UKAWA WAITESA CCM KATIKA MJINI MIKUBWA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA 2014, UKAWA YAPATA MAFANIKIO.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetikiswa na vyama vinavyounda Umoja ya Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwenye matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Katika uchaguzi huo uliofanyika nchini juzi, matokeo yanaonyesha kupanda kwa vyama vya upinzani hasa kwa kushinda maeneo yaliyokuwa yakiongozwa na CCM hali iliyokitikisa vilivyo chama hicho tawala.
Kutangazwa huko kwa matokeo hayo kunakuja baada ya kukamilika kwa uchaguzi huo katika baadhi ya maeneo nchini.
Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
MTWARA
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Limbakisye Shimwela, ametangaza matokeo ya jumla na kusema kuwa manispaa hiyo ina mitaa 111, ambako CCM imeshinda mitaa 54, sawa na asilimia 48.6, CUF 36 asilimia 32.4, Chadema 16 asilimia 14.4, NCCR-Mageuzi mitaa minne asilimia 3.6 na TLP kiti kimoja, asilimia 1.
Kutokana na idadi hiyo ipo mitaa ambayo inaongozwa na CCM lakini bado imejikuta ikiwa nyuma ya vyama vya upinzani ambavyo vipo mbele kwa kupata mitaa 57 dhidi ya CCM yenye mitaa 54.
MASASI
Msimamizi wa Uchaguzi wa katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, Beatrice Dominic, alisema wilaya hiyo ina vijiji 159, ambako CCM imeshinda vijiji 150, Chadema 4, CUF 4 na NLD kimoja, ambacho awali hakikuwa na kiti hata kimoja wilayani humo.
Alisema kuwa mitaa miwili haijafanya uchaguzi kutokana mgombea kufariki dunia na wengine wanarudia leo.
CCM, CHADEMA WAVUTANA
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepoteza mitaa 72 kati ya mitaa 175 katika uchaguzi wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Nyamagana, Mwanza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Halifa Hida, katika matokeo ya jumla CCM imeibuka na ushindi katika mitaa 96, ambayo ni asilimia 54.86, huku Chadema wakiibuka na ushindi wa mitaa 70, asilimia 40 kutoka mitaa mitatu waliyokuwa wakiishikilia.
Chama cha Wananchi CUF kimeibuka na ushindi mitaa saba, asilimia 4, huku chama kipya cha ACT kikiibuka na mtaa mmoja tu, asilimia 0.57.
Katika Kata ya Mabatini yenye mitaa 6, CCM ilipata viti 5, Chadema 1, Kata ya Mbugani yenye mitaa 6, CCM 3 Chadema 3, Kata ya Butimba yenye mitaa 8, CCM mitaa 3, Chadema 5.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, Kata ya Luchelele ina mitaa 10, CCM 4 na Chadema 5, Kata ya Mirongo mitaa 3, CCM 2 CUF 1, Kata ya Nyegezi mitaa 8, CCM 2 Chadema 6, Kata ya Mkuyuni mitaa 8, CCM 3, Chadema 3 na CUF 2.
Kata nyingine ni kata ya Lwanhima mitaa 18, CCM 16 Chadema 2, Kata ya Buhongwa mitaa18, CCM 14 Chadema 4.
Kwa mujibu wa Hida, Kata ya Nyamagana ambayo ina mitaa 4, CCM 2, Chadema 2, Kata ya Mkolani mitaa 10, CCM 5 Chadema 5, kata ya Igogo mitaa 9, CCM 4 Chadema 1 na CUF 4, Kata ya Pamba mitaa 10, CCM 7 Chadema 3, Kata ya Igoma mitaa 14, CCM 7 Chadema 6 na ACT 1, Kata ya Kishiri 12, CCM 6 na Chadema 6.
Katika Kata ya Mahina yenye mitaa 9, CCM 4 na Chadema 5, Kata ya Mhandu mitaa 11, CCM 6 na Chadema 5, Kata ya Isamilo mitaa 11, CCM 3 na Chadema 8.
MANISPAA YA ILEMELA.
Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi, Justun Lukaza, ametangaza kuwa katika mitaa 172, CCM imeshinda mitaa 106, sawa na asilimia 63 na Chadema 62, sawa na asilimia 37, mitaa mine itarudia uchaguzi kutokana na vifaa kuchelewa na kupata pungufu na vurugu kutokea.
CCM YAGARAGAZWA SHINYANGA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Manispaa ya Shinyanga kimeibuka kidedea baada ya kujizolea viti katika mitaa 29 huku CCM ikipata viti katika mitaa 26.
Msimamizi wa Uchaguzi katika Jimbo la Shinyanga Mjini, Festo Kang’ombe, alisema kati ya vijiji 17, CCM kilishinda vijiji 14 na Chadema iliambulia ushindi katika kijiji kimoja.
Kang’ombe alisema kati ya vitongoji 84 katika Manispaa hiyo, CCM imeshinda katika vitongoji 65 na Chadema ilipata ushindi katika vitongoji 18.
Alisema uchaguzi utarudiwa kesho katika Mtaa wa Katunda katika Manispaa hiyo, baada ya kushindwa kufanya uchaguzi kutokana na picha na majina ya wagombea kuchanganywa katika fomu na kuhitilafiana na nembo za vyama.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Felix Kimaro, alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata mitaa 18 kati ya 32 na CCM ikishinda mitaa 14.
Mgombea aliyetimkia CCM achaguliwa.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika Mtaa wa Mageuzi, Kata ya Ngokolo, Manispaa ya Shinyanga, Emanuel Joshua, aliyekihama chama chake Chadema na kuhamia CCM, alichaguliwa huku akiwa hayupo.
SONGEA MJINI
Chama Cha Mapinduzi kimepata ushindi wa mitaa 69 kati ya mitaa 95, sawa na asilimia 72.6, Chadema mitaa 24 sawa na asilimia 25.2 na Chama cha Wananchi (CUF) kikipata mitaa miwili sawa na asilimia 0.4, ambapo katika uchaguzi wa mwaka 2009, Chadema ilipata mitaa 6 na CUF haikuwa na mtaa hata mmoja katika Manispaa ya Songea.
TANGA
Taarifa kutoka mkoani Tanga zinaeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi katika mitaa 118, huku CUF ikishinda mitaa 60 na Chadema mitaa miwili.
Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2009, CUF ilikuwa na mitaa 42 na kwa sasa kimeongeza mitaa mipya 18, huku Chadema ikiongeza mtaa mpya mmoja tofauti na ule wa awali waliokuwa nao.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Jiji la Tanga ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji hilo, Juliana Mallange, kwa upande wa wajumbe mchanganyiko CCM imepata wajumbe 356 na viti maalumu 230, CUF wajumbe 117 na viti maalumu 62, ambapo Chadema imepata wajumbe 3 na viti maalumu viwili.
Malange alisema wananchi wengi hawakujitokeza kupiga kura ingawa walikuwa wamejiandikisha.
“Tuliandikisha watu 163,999, lakini kati ya hao waliojitokeza ni asilimia 48 pekee,” alisema.
Alisema watalazimika kufanya uchaguzi katika maeneo ya Ndumi na Ngamiani Kaskazini kutokana na uchaguzi kuingiliwa na dosari, ikiwemo wagombea kuwekewa pingamizi.
HANDENI.
Msimamizi wa Uchaguzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Thomas Mzinga, alisema katika vijiji 60, CCM imeshinda 50 kwa kupita bila kupingwa na kati ya hivyo, vijiji 10 pia ilipata vijiji 7 na Chama cha CUF kikipata vijiji vitatu.
Hata hivyo, kata 20 kati ya 33 wilayani Muheza zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana na ucheleweshaji wa karatasi za kupiga kura.
DAR ES SALAAM
Jiji la Dar es Salaam lina ya Mitaa 559 ambako CCM imeshinda mitaa 359, Chadema 72, CUF 44 huku mitaa 82 ikiwa hajafanya uchaguzi.
Taarifa kutoka Mkoa wa Kilimanjaro zinaeleza kuwa Manispaa ya Moshi imetangaza matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika ambako kati ya kata 21 mitaa 54 kati ya 60 imefanya uchaguzi.
Wilaya ya Temeke Dar es Salaam yenye mitaa 209 na majimbo mawili ya Temeke na Kigamboni, katika uchaguzi huo Chama cha Wananchi (CUF) kimeshinda mitaa 33, kati ya hiyo, mitaa 10 kimeshinda katika Jimbo la Temeke na mitaa 23 katika Jimbo la Kigamboni.
Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Temeke, Rehema Kawambwa, alisema katika uchaguzi wa mwaka 2009 walikuwa na mitaa 15 tu hivyo imeongezeka mitaa 18.
“Mitaa mingi tumeikosa kwa sababu ya kufanyiwa hujuma, kwenye maeneo mengi majina ya wapiga kura yalikuwa hayaonekani, mtu anaambiwa weka sahihi nikakutafutie jina lako halafu mwisho wa siku anaruhusiwa kupiga kura bila jina kuonekana,” alisema Kawambwa.
Alisema katika mtaa wa Charambe, karatasi za kupigia kura zilikuwa hazina majina ya wajumbe, wakati katika mtaa wa Wailes zililetwa karatasi za wagombea wa Kongowe.
Naye Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke, Bernard Mwakyembe, alisema kimefanikiwa kupata mitaa 32 kutoka mtaa mmoja waliokuwa nao baada ya uchaguzi wa mwaka 2009.
“Kwa ujumla tunashukuru kuna mafanikio, kwa sababu kutoka mtaa mmoja hadi mitaa 32 si kazi ndogo,” alisema Mwakyembe.
ARUSHA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimefanikiwa kuongeza idadi ya mitaa yake katika jiji la Arusha na kufikia 75 kutoka mitaa saba ya awali.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, CCM imeongoza kwa kuwa mbele kwa kupata viti 78, ikifuatiwa na Chadema yenye mitaa 75.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Idd Juma, alisema katika uchaguzi huo nafasi za wajumbe na wajumbe wa vitia maalumu bado kura zinaendelea kuhesabiwa.
“Katika uchaguzi wa nafasi za Wenyeviti, CCM imepata viti 78 ambavyo kati ya hivyo, viti 6 walipita bila kupingwa, Chadema (7), ACT (0), NCCR Mageuzi (0), TLP (0) na CUF (0), ila kwa nafasi za wajumbe na wale wa viti maalumu bado zoezi la kuhesabu kura linaendelea,” alisema.
Alisema juzi siku ya uchaguzi hadi saa 1.45 jioni vituo 153 vilishamaliza kupiga kura na katika kituo kimoja cha Longdom, Sokoni I zoezi la kupiga kura lilimalizika saa 4.10 usiku.
CCM YASHINDA MONDULI
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Monduli kimeshinda nafasi zote katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Monduli, Twalib Mbasha, CCM imepata ushindi wa asilimia 100 kwa kushinda katika vijiji vyote 62 ambako uchaguzi ulifanyika katika vijiji 15 baada ya wagombea wa CCM katika vijiji 47 kupita bila kupingwa na kushinda katika vitongoji vyote 236.
Akizungumzia matokeo hayo, Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema ametimiza ahadi yake kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo jimboni kwake kwa kushinda nafasi zote.
“Nimetimiza ahadi yangu kuwa nakwenda jimboni kuhakikisha Monduli inabaki kuwa ngome ya CCM,” alisema Lowassa.
KILIMANJARO
Taarifa kutoka Mkoa wa Kilimanjaro zinaeleza kuwa Manispaa ya Moshi imetangaza matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika ambako kati ya kata 21 mitaa 54 kati ya 60 imefanya uchaguzi.
Msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Moshi, Shaabani Ntarambe alisema Chadema imefanikiwa kupata mitaa 26 huku CCM ikitetea mitaa 28.
Na katika Wilaya ya Hai ambalo Mbunge wake ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaongoza kwa kupata ushindi wa vijiji 32, Chadema vijiji 20 kati ya vijiji 65 vilivyopo kwenye wialaya hiyo.
Kwa upande wa vitongoji CCM katika matokeo ya awali inaonyesha kushinda vitongoji 98, huku Chadema ikishinda 37 na CUF kitongoji kimoja.
Katika Jimbo la Vunjo, matokeo ya awali yanaonyesha chama cha NCCR- Mageuzi kimeshinda vijiji 31, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda vijiji 24, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikipata viti 16, huku Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kikiambulia viti saba.
Hata hivyo, hadi tunakwenda mitamboni, matokeo ya vitongoji bado yalikuwa hayajatangazwa kutokana na miundombinu mibovu kutoka katika vitongoji kwa mujibu wa wasimamizi wa uchaguzi kutoka katika vituo mbalimbali jimboni humo.
Katika Uchaguzi wa mwaka 2009, chama cha TLP kinachoongozwa na Mbunge wa sasa, Augustino Mrema, ndicho kilichoongoza kwa kupata vijiji vingi, kikiwa na vijiji 30 kati ya 78.
Katika uchaguzi huo, NCCR -Mageuzi ilipata kiti kimoja, CCM ikapata viti 45, huku TLP ikipata vijiji 28 na Chadema ikipata vijiji 6.
PWANI
Matokeo ya Uchaguzi katika Mkoa wa Pwani upande wa Wilaya ya Kibaha mitaa yote ni 73, ambako Chadema wamechukua mitaa 10, CCM mitaa 62, mtaa wa Kilimahewa kura zilizopigwa ziligongana kwa wagombea wa CCM na CHADEMA na hivyo utaratibu wa kurudia uchaguzi unapangwa.
Kibaha Vijijini vijiji vilivyopo ni 32, ambako CCM ilishinda mitaa 31, mitaa 10 ilishinda bila kupingwa, sawa na asimilia 96.9, upinzani ulishinda kijiji kimoja sawa na asilimia 13.1.
Wilaya ya Bagamoyo vijiji vilivyopo ni 75, CCM ilishinda vijiji 67 sawa na asilimia 90.5, lakini vijiji 8 kati ya vilivyopo havijafanya uchaguzi, vitongoji vipo 610, CCM ilishinda 540, sawa na asilimia 88.5, vitongoji 45 havijafanyiwa uchaguzi, wapinzani walishinda vitongoji sawa na asilimia 4.1.
Kisarawe Vijiji vilivyopo 66, CCM ilishinda vijiji 57, sawa na asilimia 86.4, wapinzani vijiji tisa sawa na asilimia 13.6, vitongoji 234 CCM 206, sawa na asilimia 88, Chadema vitongoji 2, CUF 26.
CHALINZE
Katika jimbo hilo idadi ya vijiji ni 75 na CCM imefanikiwa kupita bila kupingwa ni vijiji 38 wakati vijiji vilivyofanya uchaguzi ni 29.
CCM pia imepata ushindi katika vijiji vyote 10 vilivyopiga kura huku matatizo yakiwa yametokea katika vijiji vinane ambako uchaguzi utarudiwa.
Jimbo la Chalinze lina vitongoji ni 610 na CCM imepita bila kupingwa katika vitongoji 303.
Idadi ya vitongoji vilivyofanya uchaguzi ni 262 na CCM imeshinda 242, sawa na asilimia 90 ya vitongoji vyote wakati chama cha CUF kimepata vitongoji 10 na Chadema vitongoji 10.
MBEYA
Matokeo ya awali yaliyotolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mwangi Kundya, yanaonyesha CCM kimefanikiwa kuzoa idadi kubwa ya vijiji hadi sasa.
Alisema matokeo ya awali katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya lenye mitaa 181, CCM imefanikiwa kupata mitaa 106, Chadema 71, NCCR-Mageuzi mtaa mmoja.
Wilaya ya Chunya yenye Vijiji 86, vijiji vilivyokamilisha hesabu ni 74, CCM ilipata vijiji 67, Chadema vijiji 7, wakati kwa vitongoji CCM ilipata vitongoji 270, huku Chadema ikiambulia vitongoji 18.
Wilaya ya Ileje vijiji vyote ni 71 na vijiji 32 vimekamilisha matokeo yake CCM ilipata vijiji 23, Chadema vijiji 9.
Wilaya ya Kyela vijiji vyote 93 vimekamilisha matokeo yake na CCM imepata 79, Chadema 13, huku uchaguzi wa kijiji kimoja utarudiwa na kwa vitongoji 469, CCM vitongoji 377, Chadema 88, wakati vitongoji vinne uchaguzi utarudiwa.
Wilaya ya Mbarali yenye vijiji 102, CCM 81, Chadema 16, vijiji sita vitafanya uchaguzi wa marudio na vitongoji jumla ni 713 ambako CCM imeshinda vitongoji 570 , Chadema ikipata 79.
Wilaya ya Mbozi, vijiji vilivyopo ni 125 nakati ya hivyo, 92 matokeo yake yalikuwa tayari huku CCM ikiwa imepata viti 84 na Chadema imepata vijiji vinane na vijiji 33 matokeo yalikuwa bado na kwa upande wa vitongoji 664, CCM imepata 557 na Chadema 110, CUF viwili, TLP ikiambulia kiti kimoja.
Wilaya ya Rungwe vijiji 155, CCM imepata 132, Chadema 22, CUF kimoja na vijiji vitano uchaguzi utarudiwa, huku vitongoji vilivyopo ni 694, CCM 578, Chadema 111, CUF viwili na TLP viwili.
Wilaya ya Momba matokeo yake yamegawanywa katika sehemu mbili kutokana na wilaya kuwa na Halmashauri ya Mji wa Tunduma. Kwa upande wa vijiji jumla ni 72, CCM imepata vijiji 43, Chadema 24 na vijiji vitano uchaguzi utarudiwa.
Mitaa katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma ni 71, CCM imechukua mitaa 25, wakati Chadema imeongoza kwa kupata mitaa 46, hivyo kulazimika kuunda halmashauri ya mji.
TABORA MJINI
Taarifa kutoka Manispaa ya Tabora ambayo ina mitaa 130, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanikiwa kupata mitaa 86, sawa na asilimia 66, CUF mitaa 28 asilimia 21, Chadema mitaa 14 asilimia 14, huku vyama vya NCCR-Mageuzi na UDP kila kimoja vikishinda kiti kimoja.
DODOMA
Katika Wilaya ya Kondoa, matokeo yaliyopatikana ni ya kata 12 kati ya 28 ambapo katika nafasi ya mwenyekiti wa kijiji CCM ilipata 12, CUF 2 na Chadema 2.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa, Isdory Mwalongo, kwa vitongoji, CCM 89, CUF 13, Chadema viwili.
Wajumbe wa serikali ya kijiji CCM 97, CUF 15 na viti maalum CCM 83, CUF 14.
Katika Halmashauri ya Chemba, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. William Mafwere, alisema vijiji 113 vimefanya uchaguzi na matokeo yaliyopo kwa sasa ni ya vijiji 100.
Alisema kwa nafasi ya mwenyekiti wa kijiji, CCM 73, Chadema 9 na CUF 14, na kuongeza kuwa vijiji vinne vimerudia uchaguzi leo.
Kwa upande wa mwenyekiti wa kitongoji, alisema vitongoji 406 vimefanya uchaguzi ambapo CCM ilipata 313, Chadema 43, CUF 45 na NCCR-Mageuzi imepata kimoja, pia vitongoji vinne vinarudia uchaguzi leo.MTANZANIA
0 comments:
Post a Comment