Na Mtanda Blog, Morogoro.
Kuna changamoto nyingi zinazozikabiri shule za msingi Manispaa ya Morogoro lakini kwa shule ya msingi Ujirani Mwema iliyopo kata ya Mkundi inaweza kushika nambari wani kutokana na adha mbalimbali wanazopata wafunanzi wakati wa masomo yao ya kila ikiwemo na walimu wao.
Utapofika shule ya msingi ya Ujirani Mwema na kuwaona wanafunzi wapo darasani ama wapo katika mapumziko huwezi kubaini lolote linaloendelea kutokana na changamoto kedekede zinazowakabili zaidi ya hapo utakaribishwa kwa upendo wa hali ya juu kama mgeni wao lakini utapo dadisi jambo utaelezwa lundo la changamoto inayoikabiri shule yao.
Ni jambo la kushangaza, pengine kwa mtu atakapo kueleza kuwa chumba kimoja cha darasa la shule ya msingi Ujirani Mwema, wafunanzi wa darasa la saba na sita hukitumia kwa pamoja katika masomo yao ya kila siku.
Si jambo la kushangaza kuona hali hiyo ambayo sasa hivi imezoeleka kwa wanafunzi wa madarasa mawili kukaa darasa moja ambapo mwalimu anapoigia darasani na kufundisha somo linalohusu darasa la sita dasarani hapo, wanafunzi wa darasa la saba wao hutakiwa kukaa kimpya na kugeuka kuwa watazamaji na wasikilizaji tu hadi mwisho wa somo.
Kadhali inapofikia zamu ya somo kwa darasa la saba, wanafunzi wa darasa la sita nao hukaa kimpya, huo ndiyo mfumo wa uendeshaji wa elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Ujirani Mwema iliyopo kilometa 40 kutoka Manispaa ya Morogoro.
Ukweli wa adha hiyo utaweza kubaini na kuamini pale utapoelezwa baada yakutembelea na kuona jengo moja la shule hiyo yenye vyumba vitatu vya madarasa huku wengine wakilazimika kufundishwa masomo yao katika kanisa lililopo jirani na shule hiyo.
Mwandishi wa makala haya alifunga safari hadi shule ya msingi Ujirani Mwema iliyopo kata ya Mkundi Manispaa ya Morogoro ikiwa sehemu ya kuibua changamoto za elimu za shule za msingi zilizopo pembezoni mwa miji ili wahusika waweza kuzitafutia ufumbuzi ili angalau wanafunzi hao kupata elimu inayolingana na shule zilizopo katikati ya miji.
Shule ya msingi Ujirani Mwema ina walimu watano, watatu kati yao ni walimu wa kuajiliwa na wawili wa kujitolea.
Mmoja wa walimu katika shule hiyo ambaye hakutaka jina lake lichapishwe gazetini kutokana na yeye kuwa si msemaji alimweleza mwandishi wa makala haya aliyefunga safari na kwenda kwenye shule hiyo.
Alianza kwa kueleza kuwa shule ya Ujirani Mwema inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchache wa walimu, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu ambazo vimekuwa vikwazo katika maendeleo ya taaluma.
“Shule inakabiliwa na changamoto nyingi sana, shule haina nyumba za walimu, walimu wachache na vyumba vya madarasa vipo vitatu tu na chumba kimoja hutumiwa kwa wanafunzi wa madarasa mawili kukaa chumba kimoja lakini hata vyoo navyo vipo lakini milango hakuna.”alisema Mwalimu huyo.
Mwalimu mmoja hulazimika kuwa na vipindi 28 hadi 42 ndani ya wiki na ili kuwe na uwiano pangekuwa na walimu angalau 10 au 12 kwani hali hiyo ya mwalimu mmoja angeondokana na lundo la vipindi na kujikuta mwalimu akitoka shuleni kukabiliwa na uchofu wa hali ya juu.
Kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa imelazimika wanafunzi wa darasa la nne na tano kusomea chumba kimoja ikiwemo na wale wa darasa la sita na saba nao wakiwa kwenye mfumo huo.alieleza.
“Hali halisi ndivyo ilivyo katika shule hii ndugu mwandishi na katika kila chumba kimoja, wanafunzi wa darasa la nne na tano hukaa pamoja na kinachofanyika, mwalimu anapoingia kwa ajili ya kufundisha somo la Kiswahili, wanafunzi wa darasa la nne, wanafunzi wa darasa la tano watasikiliza na kukaa kimya kadhalika, la sita na saba na huo hufanya hivyo hivyo ndiyo mfumo wake ulivyo kwa sasa.”alisema Mwalimu huyu.
Aliongeza kwa kusema kuwa kwa upande wa wanafunzi wa darasa la kwanza na pili wao husomea masomo yao ndani ya kanisa lililopo eneo hilo kutokana na hali hiyo ya uhaba wa vyumba vya madarasa wakati wanafunzi wa darasa la tatu ndiyo wametengewa chumba chao na hiyo ikiwa maalumu kwa ajili ya maandalizi ya mtihani wa darasa la nne.
Shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 150 na ilianzishwa mwaka 2004 na wazazi kama shule ya awali na mwaka 2005 ilipata usajili 28/12/2011 rasmi kuwa shule msingi Ujirani Mwema.
Mitaa ya Kipera, Ngerengere na Kiegea B katika kata ya Mkundi ilidhia kuwepo kwa shule hiyo na kupewa jina la Ujirani Mwema kutokana na uwepo wa mitaa hiyo.
Mwaka 2011, wanafunzi wa darasa la nne na saba walilazimika kufanya mitihani ya taifa katika shule ya msingi Sanga Sanga
Wanafunzi wanne mwaka 2011 walifaulu wote mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu ya msingi na kwenda sekondari huku mwaka 2012 wanafunzi watano wote walifaulu mtihani wa taifa wa kuhitimu elimu hiyo ya msingi na kwenda sekondari.
Kadhalika mwaka 2013 wanafunzi 14, watano kati yao walifaulu mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na kwenda sekondari na kufanya jumla ya wanafunzi 14 kujiunga na elimu ya sekondari.
“Baadhi ya wanafunzi waliofaulu na kujiunga na elimu ya sekondari, walichaguliwa kwenda katika shule ya sekondari ya wasichaana ya Mgugu Kilosa akiwemo Monica Hamis, Theresia Kikando na wengine.”alisema Mwalimu huyo.
Alisema kuwa changamoto ama adha wanayopata walimu ni kutumia kiasi cha sh10,000 kwa siku ikiwa sehemu ya fedha za usafiri pengine na chakula kutokana na jiografia ya shule ilipo.
“Mazingira ya kazi katika shule hii ni magumu na kama hauna wito huwezi kufanya kazi kwani piga hesabu kila siku itakulazimu utumie sh10,000 na siku ukipata lifti basi ni kumshukuru mwenyezi mungu, hapa hakuna mgahawa kama ulikunywa chai saa nyumbani itakulazimu chakula cha mchana ukipate saa 10 jioni baada ya kutokashule.”alifafanua baadhi ya kero ama changamoto.
Vitendea kazi ni tatizo vikiwemo vya vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi.
Walimu kwa sasa hivi wamelazimika kukaa kwenye nyumba ya mchungaji katika kanisa hilo na kugeuza kama ofisi ya walimu huku vyoo vikiwa na matundu machache.
“Hapa shuleni kutokana na matundu ya choo kuwa machache na walimu kukocha kabisa tundu maalum kwa ajili ya kutumia walimu kwa haja ndogo ama kubwa tunalazimika kuweka ulinzi wa kukulinda iwe kwa mwalimu mwenzio au kumtoa mwanafunzi darasani ili kusimama mita 10 kuepusha wanafunzi kuingia chooni kwani hakuna milango ya kufunga choo.”alieleza mtoa habari huyo.
Kama mabosi wetu watakapofikiria kupeleka walimu wasisahau kupeleka walimu wa kike ili wawe msaada kwa wasichana ambao baadhi yao tayari wanapevuka kwani imekuwa wakati mungine kwa kuona tu unahisi kuna jambo linalohitaji msichan asaidiwe na mwalimu wa kike.aliongeza
“Kungepatikana mfadhili wa kutuwezesha usafi kama pikipiki ingesaidi kupunguza ghalama za kulipia matumizi ya siku ya sh10,000, kuwepo nyumba za walimu na kuwepo majengo mengine kwa ajili ya vyumba vya madarasa ili wanafunzi waweze kukaa kama mfumo unavyotakiwa.”alisema.
Kaka mkuu wa shule ya msingi Ujirani Mwema.Athanas John (14) ni mwanafunzi wa darasa la saba na kaka mkuu yeye anasema kuwa mazingira ya shule yao ni magumu sio kwa wanafunzi bali hata walimu pia.
“Shule yetu haina bendera ya taifa, kuna uhaba wa maji na kama wafadhili wangetujengea matenki ya maji ingesaidia kuvuna maji ya mvua na kupunguza uhaba wa maji kwa kutumia wanafunzi wawapo shuleni.”alisema John.
John alisema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya kutopatikana kwa majisafi na salama, wanafunzi wanashindwa kuonyesha vipaji vyao kutokana na kukosekana kwa uwanja wa michezo mbalimbali tofauti na shule nyingine zilizopo ndani ya Manispaa yaMorogoro.
AFISA ELIMU MANISPAA YA MOROGORO.
Afisa Elimu Manispaa ya Morogoro, Bakari Sagini, anaeleza juu ya changamoto zinazozikabili baadhi ya shule za msingi katika Manispaa hiyo ikiwemo shule ya msingi Ujirani Mwema iliyopo kata ya Mkundi.
Sagini anaeleza kuwa baadhi ya shule za msingi Manispaa ya Morogoro inakabiliwa na upungufu wa madawati 7428 na vyumba vya madarasa 474 takwimu hizo ni za mwaka 2014.
“Ni kweli shule ya msingi Ujirani Mwema ina changamoto nyingi lakini sio shule hiyo pekee yenye changamoto hizo bali hata shule nyingine za Manispaa ya Morogoro kwani mpaka sasa tuna upungufu wa madawati 7428 na vyumba vya madarasa 474.”alisema Sagini.
Shule ya msingi Mkundi katika kata hiyo ina changamoto ya uchakafu wa vyumba vya madarasa huku shule ya msingi Azimio ikiwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kuwa vichache na kuelemewa na uwingi wa wanafunzi wanaohamia baadaya wazazi wao kuhamia katika makazi mapya ya kata ya Kihonda.alisema Sagini.
Alieleza kuwa baada ya shule hiyo ya Azimio kuelemewa na wanafunzi kuwa wengi, mwalimu mkuu wa shule hiyo alifanya kazi ya kuhamasisha wazazi kutumia nguvukazi na kujenga maboma ya vyumba vya madarasa ambavyo vitasaidia kupunguza tatizo la kulundikana katika vyumba vya madarasa.
Akitoa ufafanuzi juu ya shule ya msingi Ujirani Mwema, Sagini alieleza kuwa shulehiyo ilianzishwa na wazazi wa jamii ya wafugaji kama shule ya awali lakini siku kadili ilivyoendesha shule hiyo ilisajiliwa na kuwa shule kamili kwa kupata usajili.
Shule hiyo ilipata usajili rasmi mwaka 2011 na Manispaa na mwanzoni mwa mwaka 2012 ilipeleka walimu wanne na benki ya KCB ilifadhili kwa kutoa madawati 80.
“Wakati natoa fedha za motisha ya mazingira magumu na kujikimu kwa walimu wale wanne niliwashauri wanaweza kutumia fedha hizo kununua vyombo vya usafiri kama pikipiki ili iwe rahisi kutumia katika usafiri wa kwenda na kurudi na pengine ingewasaidia kufanyia biashara.”alisema Sigina.
Baada ya Manispaa kutambua changamoto zinazoikabili shule ya msingi UjiraniMwema iliweka mikakati ya kutenga fedha kila mwaka za kuwawezesha wanafunzi wanapata chakula wakati wakiwa shuleni.
“Baada ya Manispaa kuichukua Ujirani Mwema ilianza kuihudumia kama shulenyingine ikiwemo kuitengea fedha za chakula kwa shule zenye mazingira magumu ili wanafunzi wapate chakula.”alisema Sigina.
Mwaka wa fedha 2013/2014 Manispaa iliitengea fedha kiasi cha sh25 milioni ambazo sh10 milioni zimetumika kujenga nyumba ya walimu ambayo itakuwa na uwezo wa kukaa familia nne baada ya kukamilika kwake.
Wakati mwaka 2014/2015 kuna fedha nyingine zimetengwa bajeti kwa ajili yakumalizia ujenzi huo na ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Sigina alisema kuwa changamoto zinazozikabili baadhi ya shule za msingi hasa za upungufu wa vyumba vya madarasa ama madawati tatizo hilo lingeweza kumalizwa kwa wazazi ama kupunguza baadhi za changamoto kwa kuchangia nguvukazi kama ujenzi wa vyumba vya madarasa.
“Kuna tatizo kwa upande wa viongozi wa serikali za kata na wale wa siasa katika ngazi hiyo kwani kama kungekuwa na hamasa ya kuwahamasisha wananchi na kujitolea baadhi za changamoto zinazozikabili shule zetu zingepungua.”alisema Afisa Elimu huyo.
Diwani wa kata Mkundi Manispaa ya Morogoro kupitia tiketi ya chama cha mapinduzi (CCM), alipotafutwa na mwandishi wa makala haya ili kutaka ni juhudi gani zimefanywa yeye kama diwani zikiwemo za kuhamasisha wananchi kujitolea katika nguvu kazi ikiwemo ujenzi wa maboma ya vyumba vya madarasa na n:k.
Alieleza kwa kujibu kuwa pakuwa shule ya msingi Ujirani Mwema ni shule ya serikali yeye hawezi kuzungumzia lolote bila idhini ya mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaaya Morogoro, Jorvis Simbeye ambaye anapaswa kuzungumzia changamoto za shulehiyo au kama angepata kibali cha kuzungumza angezungumza.
"Siwezi kuzungumzia changamoto zozote kwa sababu hii shule hii ya Ujirani Mwemakwani mimi sio msemaji na hii shule ni shule ya serikali vinginevyo mpaka nipate kibali cha kuzungumzia changamoto nakushauri uende Manispaa ukamuulizi Mkurugenzi (Jorvis Simbeye) hizo changamoto."alisema Diwani huyo.
chanzo/Mtanda Blog, Morogoro.
0 comments:
Post a Comment