WANAJESHI WA ISRAEL WAJIUA, NI WALE WALIOSHIRIKI VITA VYA GHAZA PALESTINA.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeanza uchunguzi kuhusiana na vifo vya wanajeshi watatu wa utawala huo walioamua kujiua baada ya kurejea kwenye vita kati ya utawala huo na Wapalestina wa eneo la Ukanda wa Ghaza.
Polisi ya Jeshi la utawala wa Israel imetangaza kuwa, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wanajeshi hao walijiua kutokana na matatizo ya kiakili na kisaikolojia yaliyosababishwa na ushiriki wao kwenye vita vya Ghaza.
Taarifa zinasema kuwa, wanajeshi hao wa Israel waliamua kujiua kwa kujifyatulia risasi na kwamba silaha walizotumia zilipatikana zikiwa pambizoni mwa viwiliwili vyao. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanajeshi wawili kati ya watatu walijiua kwenye kambi ya kijeshi iliyoko karibu na mpaka wa Ukanda wa Ghaza.
Nalo gazeti la Maariv linalochapishwa huko Israel limemnukuu mmoja kati ya maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Israel katika hospitali ya wagonjwa wa akili akisema kuwa, jumla ya wanajeshi wanane wa Israel walijiua mwaka jana.
Afisa huyo mwandamizi wa jeshi amesema kuwa, jeshi la Israel halitangazi takwimu za wanajeshi wake wanaojiua kutokana na matatizo ya kiakili.http://kiswahili.irib.ir/
0 comments:
Post a Comment