KISA CHA POLISI ZAIDI YA 18 KUZINGIRA NYUMBA YA ASKOFU GWAJIMA NDIYO HIKI.
GAri yan Polisi ikirandaranda nyumbani kwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na UZima Josephat Gwajima maeneo ya Salasala.
Dar es Salaam. Askari zaidi ya 20 jana waliizingira nyumba ya Askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa zaidi ya saa sita wakitaka kumtia nguvuni lakini hawakufanikiwa na baada ya kuondoka, muhubiri huyo alitoka na kwenda mwenyewe Mahakama ya Kisutu alikofunguliwa mashtaka.
Kiongozi huyo wa kiroho alifunguliwa mashtaka ya kutoa lugha chafu na kuacha silaha katika mikono isiyo salama.
Askofu Gwajima aliingia matatani na Jeshi la Polisi baada ya kumrushia maneno makali Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo wa Kanisa Katoliki kutokana na kutofautiana na viongozi wenzake wa Kikristo kuhusu Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Jukwaa la Wakristo lilitoa tamko la kuwataka waumini wapigie kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa, lakini Kardinali Pengo akawapinga akisema waumini wanatakiwa wafanye uamuzi wenyewe, ndipo Askofu Gwajima alipomrushia maneno hayo.
Jana, hali ilikuwa ya kutatanisha kwenye nyumba ya askofu huyo iliyopo Madale, wilayani Kinondoni ambako askari hao wa Jeshi la Polisi waliokuwa na silaha za moto wakiwa kwenye magari yapatayo saba, waliweka kambi nje ya nyumba hiyo kuanzia majira ya saa 11:00 alfajiri.
Kwa mujibu wa mashuhuda, Askofu Gwajima hakuwafungulia askari hao lango la uzio wa nyumba yake ya ghorofa licha ya kugonga kwa muda mrefu.
Mwandishi wa Mwananchi aliyefika eneo la tukio tangu saa 12:30 asubuhi, alikuta magari hayo, baadhi ya aina ya Land Rover Defender yakiwa yameegeshwa nje ya nyumba huku baadhi ya askari wapatao 10 wakiwa na bunduki aina ya SMG.
Hakukuwa na mtu yeyote kutoka kwenye nyumba hiyo ya Askofu Gwajima aliyetoka ndani kwa muda wote ambao askari hao walikuwa nje.
Ilipofika saa 3:00 asubuhi, askari zaidi waliongezeka wakiwemo askari kanzu huku waumini na waandishi wakianza kumiminika.
Hata hivyo, waumini wengi walizuiwa kufika eneo hilo kabla ya Mchungaji Msaidizi, Kabiyagze naye kufika saa moja baadaye na kisha kwenda eneo walikokuwa waumini wake na kuzungumza nao.
Polisi hao waliwakamata baadhi ya waumini hao pamoja na waandishi wa gazeti hili hadi walipojitambulisha na kutoa vitambulisho.
Mapema, waumini wawili nao walikamatwa baada ya kutokea mzozo na polisi huku muumini mwingine akikamatwa wakati akipiga picha askari hao.
Waumini hao waliwekwa kwenye ‘defender’ wakati mwanamke aliyekuwa akipiga picha, alinyang’anywa simu yake na kulazimishwa kufuta matukio yote aliyochukua.
Alipotafutwa kuzungumzia idadi kubwa ya askari waliokusanyika nyumbani kwa askofu huyo, Kamanda Suleiman Kova wa Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema:“Ninafuatilia... nitazungumza baada ya kukutana na viongozi wangu.”
Hata hivyo, mmoja wa askari waliokuwa katika operesheni hiyo, ‘aliitonya’ Mwananchi kuwa waliagizwa kumkamata Askofu Gwajima bila kuelezwa sababu, lakini walipata kikwazo cha kutofunguliwa mlango.
“Tumeagizwa kumkamata, lakini jamaa kagoma kufungua geti. Sasa hapa tunasubiri maelekezo, kama kuvunja mlango tuvunje tuingie na kumkamata,” alisema askari huyo aliyekuwa akizungukazunguka akiwa na bunduki.
Muda wote, askari hao pamoja na waumini walikuwa nje ya lango kabla ya kuanza kuondoka kwa nyakati tofauti na hadi kufikia saa 6:30 mchana walikuwa wameshaondoka eneo hilo baada ya kufanya mazungumzo mafupi kati ya viongozi wa kanisa, wakili Peter Kibatala na Askofu Gwajima kuahidi kwenda mwenyewe Kituo Kikuu cha Polisi.
Kwa mujibu wa watoa habari, polisi walimpa saa moja awe amefika kituoni hapo, lakini hakufika kwa muda aliopewa kutokana na foleni.
Msafara huo wa kwenda Polisi ulikuwa ni kama filamu kwani bada ya kufika Mbuyuni, gari lao liliingia kituo cha mafuta kujaza mafuta, ilipofika eneo la Victoria iliingia katika kituo cha mafuta cha Oilcom ambako Askofu Gwajima alishuka na kuzunguka nyuma ya kituo hicho na baadaye kurudi, akiwapungia mkono waandishi waliokuwamo kwenye gari la Mwananchi na kuwaonyesha ishara ya dole.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilimahewa, Richard Njeri aliyekuwepo eneo la tukio alisema kuwa jitihada za kufunguliwa lango ziligonga mwamba licha ya kugonga mlango kwa zaidi ya saa tano.
“Ninamshangaa anakataa kufungua mlango wakati mimi ndiye mwenye mtaa na ndiye mkuu wa usalama mtaani,” alisema.
Waumini wamwagika
Baada ya askari hao kumalizika kuondoka eneo hilo, waumini wake walimwagika na kufanya maombi huku baadhi wakiimba mapambio.
Baadhi walisikika wakilalamikia kutishiwa amani kwa kiongozi wao na wengine wakisema kuwa kama askari hawana la kufanya, wakapambane na matukio ya ugaidi kuliko kumfuata mtu wa Mungu.
Muumini mmoja, Julia Elisha alisema kuwa kilichofanywa na polisi ni uonevu wa wazi na huo ni uonevu kwa baba yao.
Ilipofika saa 7:20 mchana lilikuja gari la maaskofu wa Kanisa la Pentekoste ambao walitaka kufanya maombi pamoja na mchungaji, lakini hayakufanyika baada ya Askofu Gwajima kuwaambia ameitwa polisi.
Gwajima afungua lango
Ilipofika saa 7:30 mchana, lango la uzio wa nyumba ya Askofu Gwajima lilifunguliwa na akatoka na gari la rangi nyeusi. Akazungumza na wafuasi wake kuwa wasingeweza kufanya chochote kwa kuwa anahitajika polisi.
Kabla ya kuondoka nyumbani, wakili wake, Kibatala alisema kuwa anampeleka mteja wake Kituo Kikuu cha Polisi ambako alikuwa akitakiwa japokuwa hawakufahamu anaitiwa nini.
Alifika Kituo Kikuu cha Polisi, saa 9:10 alasiri alitumia dakika 10 kabla ya kutoka na kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu, akisindikizwa na polisi. Muda wote Gwajima alikuwa kwenye gari aina ya Toyota Noah.
Wakati akiwa kituoni, wafuasi wake walijazana na baadaye walihamia Mahakama ya Kisutu.
Gwajima mahakamani
Baada ya kutoka kituoni hapo, alikwenda Mahakama ya Kisutu alikosomewa mashtaka mawili; kutoa lugha chafu kwa Mwadhama Polycap Kardinali Pengo na kuacha silaha katika mikono isiyo salama, zikiwamo risasi tatu za bastola na risasi 17 za bunduki aina ya shotgun. Mtuhumiwa alikana mashitaka yote.
Ilipofika saa 9:34 alasiri, Gwajima alisomewa mashtaka na mawakili wawili wa Serikali ambao ni Tumaini Kweka na Shadrack Kimaro. Wakili Kibatala aliomba mteja wake apewe dhamana nafuu kwa kuzingatia muda, haki ya kila mtuhumiwa kupata dhamana iwapo atatimiza masharti ya dhamana na ubunifu wa mahakama katika kutenda haki kwa pande zote.
Kibatala aliiomba Mahakama hiyo kumruhusu mtuhumiwa ajidhamini na Hakimu Wilfred Byansobera alikubaliana na upande wa utetezi na kumpa dhamana ya masharti ya kutoa Sh1milioni ya ahadi. Kosa la pili amewekewa dhamana ya Sh 1milioni na Wakili Neema Masawe.
Katika kosa la pili la kutelekeza silaha, alishitakiwa pamoja na maaskofu wengine wawili na mchungaji mmoja ambao ni Yekonia Biyagaze, George Mzava, Geofrey Mumelulu, ambao inadaiwa walikutwa na bastola, risasi tatu zake tatu na nyingine risasi 17 za shortgun kinyume cha sheria.
Wote walikana kosa na kutakiwa kudhaminiwa na mdhamini mmoja kwa Sh1 milioni kila mmoja.
Awali, Wakili wa utetezi Kibatala alifanya kazi ya ziada kupangua vifungu ili wapate dhamana kwa mteja wake kwani mawakili wa Serikali walikuwa wakali kutokana na watuhumiwa kukutwa na silaha za moto ambazo ni hatari.
Wakili Kweka akinukuu vifungu mbalimbali vya sheria, alisema kuwa anaomba watuhumiwa wasipewe dhamana kwa sababu silaha walizokutwa nazo zimekuwa ni chanzo cha uhalifu unaotokea nchini, hivyo hakuna haja ya kupewa dhamana.
Akinukuu vifungu vya sheria, Kibatala alimuomba hakimu kwa mamlaka aliyonayo kuwapa dhamana kwani silaha hizo hazijasababisha madhara na mazingira yaliyotajwa kukamatwa ni usiku katika mashtaka ya kesi ya msingi haipo. Katika kesi ya pili, wameshtakiwa watu watatu ambao pia walipata dhamana. Mmoja wao hakufika kutokana na kutokuwapo taarifa kuwa wangefikishwa mahakamani.
Baada ya wateja wake kupata dhamana saa 11:57 jioni, wakili Kibatala aliwaambia waandishi wa habari kuwa kesi hiyo itatajwa Mei 4 kama ambavyo Hakimu Byansobera alisema.
Hali ilivyokuwa Mahakamani hapo
Baada ya Gwajima kupelekwa Mahakama ya Kisutu dakika 20 zilikuwa nyingi kwa waumini kujaa eneo hilo na kusababisha polisi kujihami kwa kuleta gari la maji ya kuwasha.
Hali iliendelea kuwa tulivu na waumini kutii kila walichoambiwa.
Baada ya kupata dhamana, wafuasi wake walilipuka kwa shangwe, na walipotakiwa kutoka nje ya mahakama hiyo bila ubishi walifanya hivyo na kuanza kutawanyika huku wengine wakibaki na sintofahamu baada ya kukosa usafiri na kulazimika kupanda magari yaliyokuwa yakitoka eneo hilo.
Mgongano wa Kisheria.
Wiki iliyopita, polisi ilimtaka Gwajima kuwasilisha vielelezo 10 vinavyohusu mali za kanisa, hatua iliyopingwa na kiongozi huyo akisema hatapeleka nyaraka zozote iwapo polisi hawataomba kwa maandishi.
Nyaraka alizotakiwa kuwasilisha ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia na nyaraka za helikopta ya kanisa.
Nyaraka nyingine ni muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa katika makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiyari na aambatane na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Hata hivyo, baadaye ilitolewa taarifa na Kibatala akielezea kusitishwa kwa hatua hiyo hadi hapo utatuzi wa masuala ya kisheria utakapofanyika.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment