MGOMBEA WA CHADEMA AMSHAMBULIA MKEWE KWA NONDO KISA AMEZUILIWA KUUZA CHAKULA CHA FAMILIA KUENDESHA KAMPENI ZA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA SHINYANGA.
MWANAMUME mmoja mkazi wa hapa, amemshambulia mkewe kwa nondo kichwani, kutokana na tofauti za itikadi ya vyama vya siasa.
Inadaiwa alifanya hivyo baada ya kuzuiwa kuuza chakula cha familia ili kuendesha kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Upigaji kura kuchagua wenyeviti wa mitaa na vitongoji utafanyika Jumapili Desemba 14, mwaka huu.
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari limefungua jalada lenye namba SHY/ RB/8025/2014, huku likimsaka mtuhumiwa ili aweze kukamatwa na kufikishwa mahakamani kujibu shitaka la kujeruhi.
Mtafaruku huo umetokea katika Mtaa wa Mwasele “A” Manispaa ya Shinyanga, wanakoishi watu hao, ambapo mume amefahamika kwa jina la Edward Bundala, mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anayegombea uenyekiti wa mtaa. Baada ya kutenda kosa hilo, Bundala alitoroka.
Mkewe ametambulika kuwa ni Theresia Dotto (35) na kwamba ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Theresia alijeruhiwa kwa nondo sehemu za kichwani.
Imedaiwa kuwa chanzo cha mtafaruku huo, kati ya wanandoa hao, ni Bundala anayegombea uenyekiti wa mtaa mpya wa Mihogoni Kata ya Kambarage, Manispaa ya Shinyanga kwa tiketi ya Chadema, kuzuiwa kuuza chakula cha familia ili aweze kupata fedha za kuendeshea kampeni.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kupatiwa matibabu jana asubuhi, Theresia alidai vurugu zilitokea ndani ya familia yao baada ya kumzuia mumewe asichukue gunia moja la mpunga kwa ajili ya kuliuza ili apate fedha za kupigia kampeni.
Alidai mara baada ya kumkataza, mumewe alichukia na kuamua kumshambulia kwa kipigo, akihoji kwa nini anamzuia asichukue mpunga huo. Alidai mpunga huo ulikuwa umehifadhiwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na mbegu za kupanda.
Alidai awali mumewe huyo aliwahi kuchukua debe mbili za mpunga na kuziuza bila ya kumfahamisha, ambapo fedha aliyoipata alikwenda kuwalipa mawakala wa Chadema, waliokuwa wakisimamia uandikishaji wa wapigakura.
Alidai kitendo hicho kilimsikitisha, ambapo alimuonya aache kuuza chakula cha familia. “Mara ya kwanza mimi alinificha, alikwenda tunakotunzia mpunga wetu akachukua debe mbili ambazo aliziuza na fedha iliyopatikana aliwalipa mawakala wa chama chake waliokuwa wakisimamia uandikishaji wa wapiga kura, kwa kweli niligombana naye sana.
”Nilifikisha suala hili kwa Mwenyekiti wa Mtaa, tukalizungumza na akaonywa aache kuuza chakula cha ndani kwa masuala ya kisiasa, na kwamba kama anataka atafute fedha kwa njia nyingine, alionesha kukubaliana na ushauri huo, sasa nashangaa jana (juzi) alitaka kuchukua gunia moja aende akauze, nikamzuia ndipo akanishambulia kwa kipigo,” alieleza.
Alidai wakati akimshambulia kwa kipigo jana alfajiri, alijaribu kujiokoa kwa kukimbia, lakini hata hivyo mumewe alichukua kipande cha nondo na kumpiga nacho sehemu za kisogoni, kilichomjeruhi na kusababisha kutokwa na damu nyingi.
Kamanda wa Sungusungu eneo la Mwasele “A”, James Mtuli aliyekuwa ameongozana na majeruhi huyo katika Kituo cha Polisi na kisha kumpeleka hospitali kupatiwa matibabu, alithibisha kutokea kwa tukio hilo na kulaani kitendo hicho.
“Huyu bwana ametushangaza sana, haiwezekani mtu ushinikize kuuza chakula cha ndani kwa ajili ya kupata fedha za kufanyia kampeni, leo anakatazwa anamshambulia kwa kipigo mkewe, tumeshatoa taarifa Polisi na hivi sasa anatafutwa ili aweze kufunguliwa mashitaka ya kujeruhi,” alisema Mtuli.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment