MAMILIONI ya shilingi yanadaiwa kutumika katika sherehe ya kuadhimisha miaka 70 ya kuzaliwa kwa Mwenyekiti wa Kampuni ya VIP Engineering, iliyokuwa ikimiliki hisa za mitambo ya kufua umeme ya IPTL, James Rugemalira.
Shughuli hiyo inayodaiwa kufanyika nyumbani kwa mtoto wake aitwaye Eve, eneo la Makongo Juu, jijini Dar es Salaam katikati ya wiki iliyopita, iliwakusanya watu wasiopungua 70, wakiwemo watoto wake, wajukuu na baadhi ya marafiki wa familia hiyo.
Habari ambazo MTANZANIA Jumamosi imedokezwa, zinaeleza kuwa mamilioni hayo ya fedha yametumika zaidi katika vinywaji baridi na pombe kali, chakula na mapambo ambayo peke yake yamegharimu shilingi milioni nane.
Taarifa hizo pia zimethibitishwa kupitia picha zilizowekwa katika akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram inayomilikiwa na mtoto wa Rugemalira, Eve, maarufu kama Eve Collections, ambazo zimetoa taswira halisi jinsi sherehe hiyo ilivyokuwa ya kufana.
Hata hivyo, haijajulikana mara moja kiasi alichotoa Rugemalira kwa ajili ya kufanikisha shughuli hiyo, lakini mtoto wake huyo, Eve, aliandika akidai kuwa yeye ndiye aliyeandaa sherehe hiyo.
Juhudi za kumpata Rugemalira, mwanafamilia yeyote au Eve mwenyewe kwa ajili ya kuzungumzia kumbukumbu hiyo kwa sij uzi zilishindikana kutokana na kuwa kwenye shughuli nyingine ya kumbukumbu ya kifo cha mtoto wake aitwaye Isabela.
Katika siku za hivi karibuni, jina la Rugemalira limegeuka kuwa gumzo katika vyombo mbalimbali vya habari kutokana na kuhusishwa katika sakata la fedha zilizochotwa katika akaunti ya Escrow, ambazo kimsingi zilihifadhiwa baada ya kuwapo mgogoro wa malipo kati ya IPTL na mteja wake wa nishati ya umeme, Tanesco.
Rugemalira, ambaye anadaiwa kupata shilingi bilioni 130 kama mgawo wake wa fedha hizo za Escrow baada ya kuuza hisa asilimia 30 alizokuwa akizimiliki kupitia kampuni yake ya VIP Engineering, kutajwa kwake katika sakata hili la Escrow, kunatokana na umahiri wake wa kugawa kiasi cha fedha hizo kwa watu mbalimbali, wakiwemo wabunge na baadhi ya watumishi wa umma, hatua ambayo imeibua maswali mengi.
Mgawo wake huo tayari umewaweka watu kadhaa matatani, akiwemo aliyekuwa Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, aliyempatia kiasi cha Sh bilioni 1.6 kupitia Benki ya Mkombozi.
Profesa Tibaijuka alifutwa kazi na Rais Jakaya Kikwete baada ya kukiri kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rugemalira.
Wengine waliokumbwa na kadhia ya kupokea fedha kutoka kwa Rugemalira na sasa wamekutana na mkono wa sheria ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge (Sh bil 1.6), Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Victor Mwambalaswa na Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba na Sheria, William Ngeleja (Sh mil 40.4).
Rugemalira mwenyewe, akijiita ‘Father James’ amekataa kutoa maelezo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rusha (Takukuru), akisema kuwa fedha hizo ni zake, hivyo kuhoji wanachomtafutia.
Hatua yake hiyo inadaiwa kuleta shida kisheria, kwani amekuwa akisisitiza kufikishwa mahakamani na si kuhojiwa na Takukuru.
Rugemalira, ambaye anatajwa kuwa na ukwasi mkubwa, katika sherehe yake hiyo ya kuadhimisha miaka 70 tangu azaliwe, kwa jinsi ilivyoonekana kufana maandalizi yake unaweza kuyalinganisha na harusi za watu wa hadhi ya kati ambazo mara nyingi gharama yake ni kati ya milioni 20-50.
Kadi za mwaliko
Wageni waalikwa waliofika katika hafla hiyo walitakiwa kupita katika meza maalumu iliyokuwa na kadi maalumu zenye jina la Rugemalira, lakini pia na majina yao (wageni waalikwa) na zilikuwa zikiwaelekeza meza wanayotakiwa kukaa.
Mapambo
Taarifa ambazo gazeti hili limezipata zinaeleza kuwa eneo ilipofanyika hafla hiyo lilipambwa kwa maua mengi halisi ya rose na mengine mengi ya gharama ya juu, huku kukiwa na mishumaa mizuri ya kutosha iliyoongeza mng’ao wa kipekee ambapo mmoja wa watu wa karibu aliliambia gazeti hili kuwa gharama za mapambo pekee zinaweza kufikia Sh milioni nane.
Mwandaaji wa hafla hiyo, ambaye ni mtoto wa Rugemalira, Eve, aliyejaaliwa kipaji cha ubunifu, hasa wa mavazi ya kike, aliandika katika akaunti yake hiyo ya Instagram kwamba mapambo ya ndani yaliyonogeshwa na mishumaa mingi yamefanya eneo hilo kuwa na mwonekano tofauti kabisa.
Ukumbi pia ulinogeshwa na mapambo ya rangi tofauti tofauti, lakini rangi kuu iliyobeba shughuli hiyo ilikuwa ya bluu, ambayo ilibebwa zaidi kwenye vitambaa vilivyotandikwa mezani na ‘napkin’ zilizowekwa kwa ajili ya wageni waalikwa kuzitumia wakati wa chakula.
Vyakula
Vyakula vingi vilikuwa vya kukaanga, vikiwa katika aina tofauti tofauti, baadhi yake ikiwa ni kuku, ndizi, na samaki aina ya kamba.
Vingine ni wali, mboga za majani na vingine vingi, huku vikienda na vinywaji mbalimbali, ikiwemo bia aina ya Windhoek iliyowekwa sehemu maalumu na kuelezewa kama kinywaji pendwa cha mzee Rugemalira.
Inadaiwa kuwa vyakula hivyo vilivyoandaliwa na Dorkacatering vilikuwa maalumu kutokana na umuhimu wake, kwani sahani moja ya chakula iligharimu kiasi cha Sh 30,000.
Keki
Ukiacha keki kuu ya shughuli iliyokuwa na ngazi tatu na iliyokuwa imezungukwa na mishumaa, kulikuwa na keki nyingine nyingi zilizowekwa meza kuu na meza nyingine maalumu.
Wageni waalikwa
Mbali na wanafamilia ambao ni watoto, wajukuu, baadhi ya marafiki wa familia hiyo, akiwemo Ritha Paulsen, maarufu kama Madam Ritha, alialikwa kuhudhuria hafla hiyo ya kipekee ambapo pia walipata muda mzuri wa kula na kucheza ukumbini hapo.
Mbali na kuandaa hafla hiyo, Eve alimshukuru Mungu kwa kumuweka baba yao hai mpaka wakati huu ambao wanasherehekea miaka 70 ya uhai wake wakiwa naye.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / RUGEMALIRA ATEKETEZA MABILIONI YA FEDHA KATIKA SHERERE YA KUZALIWA JIJINI DAR ES SALLAM.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment