PROFESA MUHONGO NI MCHAPAKAZI ANAYEGEUZWA ‘BANGUSILO’.
Waziri akitembelea makao makuu ya BG Group.
BG group ni moja ya kampuni kubwa duniani inayoongoza uchimbaji, utunzaji, usambazaji wa gesi asilia.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996 BG Group imejiimarisha zaidi kwa kujijengea uzoefu mkubwa na historia nzuri katika sekta hii nyeti ya nishati.
Pamoja na kuwa makao yake makuu yakiwa mjini Reading, Uingereza vilevile kampuni hii imeshafanya kazi nchi ishirini duniani ndani ya mabara matano tofauti ikiwa na wafanyakazi zaidi ya elfu sita kutoka mataifa mbalimbali.
Makala iliyoandakwa na Rachel Penza.
KAMA kuna jambo ambalo litaendelea kuzungumzwa au kubeba uzito katika vyombo mbalimbali vya habari basi ni lile linalohusu akaunti ya Tegeta Escrow.
Sakata hili ambalo lilianza taratibu miezi kadhaa iliyopita, limekuwa maarufu na kuteka hisia za wananchi walio wengi wakati wa mkutano wa Bunge uliomalizika Novemba 29, mkoani Dodoma.
Kuna mambo mengi yaliyosababisha mjadala uliohusu sakata hilo kufuatiliwa na wananchi wengi, baadhi yake ni kuwasilishwa bungeni kwa Ripoti ya Kamati ya Bunge ya hesabu za Serikali (PAC), chini ya Mwenyekiti wake Zitto Kabwe.
Kuwasilishwa kwa ripoti hiyo kulizua taharuki kwa watu wengi ambao baadhi yao waliamini kwamba historia ya mwaka 2008 ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi na mtangulizi wake Dk.Ibrahim Msabaha walijiuzulu baada ya Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe Mbunge wa Kyela ambaye kwa sasa ni Waziri wa Uchukuzi kuwasilisha Ripoti kuhusu zabuni tata ya ufuaji umeme baina ya Tanesco na Richmond.
Kamati hiyo katika ripoti yake ilitoa mapendekezo kadhaa yakiwemo yaliyowataka viongozi wa kisiasa wajiuzulu huku aliyekuwa Waziri Mkuu akitakiwa kujipima.
Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Kamati hiyo kwa namna moja ama nyingine kuwaona viongozi hao walihusika kwa kushindwa kuwasimamia watendaji walio chini yao.
Mazingira ya sakata la Richmond yanashabihiana kwa kiasi fulani na sakata linaloendelea kupamba vyombo mbalimbali vya habari linalohusu Akaunti ya Tegeta Escrow.
Yanashabihiana kwa kuwa, yote yanahusu masuala ya mikataba na utekelezaji wa mikataba husika ingawa kwa mazingira tofauti, lakini yote chanzo chake ni tatizo la nishati ya umeme.
Pamoja na hayo matukio yote yanashabihiana katika mapendekezo kwa sehemu fulani hasa la kuwataka viongozi wa kisiasa wajiuzulu.
Kwa maana nyingine kiu kubwa ya wabunge waliochangia hoja itokanayo na ripoti ya PAC kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow, ni kuona viongozi wa kisiasa wanajiuzulu hasa Waziri wa Nishati Profesa Sospeter Muhongo.
Hata mapendekezo ya Kamati ya maridhiano kwa serikali yametaka Waziri huyo awajibishwe kwa kushindwa kuwasimamia watendaji au kwa yeye mwenyewe kuhusika.
Hata hivyo Ripoti ya PAC pamoja na maelezo yake yote hakuna mahali ambapo imeeleza Waziri Muhongo amehongwa fedha katika mchakato wa kutoa fedha katika akaunti hiyo.
Wakati akitangaza kujiuzulu katika kikao cha Bunge mwaka 2008, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye wakati anajiuzulu alikuwa Waziri wa ushirikiano Afrika Mashariki Dk. Ibrahim Msabaha katika maelezo yake mafupi akitoa taarifa ya kujiuzulu alisema yeye amekuwa ‘Bangusilo’.
Bangusilo ni neno la kabila la kizaramo ambalo maana yake ni mtu anayesingiziwa jambo, aghlabu huwa baya au lenye kutia fedheha.
Ukiangalia utendaji kazi wa Waziri Muhongo tangu alipoteuliwa na Rais kushika wadhifa huo na mchakato mzima wa sakata akaunti ya Tegeta Escrow hana tofauti na bangusilo.
Nasema bangusilo kwa sababu tangu Waziri Muhongo alipoteuliwa na Rais kushika wadhifa huo amejikuta katika mgogoro mkubwa wa kimaslahi na baadhi ya wafanyabiashara na wabunge.
Mgogoro huo ulihusisha wafanyabiashara ambao walitamaka waziwazi kwamba watahakikisha anang’olewa katika nafasi hiyo pengine kwa kuwa kikwazo kwao.
Na hili lilijitokeza zaidi pale Wizara ya Nishati na Madini chini ya uongozi wake ilipifuta leseni kadhaa za uchimbaji madini ambazo hazikuendelezwa na mgororo wa vitalu vya gesi.
Lakini pia kulikuwa na mgogoro wa chinichini kati yake na mmoja wa wafanyabiashara ambaye alitaka akabidhiwe mitambo ya kufua umeme kwa gesi ya Kinyerezi pindi itakapomalizika, lakini uongozi shupavu wa prof. Muhongo ulikataa ombi hilo na hivyo kuwa mwanzo wa chuki.
Hayo ni baadhi ya mambo yaliyo nyuma ya pazia katika sakata zima la Tegeta Escrow, ingawa yako mengi.
Ukiacha hayo Waziri Muhongo ndiye Waziri mwenye rekodi nzuri ya kuhakikisha mipango ya kufikisha umeme vijijini inahama kutoka katika makabrasha, porojo na kugeuza uhalisia.
Kutokana na uongozi wake upatikanaji wa umeme vijijini umeongezeka kutoka asilimia 2.5 mwaka 2007 hadi kufikia zaidi ya asilimia 21 hivi sasa.
Leo hii kila kona ya nchi hasa vijijini kuna miradi inaendelea na ujenzi na hilo linaonekana wazi hasa ukitembelea maeneo hayo.
Ili kuufanya umeme huo uwe na maana kwa wananchi wengi wa vijijini ambao wengi wao ni masikini Wizara ya Nishati na Madini chini ya uongozi wake ilishusha gharama za kuunganisha umeme vijijini kutoka shilingi 177,000 hadi shilingi 27,000.
Kimsingi kuna miradi mingi ya umeme vijijini inaendelea na ujenzi ni vyema Waziri Muhongo apewe muda aweze kuikamilisha kazi hiyo, kwa kuwa kumteua waziri mpya kusimamia Wizara hiyo kutarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana.
Leo hii wabunge kila mmoja anakiri aliyekuwa Waziri wa Maliasili Balozi Khamis Kagasheki alikuwa mchapakazi hodari, wamesahau kwamba wao ndiyo walikuwa wakishinikiza ajiuzulu kwamba hafai!
Tusipoangalia yanayosemwa kwa Balozi Kagasheki pia yatasemwa kwa Prof. Muhongo. Waswahili wanasema ujinga wakati wa kwenda kurudi njia umeshaijua, tujifunze kwa kumpoteza mchapakazi Kagasheki, tusimpoteze Muhongo.
Kama hiyo haitoshi, wakati anapewa majukumu ya kuwa Waziri wa Nishati na madini taifa lilikuwa likikabiliwa na tatizo kubwa la nishati ya umeme na hata kusababisha mgawao wa umeme, kupitia uongozi wake tatizo hilo limebaki historia.
Pamoja na hayo amekuwa akijitahidi pamoja na wenzake wizarani kuhakikisha makundi mbalimbali ya jamii yanapata uelewa wa masuala mbalimbali hasa kuhusu gesi ambapo madiwani, viongozi wa dini, waandishi wa habari wamepata fursa kwa udhamini wa wizara kufanya ziara za mafunzo ndani au nje ya nchi.
Waswahili wana msemo kwamba ‘Chuki mchchukieni lakini na sifa yake mpeni, Prof. Muhongo ni jembe wala hastahili kuwa bangusilo.
0 comments:
Post a Comment