BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CHADEMA WANAPENDA KUANDAMANA, LAKINI VIONGOZI WAO HAWAPENDI KUFUATA UTARATIBU NA BARAKA ZA JESHI LA POLISI !.

http://api.ning.com/files/BvKmtVMaeBZ6Lq9AtgekaAyfce1fS-s0XBn3unrZcPLW6l9ThgBQmoK3kvLJx7bHzKRA-F2SkewTj3rd0E-luB1VL8SKKe*j/2.jpg
Baadhi ya wafuasi wa Chadema wakiandamana mkoani Morogoro.Picha ya maktaba.


LICHA ya kutakiwa kufuata taratibu kabla ya kutimiza azma yao ya kuandamana nchi nzima, viongozi wa Chadema wa mikoa mbalimbali wamesisitiza kuendelea kuunga mkono dhamira ya Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe ya kuandamana na kugoma bila kikomo ili kulipinga Bunge Maalumu la Katiba, linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma.

Maandamano hayo yamekosa baraka za Jeshi la Polisi nchini, ambalo limeeleza kuwa hayana msingi, kutokana na ukweli kwamba Bunge la Katiba lipo kwa mujibu wa sheria, hivyo linapaswa kuendelea na shughuli zake na si kupingwa kienyeji, huku maandamano hayo yakitajwa yanaweza kusababisha kuvunjika kwa amani ya nchi.

Katika kuitikia wito wa kuandamana, mikoa mitatu ya Kanda ya Kaskazini jana ilishindwa kutimiza malengo ya kuandamana, baada ya kubanwa na Jeshi la Polisi.

Mkoani Shinyanga, maandamano yaliyotarajiwa kuanza saa 2 asubuhi jana, yalikwama baada ya wafuasi wa chama hicho kujikuta wakiwa wamezingirwa na polisi kila kona ya Mji wa Shinyanga.

Yalipangwa kuanzia ofisi za chama hicho na kuelekea katika viwanja vya Shycom, ambako wangefanya mkutano wa hadhara. Lakini, yaliyeyuka huku viongozi wake waliopaswa kuyaongoza, wakishindwa kutokea.

Akitetea hali hiyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Shinyanga, Peter Machanga alisema; “Kutangaza tumetangaza kweli, ila maandamano hayakuwepo, tulikuwa tunawaweka sawa wananchi kwamba kutakuwa na maandamano, tarehe na siku ya maandamano itatangazwa.”

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mussa Athumani alisema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga halijatoa kibali kwa chama hicho kufanya maandamano hivyo kuwataka wananchi kufuata utii wa sheria bila shuruti, kwa kutoandamana.

Wakati hali ikiwa hivyo mkoani Shinyanga, katika mkoa jirani wa Simiyu, chama hicho kimeendelea na msimamo wake wa kufanya maandamano ya kupinga vikao vya Bunge hilo la Katiba, na watendaji wake wamesema leo wanatarajiwa kufanya maandamano hayo.

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Simiyu, Mshuda Wilson aliyesema maandamano yao yatakuwa ya amani na kulitaka Jeshi la Polisi kutotumia nguvu kuzuia, kwani ni haki yao kikatiba kufanya maandamano.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Venance Kimario alisema Jeshi lake halitambui kuwepo kwa maandamano hayo, kwani limeshayazuia.

Mkoani Mara, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi ya Tarime/Rorya, Benedict Mambosasa alisisitiza licha ya kupokea maombi ya Chadema, Jeshi lake limeyakataa kwa sababu za kiusalama.

“Hatuwezi kuwaruhusu kwa sababu wanachokipinga, yaani Bunge la Katibu lipo kisheria. Hatutawaruhusu,” alisema.

Maandamano yadharauliwe

Wakati hayo yakitokea sehemu mbalimbali nchini, Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wametaka Jeshi la Polisi nchini, kudharau maandamano ya Chadema, kwa kuwa inavyoonekana hayana wafuasi.

Hoja hiyo ilianzia jana kwa Mjumbe wa Bunge hilo, Paul Makonda, wakati akichangia hoja ya marekebisho ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, ili kuruhusu wajumbe walio nje ya ukumbi wa Bunge na nje ya nchi kupiga kura na upigaji kura uchukue muda mfupi.

Makonda alianza kwa kuwaonea huruma vijana walioshawishiwa kujiunga katika maandamano hayo, wakati aliyeitisha, Mbowe, `amekimbilia’ Afrika Kusini, ambako alidai anaponda raha katika Hoteli ya Dola 700, sawa na zaidi ya Sh milioni moja kwa siku.

Makonda alitaka Jeshi la Polisi kuwadharau kwa kuwa hawawezi kupata wafuasi, kwani kijana akipinga Bunge Maalumu, atakuwa anapinga kuwepo kwa Baraza la Vijana ambalo limeingia katika Katiba.

Mjumbe mwingine, Dk Hamis Kigwangala, alisema Chadema waliishiwa hoja, kwa kuwa wakati wa kuunda Sheria ya Mchakato wa Katiba, walijipanga kuhakikisha wanatumia vilivyo Bunge Maalumu la Katiba.

Kwa mujibu wa Kigwangala, baada ya rasimu kubeba mapendekezo yao, wakageuka wakitaka Bunge Maalumu, lisibadili chochote katika rasimu hiyo, wakati kipengele hicho cha kuruhusu Bunge kubadili rasimu, walikitetea wao hivyo ni bora wapuuzwe.

Dk Charles Tizeba alisema wakati walipokuwa wakiunda Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, walikubaliana kuwa wajumbe kuwapo katika Bunge Maalumu au wasipokuwepo katika Bunge, haitaathiri kura.

Mjumbe mwingine, Constantine Akitanda, alishangaa Ukawa kutoka nje ya Bunge huku akimnukuu mchambuzi mashuhuri wa mambo, Profesa Kitila Mkumbo, kwamba waliotoka nje ya Bunge hilo, walikuwa wameishiwa hoja.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: