MADEREVA WA DALADALA WAFANYA MGOMO WAKIISHINIKIZA SERIKALI KUWAONDOA MADEREVA WA TEKSI, PIKIPIKI NA BAJAJ KIGOMA.
Sehemu ya wanafunzi wakitelemka katika lori baada ya kuwepo kwa mgomo wa daladala Manispaa ya Morogoro hivi karibuni.Picha ya maktaba.
Wamiliki wa daladala mkoani Kigoma jana waligoma kupakiza abiria kwa muda usiojulikana kwa madai kuwa Serikali imepuuza madai yao ya kuwaondoa madereva teksi, pikipiki na bajaji katika vituo vya daladala.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Kigoma (KIBOA), Hussein Kalyango, alisema wameamua kusitisha huduma kwa kushirikiana na vyama vya usafirishaji Kiboa, Kibota na Umaki kutokana na kupuuzwa na uongozi wa mkoa.
Alisema wamechukua uamuzi huo baada ya Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji na Kamati ya Usalama barabarani kushindwa kuziondoa teksi, bajaji na pikipiki kwenye vituo hivyo.
“Malalamiko yetu sisi kama wafanya biashara watoa huduma kwa abiria ni kuhusiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupandisha kodi kupanda kutoka 364,000 kwenda 728,000 na bajaji kufanya kazi kama daladala inapita vituoni na kuita abiria kwa Shilingi 500 tofauti ni Shilingi 100, unajikuta zinashindwa kufanya kazi kutokana na bajaji kuwa daladala,” alisema.
Aidha, alisema kila wakati wamekuwa na mgogoro wa kugombea abiria kati ya madereva wa teksi na bajaji na madereva wa dalala na mabasi yanayotoa huduma Wilaya ya Kasulu, Kibondo, Kakonko, Buhigwe na Uvinza pamoja na maeneo mengine ya Ilagala, Kazuramimba na Manyovu.
Aliitaka mamlaka husika kuwaondoa madereva hao kwenye vituo hivyo na kuwatengea maeneo mengine kwa ajili ya kusubiri abiria wao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Jafari Mohamed, alithibitisha kutokea mgomo huo na kuwataka mamlaka husika za utoaji wa leseni kuwafutia leseni na kudai kuwa yeye ameimarisha ulinzi kuhakikisha kuna amani na utulivu.
Abiria Hawa Lameki (50), ambaye ni mfanya biashara wa samaki na dagaa, alisema: “Usumbufu tuliyoupata leo (jana) kutoka Ujiji na teksi kufika Kigoma Mjini kwa Shilingi 1,000 na kutembea kwa mguu hadi Kibirizi.
Nimenunua samaki Kibirizi nikarudi Kigoma Mjini kwa mguu tukakuta teksi zimepandisha nauli 1,500 kwenda Ujiji, huu ni usumbufu, akina mama tunaomba watusaidie viongozi warekebishe hili suala liishe.”
Juhudi za kumpata Afisa Mfawidhi wa Sumatra, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Meya wa Manispaa hiyo na Kamati ya Usalama Barabarani na Mkuu Wilaya ya Kigoma ziligonga mwamba kutokana na kuwa na kikao cha usuluhishi. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment