BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MWANASHERIA MKUU WA ZANZIBAR AONDOKA KATIKA UKUMBI WA BUNGE CHINI YA ULINZI MKALI WA ASKARI, NI BAADA YA KUPIGA KURA YA KUIKATAA KATIBA MPYA DODOMA.


MWANASHERIA Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amejikuta akipata wakati mgumu bungeni ambapo askari wa Bunge walilazimika kumlinda na kumficha katika baadhi ya vyumba vilivyopo ndani ya ukumbi.

Othman hivi karibuni aliripotiwa kujitoa miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba, kutokana na kilichodaiwa kuwa alikuwa na hoja saba alizowasilisha katika Kamati hiyo, zikakataliwa.

Baada ya kujitoa, Othman hakutokea kupiga kura ya kupitisha au kukataa Katiba Inayopendekezwa, kulikoanza Jumatatu wiki hii, wala juzi na badala yake akajitokeza jana na kupewa nafasi ya kupiga kura yake na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta.

Othman alipiga kura ya wazi na kukataa sehemu kubwa ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, hatua iliyowaamsha kwenye viti wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kuhoji kama ana msaada wowote kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

Mjumbe Yahaya Kassim Issa alisema Mwanasheria huyo ni msomi na alitarajiwa kuwa msaada katika kusaidia Zanzibar katika mjadala wa kupata Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa. Issa alihoji mtu huyo aliyepaswa kuwa msaada kwa SMZ na muda wote hakuwepo, alikuwa anawakejeli?

“Tulitarajia awepo atoe hoja zake lakini hakuwepo, sasa huyu ana maslahi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar?”

“Huyu ni Mwakilishi na msaidizi wa Rais, tulitarajia atusaidie lakini akatoroka, Mwenyekiti unaweza kueleza nini kwa mtu kama huyu?” alihoji huku baadhi ya wajumbe wakiimba kuwa Kamanda Kakimbia Vita.

Sitta Kuona hivyo, Sitta alijaribu kuokoa jahazi na kusema kura haipigwi kwa vyeo bali kila mtu kwa dhamiri yake hivyo Othman asihukumiwe kwa cheo chake. “Hatutaki kujadili kura ya mtu,” alisisitiza Sitta.

Hata hivyo, wajumbe wa Zanzibar waliendelea kuimba Kamanda kakimbia vita! Kutokana na hali ilivyokuwa, Sitta aliamua kuahirisha shughuli za Bunge mpaka leo asubuhi, lakini alipokuwa akiondoka alipokaribia mlangoni, wajumbe wa Zanzibar waliendelea kuimba.

“Hatumtaki hatufai” huku wakigonga meza za Bunge Maalumu. Askari waingilia kati Wakati baadhi ya wajumbe wakiimba kuwa Othman hatakiwi, hawafai, Mwanasheria huyo alikuwa amesimama katika kiti chake bila kufahamu atokee mlango upi, kwa kuwa mlango uliokuwa kiti cha nyuma yake, kulikuwa na wajumbe waliokuwa wakimuimba vibaya.

Othman aliamua kutoka kupitia mlango mkuu wa Spika, ambao kwa kawaida pembeni yake kuna askari wa Bunge, lakini kabla hajaenda askari wa Bunge karibu watano, walimzunguka na kumtaka aelekee katika mlango wanaotumia viongozi wakuu, akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kuingilia.

Afichwa, alindwa Baada ya hapo waandishi wa habari na baadhi ya wajumbe, walikuwa wakimsubiri Othman nje ya ukumbi wa Bunge, ambapo walishangaa kuona baadhi ya askari waliomsindikiza Mwanasheria huyo kutoka nje ya ukumbi, wakitoka wenyewe bila Mwanasheria huyo.

Baada ya zaidi ya nusu saa, askari wanne wa Jeshi la Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliingia katika viwanja vya Bunge na kwenda katika eneo la maegesho ya magari ya viongozi wakuu, yaliyo karibu na mlango huo wa kuingilia wa viongozi hao.

Zilipita dakika kama kumi, ndipo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif, alitokea katika mlango huo na kufuatiwa na Othman akiwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, askari kadhaa wa Bunge na walinzi wengine waliovalia kiraia.

Muda mfupi baadaye gari la Kificho, lilisogezwa karibu na alipokuwa Mwanasheria huyo ambaye aliingia katika gari hilo na Kificho aliyepanda mbele na kuondoka katika eneo la Bunge. Ibara alizokataa Othman alikataa ibara ya pili ya Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa inayosema.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, inayofuata mfumo wa vyama vingi vya siasa, utawala wa sheria, inayoheshimu misingi ya haki za binadamu, isiyofungamana na dini yoyote na inayojitegemea”. Pia alipinga Ibara ya tisa, ambayo katika Ibara ndogo ya kwanza inasema

“Katiba hii ni Sheria Kuu ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa na Katiba hii. Ibara hiyo ina ibara ndogo tano. Mwanasheria huyo pia amekataa Sura yote ya saba, ambayo inahusu Muundo wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo ibara ya kwanza ya sura hiyo ni Ibara ya 70, inayosema;

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakuwa na muundo wa serikali mbili.” Ibara ya 128, pia imekataliwa na Mwanasheria huyo, ambayo ibara ndogo ya kwanza inasema;

“ Mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yahusuyo Tanzania Bara, yatakuwa mikononi ya Bunge. Ibara ndogo ya tatu katika Ibara hiyo yenye ibara ndogo tano, sehemu yake inasema:

“Endapo sheria yoyote iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi inahusu jambo lolote katika Zanzibar ambalo liko chini ya mamlaka ya Bunge, shera hiyo itakuwa batili na itatanguka…”

Mwanasheria huyo pia alikataa sura yote ya 11, ambayo inahusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Sura yote ya 16 pia imekataliwa na Mwanasheria huyo, ambayo inahusu Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano, ambayo sehemu (a), inahusu Mfuko Mkuu wa Hazina na Fedha za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sehemu ya mwisho ambayo Mwanasheria huyo ameikataa, ni nyongeza ya kwanza ya Katiba, inayohusu mambo 16 ya Muungano.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: