WAZIRI MUHONGO AZUSHIWA KUWACHONGANISHA WAKAZI WA LINDI NA MTWARA JUU YA GESI.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo
KATIKA hatua isiyo ya kawaida Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezushiwa kuandika meseji za simu za mkononi zenye mwelekeo wa kuwagawa wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara katika kunufaika na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka mikoa hiyo hadi Dar es Salaam.
Hata hivyo, wakati mkakati huo wa siri ukifanywa na watu wasiojulikana, tayari mamlaka za kiserikali katika mikoa hiyo, zimebaini mbinu hizo na kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), elimu imeanza kutolewa kuepusha uwezekano wa kuzuka kwa vurugu.
Hayo yalibainika wakati Bodi ya Wakurugenzi ya TPDC, ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Michael Mwanda na Menejimenti chini ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu, James Andilile, walipofanya ziara kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya bomba hilo la gesi kutoka Madimba mkoani Mtwara na Songosongo, Lindi, mradi ambao umeelezwa kukamilika ifikapo Desemba, mwaka huu.
Akitoa taarifa ya namna Mkoa wa Lindi unavyoendelea kushiriki katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi huo mbele ya Bodi hiyo ya TPDC, Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Abdallah Chikota alisema uzushi huo dhidi ya Waziri Muhongo ulibainika hivi karibuni, lakini umekomeshwa.
Alisema watu wasiojulikana, wamebuni meseji mbalimbali za simu za mkononi, ambazo zinaonesha Waziri Muhongo akitoa upendeleo mkubwa kwa vijana wa Mtwara katika kunufaika na mradi huo, huku akidaiwa kuwapuuza wa Lindi, jambo ambalo si la kweli.
Miongoni mwa meseji hizo ni ile inayoonesha Waziri Muhongo akiwasiliana na Balozi wa Nigeria, kuomba nafasi za masomo kwa vijana wa Mtwara bila ya kuwahusisha wenzao wa Lindi na kuibua hisia kuwa anawabagua na hawapendi.
“Siku moja ghafla walifika hapa vijana kama 30 na kujitambulisha kwamba ni vijana wasomi wa Mkoa wa Lindi. Mkuu wa Mkoa (Ludovic Mwananzila) akasema tukae tuwasikilize nini shida yao.
“Katika maelezo yao tukabaini kuwa wana meseji kwenye simu zao ambazo zinaonekana kama zimeandikwa na Waziri Muhongo, moja ikionesha kuwa anawasiliana na Balozi wa Nigeria, akiomba nafasi za masomo kwa vijana wa Mtwara tu ili wafadhiliwe na Serikali ya Nigeria.
“Halafu kukawa na meseji nyingine ikieleza kuwepo kwa nafasi 500 za ajira TPDC, lakini wakipewa nafasi vijana wa Mtwara. Nyingine ilizungumzia kuwepo kwa nafasi kama 200 katika kampuni moja ya gesi lakini kwa vijana wasomi wa Mtwara tu.
“Kwa ujumla ni kwamba meseji hizo zinamuonesha Waziri Muhongo akiwasiliana na viongozi mbalimbali wa kimataifa kuomba ama nafasi za masomo au kuomba ajira lakini akiwalenga vijana wa Mtwara tu,” alisema Katibu Tawala huyo.
Alisema hata hivyo bila kutaka kuanzisha vurugu kama ambazo zilitokea wakati mradi huo unaanza, na katika hatua inayoonesha wananchi kuanza kubaini kuwepo kwa mbinu chafu za kuhujumu mradi huo muhimu kwa Serikali, vijana hao walifanya uamuzi wa kwenda ofisi hizo za Mkuu wa Mkoa.
“Tulichoamua kukifanya baada ya tukio hilo ni kuanza kutoa elimu mapema kwa kushirikiana na TPDC, kwa kuwaeleza wananchi kwamba taarifa hizo ni za uzushi na zina lengo la kuwagombanisha vijana wa Lindi na Mtwara.
“Unajua kadri muda unavyozidi kwenda mbele wananchi wanazidi kubaini kuwa mradi wa bomba la gesi si wa Serikali bali ni mradi wao. Ile sumu waliyokuwa wanajazwa wakati ule kwamba gesi inakwenda Bagamoyo wamegundua ilikuwa na nia ya kuzua vurugu na kuhujumu mradi.
“Kuna watu walidhani mradi huu ni ndoto lakini sasa wameamini kuwa mradi si ndoto upo na karibu utaanza kuzaa matunda. Wanajua ukianza maisha yao yatabadilika hawataishi kama wanavyoishi leo na sasa wanahaha,” alisema Chipota.
Mwenyekiti wa Bodi, Mwanda, alisema TPDC itashirikiana kwa karibu na serikali za mikoa na wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Gesi ya Taifa (Gasco) iliyo chini ya TPDC unawanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa.
0 comments:
Post a Comment