapo watuhumiwa hao wanahusiana na kundi lolote, alisema hawana uthibitisho na jeshi limejizatiti kiulinzi.

Kwa nini Arusha, Zanzibar?
Alipoulizwa sababu za vitendo hivyo vya ulipuaji mabomu kufanyika Arusha na Zanzibar, DCI alisema lengo ni kusababisha tishio kwa wageni wasitembelee maeneo hayo kwa kuwa ni miji ya kiutalii.

Hata hivyo alisema Jeshi la Polisi linajitahidi kuimarisha ulinzi kuhakikisha wageni wanaendelea kutembelea miji hiyo. Kuhusu madai ya baadhi ya viongozi wa Chadema kutaka kuundwa chombo ili waweze kutoa ushahidi wa milipuko, alisema yako maeneo mengi wanaweza kupeleka ushahidi wao ikiwemo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

“Hatujui wao wana wema gani hadi washindwe kujieleza. Tena ni watu wanaotarajia kuwa viongozi. Hivi wataendelea tu kuficha ushahidi?”HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: