UGONJWA WA MOYO NAMNA UNAVYOWATESA VIJANA NA KUSABABISHA VIFO, KUMBE UNADHIBITIWA KWA MAMBO MANNE TU.
NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
MAISHA ya vijana wengi wa Kitanzania yapo hatarini kutokana na unywaji pombe na uvutaji sigara kupita kiasi, unaotajwa kuwa miongoni mwa sababu za kupatwa na ugonjwa wa moyo.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Robert Mvungi, alipozungumza na waandishi wa habari katika Siku ya Moyo Duniani iliyoadhimishwa kidunia jana.
Dk. Mvungi alisema wagonjwa wa moyo wanaofika kupata tiba katika hospitali hiyo ni wastani wa watu 20,000 kwa mwaka na asilimia kubwa kati yao ni vijana.
Hospitali ya Muhimbili
Alisema hali hiyo inachangiwa na mtindo wa maisha ambao wengi wao wamekuwa wakiishi kwa kunywa pombe kupita kiasi, uvutaji wa sigara, kula vyakula vyenye mafuta ya wanyama kwa wingi pamoja na kutokufanya mazoezi.
“Tumekuwa tukipokea watu 20,000 kwa mwaka hapa Muhimbili ambao wanasumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kati yao idadi kubwa huwa ni vijana,” alisema Dk. Mvungi.
Kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa, Dk. Mvungi kupitia Kitengo cha Moyo wameamua kuhamasisha jamii kula vyakula ambavyo havina athari kwao na kuepukana na tabia ya kutokufanya mazoezi ili kuondoa uwezekano wa kupata ugonjwa huo.
“Huu ni ugonjwa hatari iwapo watu hatutachukua tahadhari, kwa sababu kila mwaka takribani watu milioni 17.3 duniani wamekuwa wakifariki dunia kutokana na kuugua ugonjwa huo,” alisema.
Septemba 29 kila mwaka, dunia nzima huadhimisha Siku ya Ugonjwa wa Moyo ambayo huambatana na kaulimbiu mbalimbali kwa lengo la kuielimisha jamii kujua na kufuatilia undani wake.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Muhimbili, Dk. Delila Kimambo, alisema maadhimisho kwa mwaka huu yamepewa kaulimbiu isemayo ‘Jenga afya ya moyo, kazini, majumbani na michezoni’, ikilenga kuhamasisha jamii kujenga mazingira mazuri katika kila eneo kwa kukwepa mambo ambayo yanaweza kusababisha kuugua ugonjwa huo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa ugonjwa wa moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.3 kila mwaka.
Ugonjwa huo ni wa pili duniani baada ya malaria unaongoza kwa kusababisha vifo vya watu.
SABABU ZA UGONJWA WA MOYO
Mienendo mibovu ya maisha ikiwamo uvutaji sigara, ulevi, ukosefu wa mazoezi ya mwili na chakula bora kwa kiasi kubwa vinachangia ongezeko la vifo vitokanavyo na ugonjwa huo nchini.
Wataalamu wa afya wanataja sababu nyingine kuwa ni umri, jinsia, historia ya familia, shinikizo la damu, kisukari, msongo wa mawazo na uchafu.
Takribani asilimia 80 ya vifo vya mapema vitokanavyo na ugonjwa wa moyo vinaweza kuzuilika kwa kuepuka sababu hizo hatarishi.
TAFITI
Utafiti uliofanyika mwaka 2012 na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na WHO, unaonyesha kuwa asilimia 26 ya Watanzania wanakabiliwa na ugonjwa wa moyo huku asilimia 20 kati yao wakiwa wanawake.
Taarifa za Wizara ya Afya zinaonyesha kuwa asilimia 92.6 ya Watanzania wenye ugonjwa huo hawapo kwenye matibabu licha ya kutambua kuwa wanaugua.
WHO inaeleza kuwa takriban asilimia 40 ya watu wazima katika Bara la Afrika wanaugua ugonjwa huo.
0 comments:
Post a Comment