Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Dk. Festus Limbu.
Serikali inakabiliwa na hali ngumu kifedha kiasi cha kushindwa kulipa madeni ya ndani yenye thamani ya Sh. trilioni 1.458.
Miongoni mwa wanaoidai fedha hizo ni watumishi wake, wazabuni, wakandarasi na watalaam washauri.
Madeni hayo yaliwasilishwa serikalini hadi Desemba 31, mwaka jana.
Akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambacho kilihudhuriwa na maofisa wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk. Festus Limbu (pichani), alisema hadi wakati huo ni Sh. bilioni 286.92 tu ndizo zilizokuwa zimelipwa.
Kwa upande wake, Waziri Nchemba alisema Serikali bado inafanya tathmini ya deni halisi ambalo inadaiwa na itatoa taarifa ndani ya mwezi huu.
MATUMIZI MAKUBWA.
Aidha, Kamati hiyo iliijia juu Serikali baada ya kubaini kwamba haina nidhamu katika matumizi yake.
Dk. Limbu alisema Serikali imetumia Sh. trilioni 1.426 ambazo hazikuidhinishwa na Bunge.
Kadhalika, Kamati imebaini kwamba katika mwaka huu wa fedha 2014/15, Serikali imepanga kutumia kiasi cha Sh. trilioni 2.061 ambazo hazijaidhinishwa na Bunge.
Alisema matumizi hayo ni kinyume cha sheria na kwamba jambo ambalo serikali ilipaswa kufanya kabla ya kutumia fedha hizo ni kurudi bungeni kuomba bajeti ya ziada.
Dk. Limbu alisema makadirio ya serikali ni makusanyo ya ndani kufikia asilimia 95 wakati mapato yasiyo ya kodi yanatarajiwa kufikia asilimia 60, huku misaada na mikopo nafuu inatarajiwa kufikia asilimia 60.
Pia alisema serikali imetumia Sh. bilioni 345 za bajeti ya 2014/ 15 kugharimia malipo ya bajeti ya 2013/14 bila idhini ya Bunge.
Dk. Limbu alisema baadhi ya maeneo ambayo fedha hizo zilipelekwa bila idhini ya Bunge ni Tume ya Taifa Uchaguzi (Nec), ambayo awali ilikuwa imeidhinishiwa Sh. bilioni 2.8 kwa mwaka mzima, lakini hadi mwisho wa nusu mwaka zilikuwa zimetolewa Sh. bilioni 16.357 kwa ajili yakufanyia shughuli zake. Matumizi hayo ni sawa na asilimia 574 ya bajeti ya mwaka mzima.
Mengine ni fedha zilizotolewa kwenye miradi ya maendeleo na kwa matumizi ya kawaida Sh. trilioni 1.529 sawa na asilimia 97.
Nyingine zilizotumika bila idhini ni zilizopelekwa katika Bunge Maalum la Katiba na uchaguzi wa serikali za mitaa.
Alisema kutumia fedha ambazo zimewekewa uzio (ring-fenced), hususani barabara na umeme vijijini katika matumizi mengine ni kinyume cha sheria na pia inachangia kukwamisha shughuli za maendeleo katika maeneo husika yaliyotengewa bajeti.
Kadhalika, alisema serikali imekuwa ikitumia matumizi makubwa ya fedha, tofauti na kiwango cha makusanyo ya mapato na kwamba makusanyo yaliyotokana na kodi kutoka TRA hadi Desemba 31, mwaka jana yalikuwa asilimia 95 ambayo hata hivyo, hayakufanya vizuri.
Sababu za kutokufanya vizuri alisema ni fedha za wafadhili kutotolewa kama ilivyopangwa, makusanyo ya maduhuli kwa serikali kuu na serikali za mitaa kuwa chini, mwitiko hasi wa wafanyabiashara kuhusiana na mashine za kielektroniki (EFD) na kutokuwapo mifumo madhubuti ya ukusanyaji mapato hayo.
Aidha, akieleza utekelezaji wa bajeti ya serikali ya 2014/ 15, Dk. Limbu alisema katika mwaka huo wa fedha, Bunge liliidhisha serikali ikusanye mapato na itumie jumla ya Sh. Trilioni 19.853 ikilinganishwa na Sh. Trilioni 18. 249 mwaka 2013/14.
Alisema mapato ya ndani yaliyoindhinishwa kukusanywa ni Sh. trilioni 12.178, mikopo trilioni 2.265, mikopo ya masharti ya kibiashara Sh. trilioni 1.32, misaada ya nje trilioni 0.922 na mapato ya halmashauri trilioni 0.458 wakati misaada ya maendeleo toka nje ilikuwa Sh. trilioni 2.019.
Bajeti ya matumizi ya kawaida ilikuwa Sh. trilioni 13. 38, bajeti ya maendeleo Sh. trilioni 6.473 ambayo ilihusisha fedha za ndani Sh. trilioni 4.453 na fedha za nje Sh. trilioni 2.019.
Dk. Limbu alisema fedha za maendeleo zilizotolewa hadi Desemba, mwaka jana kwa matumizi ya kawaida zilikuwa Sh. trilioni 1.529, wakati katika bajeti ya maendeleo, fedha za ndani zilizotolewa kwa maendeleo kwa nusu mwaka ni Sh. trilioni 1.091 kati ya Sh. trilioni 3.846., fedha za nje zilitolewa Sh. bilioni 223.5 kati ya Sh. trilioni 1.63 zilizoahidiwa na kupitishwa na Bunge kwa mwaka mzima.
Alisema fedha zilizopelekwa kwenye halmashauri za wilaya kwa ajili ya matumizi ya kawaida kwa nusu mwaka kwa ajili ya matumizi ya kawaida ni bilioni 127.2 , wakati zilizopelekwa kwa ajili ya maendeleo zilikuwa Sh. bilioni 45.7.
Kadhalika, baadhi ya mambo ambayo kamati hiyo iliishauri serikali ni kuweka vipaumbele vichache vinavyotekelezeka kulingaa na mapato, kuweka mifumo ya kuisaidia kukusanya kiwango kikubwa cha mapato yasiyotokana na kodi, kuonyesha madeni ya mwaka uliopita kwenye bajeti ya mwaka unaofuata ili yaidhinishwe na Bunge pamoja na kutafuta fedha kwa miezi mitatu na nusu kilichobaki kwa ajili ya utekelezaji bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment