BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TAASISI ZA MUUNGANO KUIMARISHWA KWA KUJENGEWA UWEZO TANZANIA BARA NA ZANZIBAR.


Rais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohammed Shein.
RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano, itaendelea kuimarisha na kuzijengea uwezo taasisi zote za Muungano, kwa lengo la kutekeleza majukumu yake vizuri ya kuwatumikia wananchi wa pande zote mbili.

Rais Kikwete amesema hayo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, katika ufunguzi wa jengo la Makao Makuu ya Uhamiaji Zanzibar, lililopo Kilimani mjini hapa.

Amesema kuimarika kwa taasisi hizo na kufanya kazi zao vizuri, kwa kiasi kikubwa kutatoa sura halisi ya Muungano yenye lengo la kunufaisha wananchi kupitia huduma hizo.

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao kwa sasa unatimiza umri wa miaka 51 ni kielelezo pekee katika Bara la Afrika kuwa Afrika ni moja na watu wake.

“Muungano wetu ni kielelezo pekee kuwa Afrika ni moja na watu wake ni wamoja, ni Muungano wa kupigiwa mfano uliodumu kwa muda wa nusu karne huku nchi zingine zilizojaribu kuungana na kushindwa,” alisema.

Alisema kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne ni kuimarisha taasisi za Muungano ziliopo nchini na kuhakikisha zinatoa huduma vizuri kwa wananchi wake.

Alifafanua kuwa juhudi hizo zimefanyika sambamba na kurekebisha kasoro mbali mbali kwa watumishi wa Muungano na kuondoa malalamiko yaliyokuwepo awali, kwamba upande mmoja haunufaiki na ajira zinazotolewa katika taasisi za Muungano.

Kwa mfano alisema wakati Muungano unatimiza umri wa miaka 51, Serikali imefanikiwa kuboresha kanuni za utumishi wa ajira wa taasisi za Muungano, kwa lengo la kuhakikisha utumishi wao unakuwa na sura ya Muungano.

“Nimefarijika kusikia katika mchakato wa ajira upo utaratibu maalumu wa kutoa ajira kwa uwiyano kwa pande mbili za Muungano... hili jambo ni zuri sana na linatakiwa kufanywa kwa vyombo vyengine vya ulinzi vilivyopo katika Muungano,” alisema.

Awali Rais Kikwete alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano, itaboresha mazingira ya Chuo Maalumu cha Uhamiaji kwa watumishi wake, kwa lengo la kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa, wenye ufanisi kutokana na kuwepo kwa mabadiliko makubwa ya teknolojia na mbinu zinazofanywa na wahalifu katika mitandao.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: