MGOMBEA CCM, MPIGA KURA WAFARIKI DUNIA GHAFLA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2014.
Askari wakiwataka wananchi kutawanyika baada ya kuahirishwa uchaguzi wa Serikali za mitaa katika kituo cha Mabibo Mpakani Mtaa wa Jitegemee, Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao.
Mikoani. Mgombea uenyekiti kupitia CCM Mtaa wa Swea, Kata ya Mkolani, Nyamagana, Mwanza, Pius Mihayo amefariki dunia ghafla akiwa mtaani kwake, muda mfupi baada ya kupiga kura.
Msimamizi wa uchaguzi huo, Halifa Hida alisema mgombea huyo alifariki dunia ghafla akiwa kwenye mtaa wake wa Swea na chanzo cha kifo hicho hakijajulikana... “Sasa kwa mujibu wa taratibu za uchaguzi, tutatangaza matokeo ya wajumbe na nafasi za wagombea wa viti maalumu, nafasi ya uenyekiti haitatangazwa hadi taratibu nyingine za uchaguzi zitakapoandaliwa,” alisema Hida.
Mkoani Arusha msongamano wa kupiga kura, katika kituo cha Mbauda, Kata ya Sombetini unadaiwa kusababisha kifo cha mtu aliyetambulika kwa jina la Suleiman Bakari.
Tukio hilo lilitokea saa tatu asubuhi katika kituo hicho ambacho kilikuwa kimefurika watu. Mjomba wa marehemu, Ramadhani Athumani alisema kifo hicho kimewashtua kwani marehemu hakuwa mgonjwa.
“Marehemu alikuwa ni kinyozi na baada ya kupiga kura alianguka ghafla,” alisema Athumani na kuongeza kuwa mazishi yatafanyika leo saa saba.
Wagoma kupitishwa bila kupingwa
Vituko vya uchaguzi vimeendelea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambako pamoja na mambo mengine, baadhi ya wagombea wa CCM waliopita bila kupingwa wameamua kujitoa baada ya kutishiwa maisha.
Tukio la wagombea kutishiwa maisha lilitokea wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu ambako uchaguzi huo ulikumbwa na vurugu mbalimbali. Taarifa zilizotolewa na Mkuu wa wilaya hiyo, Paul Mzindakaya zinasema wagombea kupitia CCM katika Mji wa Lamadi, walijiondoa dakika za mwisho.
Hatua hiyo inadaiwa imetokana na wagombea hao kutishiwa maisha, kuchomewa moto nyumba zao na kwamba kutoka kwa wafuasi wa chama kimoja cha siasa.
Mzindakaya alisema wagombea wa Chadema Kijiji cha Lamadi walienguliwa kutokana na kutokidhi vigezo baada ya kuwekewa pingamizi, huku wakisalia wa CCM pekee.
“Mpaka sasa saa sita mchana, tumeamua kusitisha upigaji kura masanduku yote tumeyaondoa, hali si shwari eneo hilo, askari wamepelekwa kurejesha usalama na kamati ya ulinzi na usalama wilaya itakaa muda huu kujadili hali hii, ili tukubaliane kama tuendelee au tusitishe,” alisema Mzindakaya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Charles Mkubo alisema askari wamejiandaa kukabiliana na vurugu zozote ambazo zingejitokeza.
Mkoani Shinyanga katika Mtaa wa Mabambasi, Kata ya Ndembezi, kura 54 ambazo tayari zilikuwa zimepigwa kwa ajili ya kuwachagua wajumbe wa Serikali ya Mtaa zilichomwa moto kwa makubaliano ya pande husika, baada ya kubaini kuwapo kwa kasoro kadhaa.
Utata huo ulitokana na mgombea ujumbe wa CUF, Seleman Haji kudai kuwa jina la mgombea wa chama hicho limekatwa na kuingizwa la mgombea wa Chadema.
Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Shinyanga, Festo Kang’ombe alisema baada ya tatizo hilo waliamua kuendelea na upigaji kura wa mwenyekiti na wajumbe wa viti maalumu, huku wakisitisha uchaguzi wa wajumbe hadi utakapotolewa utaratibu mwingine.
Wakazi wa Kijiji cha Mwalukwa, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga walikuwa hawajaanza kupiga kura hadi saa 8.00 mchana kutokana na masanduku ya kupigia kuchelewa.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Annarose Nyamubi alisema tatizo la kuchelewa kupiga kura limetokana na jiografia ya wilaya hiyo.
Katika Kata ya Itlima, Wilaya ya Kishapu, Shinyanga uchaguzi umeahirisha hadi keshokutwa baada ya wapiga kura kuona masanduku hayana mifuniko na kukosekana kwa wino wa kuchovya kwenye vidole.
Karatasi zaibwa
Mkoani Kigoma, uchaguzi wa vijiji vitatu vya Wilaya ya Uvinza, ulisitishwa kutokana na karatasi za kupigia kura kuibwa, huku kukiwa na utata wa uraia wa baadhi ya waliopitishwa kugombea uenyekiti.
Msimamizi wa uchaguzi Wilaya ya Uvinza, Nicholaus Kombe alitaja vijiji hivyo kuwa ni Nyangabo, Karago na Kapalamsenga na kuongeza kuwa sababu za kusitisha uchaguzi zilitokana na karatasi za kura kuibwa baadaye kukutwa kwa mtu asiyehusika.
Kombe alisema baadhi ya wagombea wamekutwa na dosari za uraia hivyo kusababisha uchaguzi kusitishwa hadi hapo atakapotoa taarifa nyingine.
Katika tukio jingine, lililotokea mkoani Mwanza katika Kata ya Mandu, kituo cha Shule ya Msingi Nation, baadhi ya wapiga kura walibaini kuwapo kwa utata wa fomu za wajumbe wa CCM na Chadema.
Fomu hizo ambazo zinatakiwa kuwa na wajumbe sita, zilikutwa zikiwa na majina ya wajumbe wanne jambo lililoibua hasira kwa wapiga kura na kutaka kurudiwa kwa upigaji wa kura.
Katika baadhi ya vituo vya Mkoa wa Dar es Salaam kulikuwa na matatizo ya wino na kusababisha upigaji kura kuchelewa kwa saa mbili. Kasoro hizo zilibainika katika Mtaa wa Kingugi A, Kata ya Kiburugwa, Temeke.
Imeandikwa na Antony Kayanda, Mussa Juma, Faustine Fabian, Simiyu, Suzy Butondo, Tausi Ally na Raymond Kaminyonge.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment