BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HAWA NDIYO WABUNGE 10 MACHACHARI LAKINI KUNA WABUNGE 10 WAKIMYA KATIKA BUNGE LA MWAKA 2014/2015



Dar es Salaam. Imebainika kuwa wakati Bunge la Kumi likiwa limebakiza mkutano mmoja tu wa bajeti kuhitimisha ngwe yake ya miaka mitano, wapo baadhi ya wabunge ambao hawajauliza swali la msingi, la nyongeza wala kuchangia chochote.


Kwa mujibu wa tovuti ya Bunge inayoonyesha idadi ya maswali yaliyoulizwa na michango ya kila mbunge, wapo wabunge wawili ambao hawajawahi kuuliza wala kuchangia chochote tangu Bunge hilo, lenye wabunge 358, lilipoanza Uchaguzi Mkuu uliopita hadi sasa.


Vilevile, tovuti hiyo inabainisha majina ya wabunge waliofanya vizuri zaidi katika kila eneo, yaani maswali ya msingi, ya nyongeza na michango waliyotoa katika mijadala mbalimbali.


Katika orodha hiyo, Spika Anne Makinda, ambaye pia ni mbunge wa Njombe Kusini, ndiye anayeonekana kinara kwa kuchangia mara 2,055 pale anapoongoza Bunge na kuuliza swali moja huku naibu wake, Job Ndugai (Kongwa) akiwa amechangia mara 1,350 bila kuuliza swali hata moja.


Kiwango cha michango ya wabunge kimeelezwa na baadhi ya wasomi kuwa inategemea mambo mengi, ikiwamo mbunge kuwa sehemu ya Serikali na hivyo kushindwa kuihoji, uwezo wake kielimu na msimamo wake kiitikadi. “Wabunge wengine tunaona ni wafanyabiashara ambao hawana elimu. Walishinda kwenye uchaguzi kutokana na fedha zao lakini hawana uelewa wa mambo. Sasa hawa hawawezi kuchangia chochote kwa sababu hawajui,” alisema Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu) alipoulizwa kuhusu suala hilo.


Katibu msaidizi wa Bunge, Emmanuel Mpanda alisema pamoja na kuwa taarifa za tovuti hiyo zinahuishwa mara kwa mara, zilizomo kwa sasa hazihusishi michango ya wabunge ya Mkutano wa 19 uliomalizika Aprili Mosi.


Alisema orodha ya wabunge 10 waliochangia sana na wengine 10 waliochangia mara chache, haihusishi kiti cha spika, wenyeviti wa Bunge na mawaziri.


Wabunge 10 wenye michango michache
Nambari moja inashikwa na wabunge wawili ambao pia ni viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambao ni mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Mohamed Said Mohamed (CCM) ambaye ni mwakilishi wa Mpendae na Naibu Waziri wa Kilimo na Maliasili, pamoja na mbunge wa Kitope (CCM), Balozi Seif Ali Iddi ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar. Hao ndiyo pekee ambao hawakuchangia kitu chochote bungeni.


Anayefuatia ni mbunge wa Babati Mjini, Kisyeri Chambiri (CCM) ambaye amechangia mara nne lakini hakuwahi kuuliza swali lolote.


Katika orodha hiyo wabunge waliochangia mara tano bila kuuliza maswali yoyote ni Dk Mohamed Seif Khatibu (Uzini - CCM), Edward Lowassa (Monduli), Shawana Hassan (Dole - CCM). Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa aliuliza maswali matatu ya nyongeza na kuchangia mara mbili.


Mwingine ni Ali Haji Juma wa (Chaani – CCM) aliyechangia mara nne, akauliza swali moja la msingi na moja la nyongeza.


Wanafuatia Khamis Ali Kheir wa Jimbo la Kwamtipura (CCM) aliyechangia mara nane bila kuuliza swali lolote, wabunge wa viti maalumu (CCM), Mwanakhamis Kassim Said aliyeuliza swali moja la msingi na kuchangia mara saba na Kiumbwa Mbaraka aliyeuliza maswali manne na kuchangia mara tatu.


Wabunge 10 waliochangia zaidi
Wabunge waliochangia mara nyingi wanaongozwa na John Mnyika wa Ubungo (Chadema) ambaye amechangia mara 540 na kuuliza maswali 16 ya msingi na 52 ya nyongeza.


Anayefuatia katika orodha hiyo ni Tundu Lissu (Singida Mashariki - Chadema) mwenye michango 276, maswali manane ya msingi na 24 ya nyongeza.


Mbunge wa tatu ni wa Kasulu Mjini (NCCR - Mageuzi), Moses Machali ambaye aliuliza maswali 23 ya msingi, 68 maswali ya nyongeza na kuchangia mara 214.


Nambari nne imekwenda kwa Mbunge wa Kilwa (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza maswali 26 ya msingi 74 ya nyongeza na kuchangia hoja mara 131.


Mbunge wa tano ni Diana Chilolo (Viti Maalumu-CCM) aliyeuliza maswali ya msingi 19, ya nyongeza 88 na michango 116, wa sita ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu - Chadema) aliyeuliza maswali 23 ya msingi, 60 ya nyongeza na kuchangia mara 139.


Anayeshika namba saba ni Halima Mdee wa Kawe (Chadema) aliyeuliza maswali 11 ya msingi, 32 ya nyongeza na michango 175. Nambari nane imeshikwa na Felix Mkosamali (Muhambwe-NCCR) aliyeuliza maswali 19 ya msingi, 44 ya nyongeza na michango 151.


Aliyeshika namba tisa ni Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini - Chadema) aliyeuliza maswali 13 ya msingi, 49 ya nyongeza na michango 149 kabla ya kujiuzulu ubunge baada ya kufukuzwa uanachama na chama chake.


Mbunge wa 10 ni Seleman Jafo (Kisarawe-CCM) aliyeuliza maswali ya msingi 17, ya nyongeza 35 na michango 141.


Mtazamo wa wasomi
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Rucu), Gaudence Mpangala alisema hatua ya baadhi ya wabunge kukaa kimya bungeni ina sura mbili. Kwanza; baadhi yao wanajiona ni sehemu ya Serikali kwa hiyo wanaogopa kuikosoa.


Alisema kundi hili linajumuisha baadhi ya wabunge ambao ni mawaziri, waliowahi kuwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na baadhi ya wabunge kutoka CCM.


Kundi la pili, Profesa Mpangala alisema ni la wabunge wenye upeo mdogo wa mambo, kwa kuwa ili mbunge aweze kuuliza maswali na kuchangia hoja, lazima awe na upeo mkubwa wa mambo ya kijamii, kiuchumi na kimataifa.


Mwanazuoni huyo alikumbuka pendekezo lililotolewa kwenye Rasimu ya Katiba kuweka sifa ya elimu kwa mbunge, lakini likatupiliwa mbali kwa sababu kiligusa masilahi ya wabunge wengi.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Bakari Mohamed alisema kuna mambo ambayo Serikali inakuwa imeweka msimamo, hivyo wabunge walio kwenye mrengo wa Serikali hawawezi kuuliza au kuchangia kinyume na msimamo waliouweka.


Alisema wabunge wanatofautiana kiutendaji, baadhi wakijizatiti kwenye majimbo yao bila kuona umuhimu wa kuzungumza bungeni.


Hata hivyo, alisema wabunge wa namna hiyo hawana sifa za kuwa wabunge kwa sababu ni udhaifu mkubwa kukaa bungeni miaka mitano ukashindwa kuuliza au kuchangia chochote chenye masilahi kwa wananchi.


Msomi huyo aliongeza kuwa pamoja na kuwapo viongozi wa Serikali bungeni ambao hawawezi kuikosoa, jambo hilo haliwanyimi fursa ya kuuliza au kuchangia juu ya mambo yanayohusu majimbo yao.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: