BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TANZANIA YAWEKA HISTORIA, RAIS KIKWETE, DK SHEIN WAKABIDHIWA RASIMU YA KATIBA, MZIGO SASA KWA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Mohamed Ali Shein wakiwa wameinua juu Katiba inayopendekezwa katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa michezo wa Jamhuri mjini Dodoma Oktoba 08, 2014 Kulia ni
Mwenyekiti wa Bunge maalum la Katiba Mhe.Samuel Sitta akifuatiwa na Makamu wake Mhe samia Suluhu Hassan.



WAKATI kukiwa na matamanio na ushauri wa kutaka Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha Katiba Mpya inapatikana kabla ya kuondoka madarakani, suala hilo limeachwa kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupatiwa ufumbuzi.

Rais Jakaya Kikwete alisema kwa kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 inatamka kwamba baada ya Katiba Inayopendekezwa kukabidhiwa, kura ya maoni inatakiwa ifanyike ndani ya siku 84, lakini muda uliobaki ni finyu na hautawezesha wala kutosha kukamilika kwa shughuli hii kutokana na Tume ya Uchaguzi kutokamilisha mchakato wa daftari la wapiga kura.

Hata hivyo alisema jambo hilo inabidi bunge lijalo lifanye mabadiliko ili kukidhi matakwa hayo ya kisheria.

Kikwete alisema hayo jana kwenye sherehe ambazo Katiba Inayopendekezwa ilikabidhiwa kwake pamoja na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein mjini Dodoma.

Rais ambaye kwenye sherehe hizo alieleza milima na mabonde aliyokumbana nayo katika kuanzisha mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya, alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka kuendesha kura ya maoni ndani ya siku hizo kutoka tarehe ya rais kupokea katiba inayopendekezwa.

Hata hivyo, alisema kulingana na maoni yaliyotokana na mazungumzo kati yake na viongozi wa vyama vinavyounda Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ilibainika muda uliobaki hautatosha kukamilika kwa shughuli hiyo.

Alisema kutokana na maoni hayo, ilikubalika kushughulikia mambo ya msingi ili kuwezesha uchaguzi kufanyika na hatimaye Kura ya Maoni ifanyike baadaye.

“Inabadi sheria hii ipelekwe bunge lijalo kuruhusu mabadiliko hayo. Maanake sasa ni siku 84. Nataka kusema Mwanasheria Mkuu wanaangalia nini kinaweza kufanyika…mchakato unaendelea,” alisema Kikwete.

Aliendelea kusema: “Lakini pia, wako watu wanasema tufanye sasa kura ifanyike tumalize (alishangiliwa) lakini tume inasema wao wanaandika daftari jipya na kazi inaisha Mei. Hapo ndipo penye mgogoro.”

Hata hivyo, alisema wapo ambao wamekuwa wakimwambia kwamba mbona mbunge akifariki, uchaguzi hunafanyika na hivyo kuhoji kwa nini daftari linalotumika kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo, lisitumike kwa kura ya maoni.

“Penye wengi pana mengi. Haya ndiyo yanaendelea kwenye tafakuri… ikifika mwisho wananchi watafahamishwa, “ alisema.

Miongoni mwa waliotamka bayana matamanio ya Kura ya Maoni kupigwa kabla ya Rais Kikwete kutoka madarakani, ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyetoa maoni hayo wakati wa kuhitimisha Bunge Maalumu la Katiba .

Kauli hiyo ya Pinda iliyoungwa mkono na watu wengine akiwamo mjumbe wa bunge hilo, Askofu Amos Mhagache aliyesisitiza jana kwenye sherehe hizo, ilizua mjadala huku baadhi ya watu wakiitafsiri kwamba ni uamuzi wa Serikali na hivyo kushutumu kuwa inapingan na makubaliano yaliyofikiwa kati ya rais na TCD.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: