BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS JAKAYA KIKWETE AFUNGUA MILANGO YA URASI 2015.


Rais Jakaya Kikwete akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge 2014, Rachel Kassandra kwenye sherehe za Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge huo na Kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere zilizofanyika katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora jana. Picha na Freddy Maro wa Ikulu


Tabora/Dar.
Wakati mbio za kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 zikianza kushika kasi nchini, Rais Jakaya Kikwete amewataka vijana kumchagua mtu anayefanana na kijana kurithi nafasi yake.


Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja huku kukiwa na makada kadhaa ndani ya chama chake ambao wametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo huku baadhi wakifungiwa kwa kuanza kampeni mapema na wengine wakiendelea na mikakati ya chinichini kabla ya kujitangaza.


Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Tabora alipokuwa akihutubia wananchi waliohudhuria kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere zilizokwenda sambamba na kilele cha Wiki ya Vijana na hitimisho la Mbio za Mwenge wa Uhuru.


Alisema vijana ndiyo chachu ya maendeleo ya Taifa lolote hivyo washiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura kumchagua rais anayefanana na kijana kama alivyokuwa yeye wakati akigombea urais 2005, wakati huo akiwa na umri wa miaka 55.


“Siyo kijana wa chini ya miaka 35, Katiba yetu hairuhusu, lakini mtu ambaye anaonekana kijana kama nilivyokuwa mimi wakati nagombea nafasi hiyo mwaka 2005,” alisema Rais Kikwete huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria uwanjani hapo.


Mgombea mwenye sifa zilizotajwa na Rais Kikwete anaweza kutoka nje au katika kundi la wanaCCM wanaotajwa au kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu.


Miongoni mwa wanaotajwa wamo makada sita waliopewa onyo kali na chama hicho kwa kuanza kampeni mapema wakiwamo mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa (61) na Frederick Sumaye (64) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (61).


Wamo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira (69), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (40) na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (47).


Mbali na hao waliopewa onyo, wanaCCM wengine wanaotajwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (66), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (72), Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla (39), Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (39) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya (65).


Pia wamo Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi (43), Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (66) na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal (69).


Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni kama ile iliyowahi kutolewa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa mwaka 2005, kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ambapo aliweka bayana kwamba wakati huo ulikuwa ni wa vijana kuongoza nchi kwa kuwa tafiti ndivyo zilivyokuwa zikionyesha.


Baada ya Rais Mkapa kutoa kauli hiyo, wakati huo Kikwete ndiye aliyepitishwa na CCM kugombea urais kwa kuwashinda wenzake 11 waliojitokeza ndani ya chama hicho kuwania uteuzi huo.


Rais Mkapa alisema pamoja na kuwa mgombea wa CCM anapaswa kuwa na sifa 13 zilizoainishwa na NEC, yafaa pia kuwa na sifa za ziada ambazo ni kuwa na mtu anayechagulika pande zote za Muungano, anayekubalika katika kundi la vijana, ana historia iliyotukuka ndani ya chama na si mtu aliyechipuka tu, anayeijua zaidi CCM, Muungano na Mapinduzi na kwamba Tanzania chini yake itakuwa salama.


Pia awe ni mtu asiye na visasi, chuki, hasira na anayepima mambo kabla ya kufanya uamuzi.
Akizungumzia umuhimu wa vijana jana, Rais Kikwete alibainisha kuwa umetambuliwa katika Katiba Inayopendekezwa kwa kuundwa kwa Baraza la Vijana litakalowaunganisha vijana wote nchini bila kujali tofauti zao.


Alizitaka wizara zinazohusika kuhakikisha mifuko ya maendeleo ya vijana pamoja na wanawake inakuwa na fedha za kutosha na kuhakikisha zinawafikia walengwa.


“Pia naziagiza halmashauri zote nchini kuanza kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila baada ya miezi minne kuanzia Desemba mwaka huu,” alisema na kuongeza kuwa iwe mara ya mwisho kwa halmashauri kufanya vibaya.



Kuhusu Nyerere
Rais Kikwete alimtaja Mwalimu Nyerere kuwa kiongozi ambaye hana mfano nchini akieleza kuwa aliona umuhimu wa kuwa na Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, ndiyo maana Katiba Inayopendekezwa inatambua Muungano wa serikali mbili.


Alielezea nadhiri aliyoiweka Mwalimu Nyerere juu ya Mwenge wa Uhuru kwa kunukuu maneno yake, “Sisi watu wa Tanzania tutaweka mwenge wa uhuru katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ili uangaze palipo na giza, ulete tumaini palipo na chuki na ulete umoja palipo na utengano.”


Alimwelezea kiongozi huyo kama alama ya ukombozi wa Bara la Afrika kwa kuwa alisaidia nchi nyingi kupata uhuru, zikiwamo Namibia, Afrika Kusini na Msumbiji.


“Rais wa sasa wa Namibia (Hifikepunye Pohamba) alikuja kuishi uhamishoni hapa Tanzania mara tu tulipopata uhuru. Alikuwa anaishi kule Temeke, anaongea Kiswahili vizuri kama vijana wa siku hizi.”


Apigia debe Katiba Inayopendekezwa
Rais Kikwete alisisitiza kuwa Katiba Inayopendekezwa ambayo imepitishwa na Bunge la Katiba hivi karibuni ni bora kuliko inayotumika sasa kwa sababu imetoa majawabu kwa changamoto mbalimbali za kitaifa.


“Sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zingeingia dosari kama Bunge Maalumu la Katiba lingependekeza muundo wa serikali tatu,” alisema Rais Kikwete.


Alisema Katiba hiyo imetambua haki za makundi mbalimbali ya kijamii wakiwamo vijana, wanawake, watoto, wakulima, wavuvi na wasanii. Hata hivyo, alisema Katiba hiyo ni matokeo ya ushirikishwaji wa wananchi ndani na nje ya Bunge la Katiba.


“Ndugu zangu mjitokeze kupiga kura ya ‘ndiyo’ kwa sababu Katiba hii ni bora, ni zaidi ya nzuri. Msikubali kutumiwa na wanasiasa na wanaharakati kwa mambo ambayo hayana tija kwenu,” alisema.


Vita dhidi ya dawa za kulevya


Rais Kikwete alikiri kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya ni ngumu lakini Serikali imekuwa ikijitahidi kupambana na watu wanaosafirisha dawa hizo ambazo zinawaharibu vijana wengi nchini.


Alisema vita inakuwa ngumu kwa sababu watu wanabuni mbinu mbalimbali za kusafirisha dawa hizo.


“Watu wanasafirisha dawa za kulevya kwenye malori ya mafuta, wengine wanaficha katika sehemu ambazo hazistahili hata kutajwa. Pamoja na mbinu zote hizo tumekuwa tukiwabaini,” alisema na kuongeza kuwa watu 6,875 wamekamatwa na dawa hizo katika kuanzia Januari – Oktoba mwaka huu.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: