Askofu Gwajima.
MAHOJIANO baina ya Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima na Jeshi la Polisi yaliyokuwa yaendelee jana jijini Dar es Salaam, yalishindwa kufanyika baada ya mawakili wa Gwajima kutaka kwanza wapewe waraka maalumu wa kutakiwa apeleke nyaraka walizomuagiza.
Kutokufanyika kwa mahojiano hayo kulithibitishwa na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Akizungumzia sababu za kiongozi huyo wa kiroho kutofika Polisi kuendelea na mahojiano, Kova alisema hiyo imesababishwa na Jeshi la Polisi kusubiri kupata ushauri wa kisheria kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), ndipo wajue nini cha kufanya kuhusiana na madai yaliyowasilishwa na mawakili wake.
"Ni kweli Gwajima hajafika kama ilivyotakiwa afanye hivyo na suala lake bado tunalishughulikia. Kwa sasa tunasubiri ushauri kutoka kwa DPP na baada ya hapo tutaitisha kikao na waandishi wa habari kutoa taarifa kwa ujumla inayozungumzia mwenendo wa kesi yake," alisema Kamanda Kova.
Gwajima alitakiwa afike kuendelea na mahojiano na polisi jana kwa kile kilichodaiwa ni kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini mwezi uliopita na kuilazimu Polisi kumtaka ajisalimishe mwenyewe kituoni.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Wiki iliyopita Polisi ilimtaka kiongozi huyo kuwasilisha nyaraka kumi za mali na vitu vingine anavyovimiliki ili kuendelea na mahojiano, lakini siku chache baadaye kupitia kwa mawakili wake, John Mallya na Peter Kibatala, aliwasilisha barua kupinga kupeleka nyaraka hizo na kulitaka Jeshi la Polisi kutoa waraka maalumu unaomtaka yeye kuwasilisha nyaraka hizo na pia waseme ni sheria gani waliyotumia kumtaka apeleke nyaraka hizo.
Akizungumza na Gazeti hili juzi, ikiwa ni siku moja kabla ya kuripoti Polisi, Mallya alisema bado hawajapokea majibu kutoka Polisi kuhusiana na barua yao na hivyo wangeenda kuripoti kama walivyoambiwa bila ya kupeleka nyaraka hizo.
Hata hivyo kutokana na kauli ya Kamanda Kova, haijajulikana ni lini tena kiongozi huyo atarejea kuendelea na mahojiano hadi hapo polisi watakapotoa taarifa ya kumtaka afike kuendelea na mahojiano kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.
Gwajima alitakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu za hati ya usajili wa kanisa lake, namba ya usajili wa kanisa, hati ya umiliki wa helikopta, hati ya nyumba anazomiliki, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake pamoja na ritani za kanisani zinazohusu mapato na matumizi ya kanisani.
Nyaraka zingine ni bodi ya wadhamini wa kanisa na majina yao, mtu anayerekodi picha za video kanisani siku ya ibada na shughuli nyingine za kanisani hapo na waraka wa maaskofu uliosomwa makanisani na kuzua mtafaruku, baada ya Gwajima kudaiwa kumshambulia kiongozi mwenzake wa dini hivi karibuni.HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / kitaifa
/ ASKOFU GWAJIMA AIVURUGA JESHI LA POLISI, SASA SAKATA LAKE LATUA KWA DPP KWA KUAMULIWA.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment