BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS KIKWETE AWAPOZA MAKALI WAFUNGWA 400 GEREZANI KATIKA KILELE CHA SHEREHE ZA MUUNGANO.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Jakaya Kikwete akipunga mkono kuwasalimia wananchi wakati akiwasili kwenye Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam jana kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kushoto ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange. (Picha na Robert Okanda).

RAIS Jakaya Kikwete ameongoza Watanzania kuadhimisha miaka 51 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964, katika sherehe zilizofanyika jana katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kufana.


Baada ya kuwasili uwanjani akiwa kwenye gari ya wazi, akiambatana na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange, Rais Kikwete alipigiwa mizinga 21 na kwenda moja kwa moja kukagua gwaride la heshima.

Katika sherehe hizo ambazo kama ilivyo kawaida, hazikuwa na hotuba zozote zaidi ya kushuhudia gwaride na burudani mbalimbali, kwa upande wake Rais Kikwete ni za mwisho kushiriki akiwa Rais wa nchi.

Rais Kikwete ambaye anahitimisha awamu yake ya nne ya uongozi, hii ni mara ya mwisho kukagua gwaride la heshima na mara yake ya mwisho kushiriki maadhimisho ya kitaifa akiwa madarakani.

Maadhimisho yaliyobaki kufanyika kwa mwaka huu ni sherehe za Uhuru za Desemba 9, ambazo zitafanyika wakati ameshapatikana Rais wa Awamu ya Tano baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Maadhimisho ya kipekee Tofauti na maadhimisho mengine, sherehe za mwaka huu katika gwaride la heshima, gadi 13 za majeshi ya ulinzi na usalama zilipita mbele ya Rais kutoa heshima kwa mwendo wa haraka na mchakamchaka.

Miaka iliyopita, gadi za majeshi ya ulinzi na usalama zilikuwa zikipita kwa mwendo wa pole na baadaye mwendo wa haraka. Pia kwa mwaka huu, hakukuwa na maonesho ya zana vya kivita kupitishwa kutoa heshima kwa Rais.

Badala yake, maofisa watumiaji wa zana hizo, wakiwa na uwiano sawa wa wanawake na wanaume, ndiyo walipita kutoa heshima kwa Rais. Ndege za jeshi zilipita juu ya Uwanja wa Uhuru kutoa heshima.

Maonesho ya gadi za majeshi ya ulinzi na usalama, yalifuatiwa na halaiki ya watoto waliotengeneza umbo la miaka 51 ya Muungano. Watoto hao walionesha pia uwezo wa kupita kwenye kamba na kucheza ngoma za asili.

Katika sherehe hizo, watoto hao waliwataka viongozi na wananchi wote waliokuwapo uwanjani hapo kusimama kwa dakika moja kama ishara ya kupinga mauaji ya albino.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni ‘Miaka 51, tudumishe amani na mshikamano, Piga kura ya Ndiyo Katiba Inayopendekezwa na tushiriki Uchaguzi Mkuu’.

Wakongwe wafunguka Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa pande mbili za Muungano, Mabalozi na wageni wengine waalikwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, aliyekuwa Spika wa Bunge la Muungano, Pius Msekwa alisema kwa sasa wazee wanawaachia vijana jukumu la kuendelea na Muungano wa amani kwa miaka 51 ijayo.

Alisema Muungano umekuwa na changamoto kadhaa, lakini zimekuwa zikishughulikiwa na viongozi wa nchi. Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema moja ya mafanikio makubwa tangu kuasisiwa Muungano ni amani na umoja wa Watanzania.

“Tumeweza kuimarisha nchi kwa Muungano na pia tumeona uchumi ukikua kwa haraka na kuimarika kwa huduma za kijamii, tunatakiwa kujivunia kwa hilo,” alisema Butiku.

Alielezea matumaini kwamba kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa pamoja na Uchaguzi Mkuu, vitafanyika kwa amani. China yapongeza Wakati huo huo, Rais wa China, Xi Jinping, ametuma salamu za pongezi kwa Rais Kikwete kwa kusherehekea miaka 51 ya Muungano.

“Kwa niaba ya Serikali ya China na watu wa China na kwa niaba yangu mwenyewe, natoa pongezi zangu za dhati kwako wewe na watu wa Tanzania,” alisema Xi kupitia taarifa yake.

Alisema tangu kuanzishwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, serikali imekuwa katika jitihada za kupiga hatua ya mafanikio katika uchumi na maendeleo ya kijamii, jambo ambalo limechangia kiasi kikubwa amani, utulivu na utengamano wa kikanda.

“Tunafarijika na mafanikio yenu na tunawatakia mpate mafanikio makubwa zaidi ya maendeleo,” alisema. China na Tanzania zimekuwa katika urafiki wa jadi uliodumu kwa takribani nusu karne.

Rais huyo wa China alisisitiza, “Napenda kuhakikishia umuhimu mkubwa wa kuendeleza uhusiano kati ya China na Tanzania, nitaendelea kufanya kazi na wewe katika kuhakikisha uhusiano wa kirafiki wa China na Tanzania unakuwa wa kiwango cha juu na kwa faida ya hizi mbili na watu wake.

” Msamaha wafungwa Katika hatua nyingine, Rais Kikwete jana amewapa msamaha wafungwa 400 na kuwapunguzia adhabu ya moja ya sita ya kifungo wafungwa 3,729 ikiwa ni katika maadhimisho ya Muungano.

Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil, Rais amefanya hivyo kwa mamlaka aliyopewa kwa mujibu wa Kifungu 45(1) (d) cha Katiba. Taarifa hiyo inabainishwa kuwa kupunguziwa adhabu ya kifungo kwa moja ya sita ni zaidi ya utaratibu wa kawadia wa kuwaachia huru wafungwa.

Wafungwa walionufaika na msamaha huo ni waathirika wa Ukimwi, wenye TB, wenye saratani, wanaonyonyesha, wajawazito na watu wenye matatizo ya akili na walio na umri wa miaka 70 na kuendelea.

Hata hivyo, wafungwa waliohukumiwa kwa mauaji ya albino, matumizi mabaya ya madaraka, waliokutwa na dawa za kulevya na wale waliohukumiwa kwa makosa ya wizi wa kutumia silaha, waliokutwa na hatia ya kuiba nyara za serikali, majangili na waliohukumiwa kifungo cha maisha hawakupata msamaha wa rais.

Wengine waliokosa msamaha ni waliokutwa na hatia ya ubakaji na ulawiti, waliohukumiwa kifo, wizi wa magari, waliowapa ujauzito wanafunzi na waliohukumiwa kwa kutaka kutoroka gerezani.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: